8/31/2010

Mkutano wa Kampeni: JK afunika mkoani Mbeya ateka maelfu












Na Joachim Mushi
Mbeya
MGOMBEA nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete jana alipokelewa kwa namna ya pekee na umati mkubwa wa wanachama na wapenzi wa chama hicho katika uwanja wa Sokoine mjini hapa.
Makundi ya wanachama na wapenzi walianza mapokezi kwa kujipanga pembezoni mwa barabara wakimsubiri kutokea Wilaya ya Rungwe ambapo alifanya mkutano wa kampeni kabla ya kuja Mbeya mjini.
Akiwa njiani polisi ndio kundi lililokuwa na kazi ya kuwazuia wanachama na wananchi wengine waliokuwa wakitaka kuzuia msafara wake kuelekea uwanja wa Sokoine, wakitaka asimame kuwasalimia.
Hata hivyo mgombea huyo akiwa njiani alilazimika kusimama baadhi ya maeneo kama vijiji vya Ntokela na Uyole ya Chini kuwasalimu na kuwaomba kura wananchi.
Katika uwanja wa Sokonine alipokelewa na maelfu ya wanachama na wapenzi wa CCM, maandamano makubwa ya pikipiki na baiskeli makundi ya akinamama, vijana pamoja na vikundi mbalimbali vya burudani.
Machifu wa Mbeya walimvisha shuka, kumkabidhi mkuki, kiti kama ishara ya heshima ya uchifu na kumtakia ushindi mkubwa na uongozi bora akiingia Ikulu.
Awali akiwahutubia wananchi wa Mjini wa Tukuyu wilayani Rungwe Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, alisema Serikali kwa sasa haitakuwa ikipeleka nje tena wagonjwa wa maradhi ya moyo baada ya huduma hiyo kuanza kutolewa nchini.
“Hatupeleki mtu nje sasa kwa matibabu kama haya kama ilivyokuwa hapo awali kwani tayari madaktari wetu wanafanya kazi hizo hapa hapa…pia tunafanya mazungumzo na madaktari bingwa wengine ili kuweza kushirikiana kuboresha huduma za afya,” alisema Kikwete.
Akizungumzia uboreshaji wa huduma kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi, Kikwete alisema Serikali ya CCM kwa kuwajali wagonjwa hao imehakikisha dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs) zinatolewa bure ili kuwasaidia waathirika.
“Kama kuna wagonjwa wowote wa Ukimwi ambao bado wanauziwa dawa hizo watoe taarifa kwa viongozi wa Serikali katika maeneo yao, kwani dawa hizi zinatolewa bure kwa wahusika,” alisema Kikwete.
Hata hivyo aliwataka wana-Rungwe kuwa makini na ugonjwa wa Ukimwi kwani unaweza kuzuilika endapo watafuata mafundisho ya viongozi wa dini anuai pamoja na wale wa Serikali.
“Kuupata ugonjwa huu si kwa dharura hata kidogo maana watu wanapanga siku, muda na sehemu…mimi naongeza linguine kama yametushinda ya viongozi wa dini basi tupange na kinga ya ugonjwa huo kabla ya kwenda kwenye tukio,” alieleza Kikwete.
Kikwete, ambaye wilayani Rungwe aliongozana na wagombea ubunge majimbo ya Rungwe Mashariki na Magharibi-Profesa Mark Mwandosya na Profesa David Mwakyusa aliahidi kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Katumba kwenda Mbambo na Tukuyu.
Mwisho.

Mkutano wa Kampeni Mbeya Mjini: JK anasimikwa na Wazee wa Mbeya, akabidhiwa vifaa Vya Kazi







Chifu Mkuu wa Mbeya Chifu Mweshenga na machifu wengine wa wilaya zote Mkoani Mbeya wamemsimika Mheshimiwa Jakaya Kikwete ikiwa ni ishara ya kumkaribisha Mkoa wa Mbeya na alama ya uongozi.

Wakimsimika rasmi kama kiongozi, machifu hao wamesema ujio wa wana CCM na wananchi wengi Mkoani Mbeya ni ishara nzuri ya ushindi wa kishindo kwa CCM na Mheshimiwa Kikwete.
Chifu Mweshenga ameanza kwa kumvika shuka nyeupe ishara ya uongozi wa ki-chifu kwa mkoa wa Mbeya. Pia Chifu huyo amemkabidhi Mheshimiwa Kikwete Mkuki na kusema "Mheshimiwa wewe ni kiongozi sasa lakini pia ni mwanaume (hivyo kwa mila yetu) unatakiwa kuwa na mkuki nyumbani"

Mwisho kabisa machifu hao wa Mkoa wa Mbeya walimkabidhi Mheshimiwa Kikwete kiti cha jadi na kusema kwamba wao wanaamini kuwa mgombea huyu wa CCM atarudi Ikulu, na hivyo atumie kiti hicho kukalia na kufanya maamuzi muhimu ya uongozi.

Ujumbe huu wa Machifu uliongozwa na Chifu Mkuu Mkoani Mbeya Chifu Mweshenga, Katibu wa Machifu Mkoa Chifu Mwaluego, Chifu Kiongozi Mkoa Chifu Lioto, Chifu Mwongole na Chifu Richard Mwavipa.

Ze Original Comedy ndani ya Mkutano wa Kampeni Mbeya Mjini

Ni shangwe na burudani za hali ya juu hapa Mjini Mbeya kwenye uwanja wa Sokoine ambapo maelfu ya washabiki wa CCM wamefurika kuhudhuria Mkutano wa Kampeni ya Mheshimiwa Kikwete.
Sasa hivi walioko jukwaani ni kundi la Original Comedy na wameshaigiza nyimbo maarufu ya Komba "wembe ni ule ule", pia wameigiza "FM academia wazee wa ngwasuma, na sasa wanaimba Pembe la Ng'ombe.
Pia kundi hilo limetoa ujumbewa pongezi kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya kipindi kwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza Mgombea Urais wa tiketi ya CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Wasanii hawa wataendelea kutoa burudani mara baada ya Mheshimiwa Kikwete kuzungumza na wananchi.

Marlow aongoza wasanii wa kizazi kipya na kuwapagaisha wana CCM Mbeya Mjini

Marlow akiondoka kiduku na vuvuzela wakati akitumbuiza wana CCM na wimbo wake wa Pipi CCM remix.


Bushoke na Hafsa Kazinja (chini) nao walikuwepo kwenye kundi hilo la wasanii. Maelfu ya wana CCM waliofurika kwenye uwanja wa Sokoine waliburudika sana na nyimbo za wasanii hawa.

Vikundi mbalimbali vya wasanii vimepamba Mkutano wa Kampeni ya Mgombea Urais wa CCM Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mjini Mbeya jioni hii lakini Marlow na wimbo wake Pipi Remix CCM umefunika!
Wengine waliokwisha kutumbuiza hadi sasa ni Hafsa Kazinja, Bushoke, Inspekta Harun. Ambao wanatarajiwa kupanda kwenye stage baada ya Marlow ni kikundi cha vichekesho cha Original Comedy.

Mojawapo ya vivutio vilivyowachanganya wana CCM uwanjani hapa ni uwezo mkubwa wa muimbaji huo kuimba bila vyombo mashairi ya wimbo wake mpya ambao umetamba sana kwenye kampeni hii ya Mheshimiwa Kikwete.

"Pipi...move out of the way, hatukuja kupoteza time, tunarudi tena kwa kishindo na Jakaya ndiyo Rais. Haloo sasa tuungane tushikamane, kwa pamoja tusonge mbele CCM ni Zaidi"
Blog hii ya kampeni inasubiri maneno kamili ya mwimbo huu ambao unapatikana kwenye CD ya mkusanyiko wa nyimbo za kampeni ya CCM za wasanii wa kizazi kipya. Wasanii wengine wanaosikika kwenye albamu hii mpya ya CCM ni Mheshimiwa Temba na Chege na wimbo wao wa "Mkono mmoja CCM remix" Diamond na mwimbo wake wa "Chagua CCM" wenye midundo ya "Mbagala" na msanii maarufu kutoka nchi jirani Kidumu.

Mkutano wa Kampeni, Rungwe








Mapokezi makubwa yamemkaribisha Mheshimiwa Kikwete alipowasili Rungwe kwenye mkutano wake wa pili wa kampeni kwa siku ya leo.

Mapokezi hayo yaliambatana na mapikipiki 50 yaliyomlaki njia panda na kumsindikiza hadi kwenye eneo la mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Tandale hapa Rungwe.

Kabla ya Mheshimiwa Kikwete kuzungumza na umati huo mkubwa wa watu, wabunge wawili wa Rungwe walizungumza ambao wote ni mawaziri; Mheshimiwa Mark Mwandosya na Mheshimiwa David Mwakyusa.

Kwenye salamu zao za shukrani, mawaziri hao wawili walimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa imani yake kwao kuwapa majukumu ya kuongoza wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Naye Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea wa Urais CCM Mheshimiwa Kikwete akizungumzia mafanikio ya Chama cha Mapinduzi kwenye upande wa afya alisema yeye na Mheshimiwa Mwakyusa wamebuni mikakati mingi zaidi ya kukabiliana na Malaria ikiwa ni pamoja na kugawa vyandarua viwili kila kaya Tanzania nzima.
Pia Mwenyekiti alichukua nafasi hii kuelezea mafanikio mbalimbali ya utekelezaji wa ilani ya CCM na mengine yaliyoongezeka kwa miaka mitano ijayo.
Mwisho kabisa Mheshimiwa Kikwete aliwaombea kura madiwani na wabunge wa CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa oktoba mwaka huu.

Mkutano wa Kampeni Kyela katika Picha

Picha zote na Press Kikwete 2010

















Ratiba ya Kampeni ya Mheshimiwa Kikwete Leo - Jumanne 31/8/2010

Kampeni za Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo zimeingia siku ya kumi na moja tangu zianze.
Mheshimiwa Kikwete anatarajia kufanya Mkutano wa Kampeni wa kwanza kwa siku ya leo Kyela na baadae msafara wake utaenda Rungwe. Msafara huo unategemewa kumalizia na Mkutano wa Kampeni Mbeya Mjini.

8/30/2010

Mkutano wa Kampeni Mbalizi Mbeya Vijijini: Wanachama 367 Chadema waingia CCM

Aliyekuwa Katibu wa Chadema akionyesha kadi za chama hicho alizozikabidhi CCM baada ya kutangaza rasmi kuingia CCM akiongozana na viongozi wengine saba na wanachama wengine zaidi ya 300.



Aliyekuwa Katibu wa Wilaya ya Mbeya Vijjijini na hatimaye Katibu wa Mkoa wa Mbeya Chadema Ipyana Seme ameingia Chama Cha Mapinduzi akiongozana na wengine 366 wa CHADEMA.
Akishangiliwa na umati mkubwa wa watu uliofika kumsikiliza Mheshimiwa Kikwete, Seme alitangaza sababu kubwa tatu zilizomfanya kuhamia CCM ikiwa ni pamoja na kuchoshwa na siasa za ukabila, uongo na kufumbia macho mazuri yaliyofanywa na CCM.
“Leo naingia CCM na nimeongozana na viongozi saba ngazi ya Wilaya na jumla ya wanachama 367” Seme alisema huku akishangiliwa na wana CCM kwa vigelegele.
Viongozi waliotajwa kuingia CCM ni wale walio kwenye ngazi zifuatazo: Mwenyekiti wa baraza la wanawake mkoa, Mweka hazina wa wilaya, Mwenyekiti baraza la wazee, Mjumbe wa halmashauri kuu ya wilaya, Mshauri wa wanawake wilaya na mwenyekiti wa vijana wa wilaya.
Seme aliwatambulisha viongozi hao waliofika jukwaani na kukabidhiwa kadi zao na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea Urais Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Mwisho Seme alitoa ujumbe kwa mgombea urais kupitia Chadema “Mpelekeeni kadi hizi (za Chadema) kwenda Ikulu bado kwa Mheshimiwa Slaa….bai bai”

Mtwara waahidiwa vivuko viwili

Na Happiness Katabazi, Mtwara

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kivuko cha Kilambo kwenda nchini Msumbuji na kile Msangu Mkuu mkoani hapa vitakuwa vimeanza kutoa huduma ya usafiri.
Hayo yalisemwa leo na mgombea mwenza wa (CCM), Dk. Mohamed Gharib Bilal wakati akiwahutubia wakazi wa wilaya za Newala, Masasi na Nanyumbu mkoani hapa katika mikutano yake ya kampeni iliyofanika katika Kata ya Namionga wilaya ya wilaya ya Newala, uwanja wa SIDO uliopo katika kijiji cha Lukuledi wilayani Masasi na uwanja wa Mangaka wilayani Nanyumbu.
Dk.Bilal alisema anafahamu jinsi wananchi wa mkoa huu wanavyoteseka na ukosefu wa vivuko hivyo na ndiyo maana serikali ya CCM ilikwishatenga fedha ya kununulia vivuko hivyo na kuongeza kuwa tayari wataalamu wameishanunua vifaa vya kuunganishia vivuko hivyo na muda wowote vitaingizwa nchini kwaajili ya kuanza kuviunganisha.
“Tunawaomba wakazi wa Mtwara na wilaya zake muwe wavumilivu na mvute subira kwani ifikapo mwisho mwaka huu, vivuko hivyo vitakuwa vimeishaingia chini na kuanza kufanyakazi….na hiyo yote inatokana na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya CCM ambayo siku zote ina dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi wake,” alisema Dk.Bilal.
Mgombea huyo aliwakumbusha wananchi hao kwamba ifikapo Oktoba 31 mwaka huu, kwa amani wakipigie kura za ndiyo chama hicho ili kuweze kutwaa madaraka na kuweza kuwaletea maendeleo zaidi na kuongeza kwa kuwaomba wamchague rais Jakaya Kikwete, wabunge na madiwani wa CCM.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge wa Jimbo la Newala, George Mkuchika ambaye pia Waziri wa Habari na Utamadini, mgombea ubunge wa jimbo Nanyumbu, Danstan Mkapa na mgombea ubunge wa jimbo la Masasi Mariam Kasembe na kuwaomba wananchi hao wawapatie wabunge hapo kura za ndiyo. Jana Dk.Bilal amemaliza ziara yake mkoani hapa na leo anaanza ziara mkoani Ruvuma.

DK BILAL













1:-Dk. Bilal akizungumza na wanachi wa Wilaya ya Nanyumbu baada ya kuingia mpakani mwa wilaya hiyo na Masasi leo Agost 30 Baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara, wakiwa katika magari kwenye msafara wa kumsindikiza Mgombea Mwenza wa nafsi ya urais,

2:-Mgombea Mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal na Mama Asha Gharib, wakiingia katika uwanja wa Kijiji cha Nangaka kwa ajili ya kuhutubia wananchi wa Kijiji hicho leo Agost 30.

3,4 na 5:- Mwalimu wa Kidato cha kwanza na cha pili wa Shule ya Sekondari Lukuled, Tomoko Ada Chi, Raia wa Japan, akiwa ni mmoja kati ya wananchi wa Kijiji cha Lukuledi Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara, waliojitokeza kumsikiliza mgombea Mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akiwahutubia wananchi hao na kuwanadi wagombea Ubunge wa Jimbo la Lulindi na Bwanausi Dismas na Mariam Kasembe wa Jimbo la Masasi leo Agost 30
6:-Wananchi wa Lukuledi wakimsikiliza Dk Bilal

7:-Wananchi wa Kijiji cha Lukuledi Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara, wakimsikiliza mgombea mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji hicho leo mchana Agost 30.

8:- Wananchi wa Kijiji cha Mikangauka mpakani mwa Wilaya ya Newala na Masasi, wakimshangili Mgombea mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akipita njiani kuelekea Masasi leo Agost 30.


9:- Mgobea Mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal, akisalimiana na wananchi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Masasi, baada ya kuingia mpakani mwa wilaya hiyo na Newala, leo Agost 30.
10:-Kamanda wa Chipukizi wa Wilaya ya Masasi, Fatuma Rajab, akimvisha skafu Mgombea Mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akiingia mpakani mwa Wilaya ya Masasi akitokea Wilaya ya Newala leo mchana Agost 30.

11:- Wananchi wa Kijiji cha Mangaka Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara Jimbo la Nanyumbu, wakimsikiliza mgombea mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji hicho leo mchana Agost 30.

12:- Dk Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akitoka Wilaya hiyo kuelekea Wilaya ya Masasi leo asubuhi Agost 30.

Dk Bilal amfagilia Mkapa *Amtaja kuwa kiongozi mahiri kuwahi kuwapo Tanzania *Afafanua kuwa aliacha kasma ya mabilioni hazina

Dk Bilal amfagilia Mkapa
*Amtaja kuwa kiongozi mahiri kuwahi kuwapo Tanzania
*Afafanua kuwa aliacha kasma ya mabilioni hazina

Na Happiness Katabazi, Masasi
MGOMBEA mwenza wa nafasi ya urais kupitia CCM, Dk. Mohamed Gharib Bilal amewaambia wananchi wa Masasi kuwa, rais mstaafu wa awamu ya tatu ambaye ni mkazi wa jimbo la Masasi, Benjamin William Mkapa alikuwa ni kiongozi mahiri ambaye Tanzania imewahi kupata na akafafanua kuwa atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya Tanzania.

Dk Bilal amewahi kufanya kazi na Rais Mstaafu Mkapa wakati wa awamu ya pili, wakiwa pamoja katika Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu.

Dk Bilal aliyepo hapa Masasi akitokea Newala mkoani Mtwara anafanya mikutano ya kampeni na baada ya mkutano wake wilayani Masasi, alifanya mkutano mwingine katika wilaya ya Nanyumbu eneo la Mangaka.
Mgombea huyo mwenza alifafanua kuwa, uongozi wa Mkapa uliingia madarakani katika kipindi cha mabadiliko ya uchumi hali iliyoifanya Tanzania kuwa katika kipindi kigumu, lakini alifanya kazi kubwa katika kipindi cha utawala wake, hali iliyoifanya Tanzania kubakia na kasma ya kutosha Hazina wakati anatoka madarakani.

“Kila nikifika hapa nakumbuka majina ya viongozi mahiri waliotoka hapa. Nafahamu jambo kubwa walilolifanya kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania. Kila siku nitawakumbuka mzee Mkapa na Mama Anna Abdallah. Wote hawa wamefanya makubwa ya kuenziwa katika Tanzania,”alisema na kuongeza;

“Wana Masasi mkipigieni kura chama cha Mapinduzi kwa kuwa kinawajali na kina ilani inayotekelezeka. Tena tambueni kuwa hiki ndicho chama pekee kinachogusa maendeleo ya wanyonge.”

Awali akinadi ilani ya chama cha Mapinduzi kwa mamia ya wakazi wa wilaya ya Masasi, Mgombea Mwenza Dk. Bilal alisema, kila anapoitazama Tanzania na kukitazama chama cha Mapinduzi anakumbuka namna njema ya utumishi uliotukuka uliomo miongoni mwa wananchi sambamba na viongozi wa chama hicho.

“Ndani ya chama chetu kuna viongozi mahiri ambao wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya maendeleo yetu. Wanajituma kwa nguvu zao zote na wana hakikisha kuwa kila jambo linalotakiwa na wananchi analipatia utatuzi,” alisema.
Dk. Bilal amekuwa katika kampeni katika mkoa wa Mtwara tangu juzi na leo anaanza kampeni katika mkoa wa Ruvuma. Tangu aingie katika mikoa yaKusini, amegeuka kuwa kivutio kwa wanachi ambao mara kwa mara wamekuwa wakisimamisha a msafara wake na kumtaka awasalimu.

Mwisho.

Uwanja Mpya wa Ndege Kujengwa Songwa

Na Mgaya Kingoba, Mbeya

UWANJA wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya ambao ujenzi wake umekuwa ukisuasua, sasa unatarajiwa kukamilika Machi mwakani, wakati ndege zitakapoanza kuruka, imeelezwa.
Imeelezwa kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa uwanja huo kulitokana na kubadilishwa wazo la awali la kuwa na uwanja wa kawaida, na badala yake kujengwa uwanja wa kisasa wa kimataifa utakaohudumia watu wengi na hasa kupanua uwekezaji katika Ukanda wa Kusini.
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete alibainisha hayo leo alipowahutubia wananchi wa Mbalizi katika Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya kwenye Stendi Kuu ya Mabasi akiomba kura za wananchi ili kuongoza tena Tanzania.
Kikwete alisema wazo la awali la kujenga uwanja wa kawaida, lilibadilishwa na kuwa la kujenga uwanja wa kisasa wa kimataifa, lilibadilishwa na kuwa uwanja wa kimataifa, hivyo kazi ikabadilika na kusababisha ujenzi huo kuchukua muda mrefu kuliko ilivyopangwa awali.
“Novemba mwaka huu, kazi itakuwa imekamilika na kufikia Machi mwakani, ndege zitaanza kuruka. Zitaruka ndege kubwa za Boeing 747. Wachina wameshaanza kujenga jengo la kupokea abiria. Mbalizi itanufaika sana na ujenzi wa uwanja huu,” alisema Kikwete.
Alisema mbali ya wakazi wa Mbalizi na Mkoa wa Mbeya kunufaika na uwanja huo, pia watanufaika wafanyabiashara wa kilimo cha maua ambayo yatakuwa yanasafirishwa moja kwa moja kutoka uwanja huo wa ndege kwenda Ulaya, na hivyo maua hayo kutoharibika.
Akizungumzia upatikanaji wa maji katika mji huo wa Mbalizi, alisema kumaliza tatizo hilo, maji yatavutwa kutoka Mbeya Mjini, na kufikia Desemba mwaka huu, watapata meta za ujazo 45,000 ili kukidhi mahitaji ya mji huo na suala litakalobaki ni usambazaji wa mtandao wa maji.
Alizungumzia pia suala la umeme, akisema awamu ya kwanza itakuwa na vijiji vine na katika miaka mitano ijayo, vijiji vyote vya Mbeya Vijijini, vitakuwa vimepatiwa maji.
Akiwa amesimama katika mji wa Mlowo, aliahidi kumaliza tatizo la maji; kuhakikisha kunakuwepo na benki mjini humo; kupewa gari katika Kituo cha Polisi na kuongeza ruzuku ya pembejeo ya kilimo.
Mapema leo asubuhi, alihutubia mkutano wa kwanza katika Makao Makuu ya Wilaya ya Mbozi mjini Vwawa, ambako alisisitiza utulivu na amani nchini; kupeleka umeme vijijini na uwezeshaji wa wananchi.
Kesho Kikwete anatarajia kuzuru wilaya za Kyela, Rungwe na Mbeya Mjini.

Ratiba ya Kampeni za Mheshimiwa Kikwete Leo - Jumatatu 30/8/2010

Kampeni za Mgombea wa Urais kupitia CCM, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo zimeingia siku ya kumi na ziko Mkoa wa Mbeya. Kwa mujibu wa ratiba, Mheshimiwa Kikwete atahutubia Mkutano wa Kampeni Vwawa Wilaya ya Mbozi na kuelekea Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini. Pia Mheshimiwa Kikwete atasimama Mlowo kusalimiwa wananchi kabla hajaendelea Mbalizi.
Mheshimiwa Kikwete atafanya Mikutano wa Kampeni Mkwajuni na Makongolosi wilayani Chunya kabla hajaendelea Chunya Mjini kukutana na Wazee wa Chunya.

8/29/2010

Mkutano wa Kampeni Kate, Matai, Laela na Tunduma – JK Epukeni Vyama Vya Uchaguzi













Agosti 29, 2010


. Asema uchaguzi ukimalizika, havionekani tena


. Kulivalia njuga tatizo la watumishi kutoripoti mikoani


. Vijana wa Chadema wamshangilia, lakini…


Na Mgaya Kingoba, Sumbawanga


MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kutochagua vyama ambavyo vinaonekana wakati wa Uchaguzi Mkuu tu, badala yake wakichague chama hicho tawala kwa sababu kipo na wananchi wakati wote.

Amesema CCM imekuwa na wananchi wakati wote tangu enzi za TANU na ASP na zaidi, kimekuwa katika maeneo wanayoishi wananchi ambako wanaweza kupeleka shida zao kwa viongozi waliopo katika maeneo yao na shida hizo kutatuliwa.


Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mikutano ya kampeni ya kuomba kura kwa wananchi wa Rukwa katika maeneo ya Kate, Matai na Laela, kabla ya kuingia mkoani Mbeya alikohutubia Tunduma wilayani Mbozi na Itumba wilayani Ileje.

"Chagueni CCM, ni chama kilichoenea kila mahali, mnacho wakati wote na mkiwataka
viongozi wake mnajua wapi kwa kuwapata. Msichague vyama ambavyo mnaona wakati wa uchaguzi, na baada ya uchaguzi hamuonani tena. Hivyo ni vyama vya uchaguzi," alisema Kikwete.


Alisema CCM ni chama kilichopo wakati wote, mafanikio yake yanaonekana, kazi
iliyofanyika inaonekana na kwamba hakitoi ahadi kwa nia ya kuchaguliwa au
kuwadanganya watu.

"Tuliposema tutaleta maendeleo kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, haikuwa
ahadi ya uongo…ilikuwa ya dhamira ya dhati kutoka mioyoni mwetu, haikuwa ahadi
ya uchaguzi. Haikuwa kauli ya maneno, ilikuwa kauli ya dhamira ya dhati," alisema Kikwete anayeomba miaka mingine mitano Ikulu.


Akiwa Laela, aliwahakikishia wananchi wa mji huo kwamba serikali ya CCM italishughulikia suala la maji na tayari imeanza mipango na itachangia fedha baada ya wananchi kutoa Sh milioni sita.


Aliahidi pia kujenga lami katika miinuko mikali kwenye barabara za Nyangalua-Chome na Ilemba, na pia kuhakikisha umeme unafika katika maeneo ambayo hayana nishati hiyo kwa sasa.


Kuhusu watumishi wanaopangwa kufanya kazi mkoani Rukwa kutofika katika vituo walivyopangwa, alisema serikali italifuatilia kwa karibu tatizo hilo ili kuhakikisha mikoa ya pembezoni , haithiriki kiutendaji kwa watumishi wa umma kukataa kuripoti kazini.


Akihutubia mjini Matai, alisisitiza kuwa serikali itanunua tani 400,000 za mahindi kila mwaka nchi nzima, badala ya tani 150,000 za sasa, kwa sababu uzalishaji umekuwa mkubwa.


Aliwataka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuacha kutoa sababu alizoziita za kitoto za kushindwa kununua mahindi ya wakulima kwa madai kuwa hawana mizani za kutosha. Aliwataka wanunue haraka mahindi hayo ili yasikutwe na mvua.


Akiwa Tunduma, alikiri kuwa mji huo unakabiliwa na tatizo la maji, lakini limeanza kufanyiwa kazi ikiwemo kutengwa kwa zaidi ya Sh milioni 450, na katika miaka mitano ijayo, litamalizwa kabisa.


Kuhusu msongamano wa malori mpakani hapo yakiwa yanakwenda nchini Zambia, alisema amezungumza na Rais Rupiah Banda, na kukubaliana kuwa malori hayo yakishamaliza taratibu za forodha upande wa Tanzania, yaruhusiwe kuvuka kuingia Zambia, na hilo limekubaliwa.


Hata hivyo, katika mkutano huo uliofurika maelfu ya watu, kundi la vijana ambao baadhi yao walikuwa wameshika chupa zenye bia mkononi na wakiwa juu ya mapaa ya nyumba katika eneo la Uwanja wa CCM mjini Tunduma, walikuwa wakipiga kelele wakati mkutano huo ukiendelea.


Vijana hao walimshangilia mgombea huyo wa Urais wa CCM, lakini hawakuwa na makeke kama hayo wakati alipotambulishwa mgombea wa ubunge Mbozi Magharibi, Lukas Siyame.


Baada ya mkutano huo, vijana hao waliandamana mjini humo huku wakinyoosha juu vidole viwili vya mkononi; alama inayotumiwa na chama cha siasa cha Chadema, na baadhi yao waliwavamia watu waliovaa sare za CCM na baadhi ya magari ya watu waliofika kwenye mkutano huo.


Kesho mgombea huyo wa CCM atafanya mikutano katika Makao Makuu ya Wilaya ya Ileje mjini Vwawa na kuendelea na kampeni katika miji ya Chunya, Mbeya Mjini na Vijijini.