9/30/2010

Mkutano wa Kampeni Urambo: S. Sitta aongoza Wana Urambo, Wammwagia sifa JK

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!!
Kidumu Chama Tawala!
 
Na hivyo vingine?
Vinatuudhi!!

Hivi ndivyo wakina mama wa Urambo walivyokuwa wanaitikia mara muhamasishaji aliposema kidumu Chama Cha Mapinduzi. Ni katika shamrashamra za kumpokea Mwenyekiti wa CCM taifa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Msafara wa Mheshimiwa Kikwete umefika hapa Urambo mnamo majira ya saa nane mchana ukitokea Kaliua na Uyowa Ulyakhulu.

Akisoma mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM, mgombea ubunge wa jimbo la Urambo na Spika wa Bunge lililopita la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samuel Sitta alisema kwenye upande wa elimu miaka mitano iliyopita kulikuwa na shule mbili na sasa kuna shule 15, karibu kila kata ina shule na kata nyingine shule mbili za sekondari.

Kwa upande wa huduma ya maji vimejengwa visima 56 ambavyo vimejengwa karibu na shule za Uramboili kuhakikisha huduma hiyo inafika kwanza mashuleni. Awamu ya pili ya ujenzi wa visima hivyo, vitanjengwa kwenye maeneo ya watu na vijijini.

Akizungumzia upatikanaji wa umeme, Mheshimwa Sitta alisema kwenye kipindi cha miaka mitano ya Mheshimiwa Kikwete, umeme umefika vijiji vya Mabatini, Block Q, kuelekea Seedfarm, Mbaroni, Motomoto, kuelekea Usoke Milimani na Yelayela.

Mheshimiwa Sitta alichukua fursa hiyo kuomba huduma ya maji ya kutosha na kulingana na shughuli za kilimo za Urambo ambapo aliitaja kama kitovu cha uzalishaji wa zao la tumbaku nchini.

Mheshimiwa Sitta pia alizungumzia ujenzi wa barabara kutoka Manyoni, Itigi, kupita Urambo hadi Kigoma.

Alimalizia kwa kumuombea kura Mheshimiwa Kikwete na kuwasihi wana Urambo kutoka tarehe 31 Oktoba 2010 kwenda kupiga kura. Aliongeza, yeye kama mwanasiasa mkongwe anajivunia uongozi wa Rais Kikwete na kwamba hana mpinzani hapa Tanzania. Amelelewa vizuri na Mheshimiwa Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere.




Mwisho aliomba kura kwake yeye binafsi na kusema kwamba yeye ni chuma cha pua, na anaelekea kwenye kustaafu siasa, hivyo anaomba wana Urambo wasimuangushe. Alisihi kura hizo zisizidi za Mheshimiwa Kikwete ambazo ni 100%, alisema zake ziwe 97%.

9/29/2010

Mkutano wa Kampeni Tabora Mjini: Mapokezi ya JK yatia fora! Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi wafurika


Umati wa wananchi wa Tabora Mjini wamefurika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi leo kumsikiliza Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipofanya mkutano wa kampeni leo tarehe 29.9.2010


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Tabora Mjini kwa Mkutano wa kampeni jioni hii na kuteka umati wa watu wa Tabora.

Huu ni mkutano wake wa tatu kwa siku ya leo na kwa mkoa huu wa Tabora ambapo asubuhi alianzia Bukene, Nzega na sasa Tabora Mjini.

Mkutano wa Kampeni Nzega: JK akiri tatizo la maji Nzega, aahidi kuvuta maji kutoka Shinyanga kumaliza tatizo

Mipango imeanza ya kuvuta maji safi na salama kutoka Shinyanga ili kuhudumia wananchi wa Wilaya ya Nzega na vijiji vyake.

Hayo yamesemwa na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipowahutubia maelfu ya wananchi wa nzega kwenye mkutano mkubwa wa kampeni.

Akifafanua mpango huo mkubwa, Mheshimiwa Kikwete alianza kwa kukiri kuwa Nzega imekuwa ikisumbuliwa na tatizo hilo la maji kwa muda mrefu. "Nilipokuja mara ya mwisho niliahidi kulivalia njuga tatizo hili, na sasa mipango imekamilika ili mpate maji kutoka Shinyanga. Na hayataishia hapa, mabomba yatapita hadi Tabora Mjini" alisema Mheshimiwa Kikwete.

Ahadi nyingine alizozitolea ufafanuzi ni usambazaji wa umeme. Mheshimiwa Kikwete alisema japo Nzega Mjini kuna umeme, lakini baadhi ya vijiji bado umeme haujafika. Alisema kabla ya miaka mitano kuisha tatizo hilo litakuwa limeisha.

Mbali na umeme, Mheshimiwa Kikwete pia alisema barabara ya Nzega - Tabora Mjini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. 

Mheshimiwa Kikwete pia hakuacha kusisitiza janga la kitaifa la maradhi ya UKIMWI. Aliwaambia wana Nzega kuwa kwa sasa hapa Nzega watu 1,242 wanapata dawa za kurefusha maisha (wameathirika na maradhi ya UKIMWI). Aliwakumbusha watu wa Nzega kusikiliza ushauri wa viongozi wa dini ili kuupiga vita UKIMWI. Aliongeza ikishindikana kusikiliza mawaidha hayo, basi watumie kinga ili kuhakikisha wako salama.

Mwishoni Mheshimiwa Kikwete aliwaombea kura wagombea udiwani wa kata zote za Nzega, na baadaye kumnadi mgombea ubunge jimbo la Nzega, na yeye mwenyewe.

9/28/2010

Mkutano wa Kampeni Kahama Mjini: Wakazi wa Kahama wampa asante JK

Wakazi wa Kahama wamempa asante Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa kutekelezewa ahadi mbili kuu ambazo aliziweka na kuahidi kuzitekeleza kwa wakati.

Ahadi hizo ni ile ya kuupa hadhi mji wa Kahama ambapo tarehe 1-07-2010 Kahama iliwekwa rasmi kuwa Halmashauri ya Mji na ile ya kusambaza maji mji wa Kahama na kufanya idadi ya wakazi wanaopata maji mjini hapa kuongezeka zaidi ya mara kumi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa amemsihi Mwenyekiti wa CCM taifa Mheshimiwa Kikwete kukamilisha ujenzi wa barabara itakayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo tathmini yake imekamilika na tayari imekwisha anza kujengwa.

Akizungumza na wananchi wa Kahama, naye Mheshimiwa Kikwete alifafanua mafanikio hayo ya CCM kwenye ahadi kuu zilizoorodheshwa kwenye ilani ya CCM ya 2005.

Akizungumzia ahadi ya kusambaza maji Mheshimiwa Kikwete alisema vijiji 15 vilivyopitiwa na bomba kuu la maji kutoka Ziwa Victoria, vitaletewa maji kwenye kila kaya. Fedha zimeshatengwa ili kuhakikisha ahadi hiyo inafanikiwa.

Huduma ya umeme nayo ilizungumziwa ambapo vijiji 11 vya Kahama vitapata umeme kutokana na mradi mkubwa wa serikali wa kusambaza umeme. Umeme huo utapita kuelekea Ushirombo ambapo pana tatizo la upatikanaji wa umeme.

Kwa upande wa kilimo, Mheshimiwa Kikwete alisema aliahidi 2005 kwamba CCM itafanya mageuzi ya kilimo chini. Leo miaka mitano baadaye, safari hiyo imeanza ambapo hatua saba muhimu zimechukuliwa ili kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanafaidika na shughuli ya kilimo.

Hatua hizo ni ujenzi wa barabara ili bidhaa za kilimo zipite kwenda sokoni, usambazaji wa ruzuku ya mbegu, mbolea, dawa za mimea, utafutaji wa masoko, upatikanaji wa maji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

Kwa upande wa barabara, Mheshimiwa Kikwete alisema hata yeye anakubaliana na kilio cha wakazi wa Kahama wa kujengewa barabara yao. Alisema fedha ipo na haoni sababu ya ujenzi wa barabara hiyo kusimamishwa. Alimalizia huku umati mkubwa wa watu ukimshangilia alipotaja juu ya ujenzi wa barabara hiyo.

Mwisho aliwanadi wagombea wa udiwani na ubunge wa CCM na kuwasihi wana Kahama kuchagua CCM

Kampeni za Mheshimiwa Kikwete Leo

Kampeni za Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo zinaanzia vituo viwili ambavyo hapo jana Msafara huo ulishindwa kupitia vituo hivyo kutokana na muda.

Vituo hivyo ni Muhunze na Malampaka ambapo atafanya mikutano mikubwa ya kampeni na wananchi wa hapo kabla ya kuelekea Lyabukande, Ushirombo na Masumbwe.

Mkutano wa mwisho wa kampeni kwa siku ya leo utafanyika Kahama Mjini

9/27/2010

Kampeni za Mheshimiwa Kikwete Leo

Kampeni za Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo zimeanzia makao makuu ya Wilaya mpya ya Itirima, Lagangabilili Mkoani Shinyanga.

Baada ya hapo msafara wa Mheshimiwa Kikwete utaelekea Mwandoya jimbo la Kisesa na Mwanhuzi ambapo atafanya mikutano ya kampeni. Kituo kitakachofuata baada ya hapo ni Lalago na Mwaswa kabla hajaelekea Malampaka na Mhunze.

Mkutano wa mwisho wa kampeni kwa siku ya leo utakuwa Shinyanga Mjini.

9/26/2010

Mkutano wa Kampeni Bariadi: Mapokezi ya Kishindo kwa JK

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Bariadi Mjini kwa mkutano mkubwa wa kampeni na kulakiwa na maelfu ya wananchi wa Bariadi.

Baada ya kuwasili kwenye uwanja wa mkutano wa Sabasaba Bariadi Mjini mnamo majira ya saa 11, Mheshimiwa Kikwete alielezwa wananchi wa Bariadi wamekuwa wakimsubiri mgombea huyo wa CCM tangu saa tatu asubuhi.

Akisoma Mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2005 - 2010, Mgombea Ubunge Jimbo la Bariadi Mheshimiwa Andrew Chenge alisema kwenye mafanikio mengi hapakosi changamoto. Changamoto mojawapo ni ile ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Bariadi hadi Lamadi, ili kuunganisha Mkoa wa Shinyanga na Mwanza.

Changamoto nyingine ni maji na usambazaji wa maji safi yaliyochujwa kwa ajili ya wananchi wa Bariadi. Alimsihi Mwenyekiti wa CCM kuwafikiria wananchi wa Bariadi pindi atakapopata Urais ili kuhakikisha maji safi yanapatikana.

Akimkaribisha Mheshimiwa Kikwete kuzungumza na wananchi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa alisema wananchi wa Bariadi wana hamu kubwa ya kumsikiliza. Na kuongeza wakulima wa mkoa wa Shinyanga wametuma salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Kikwete kwa kuongeza shillingi 80 kwenye bei ya kila kilo ya pamba mwaka jana wakati wa janga la mtikisiko wa uchumi. Wakulima wa Shinyanga hawatamsahau kamwe, na wanatambua kwamba yeye ni kipenzi cha wakalima, hawatomuangusha.

Naye Mgombea wa CCM, Mheshimiwa Kikwete alianza kwa kuwapongeza wana Bariadi kwa Wilaya yao kuzaa wilaya nyingine na kuwa wilaya mbili. Alisema yote hayo ni kusogeza maendeleo karibu na watu.

Alielezea sababu kuu tatu za wanabariadi kuchagua CCM kwanza CCM ni chama makini, pili kimeongoza nchi vizuri na tatu CCM ni waaminifu, wakiahidi wanatimiza.

Mheshimiwa Kikwete alizungumzia ahadi zilizowekwa na CCM mwaka 2005 za kuendeleza na kudumisha amani nchini, upanuzi wa elimu ya sekondari, kusambaza maji safi na salama vijijini. Kwa upande wa barabara Mheshimiwa Kikwete alisema ujenzi wa barabara Maswa - Bariadi na Bariadi - Lamadi zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Suala la maji Mheshimiwa Kikwete alisema amelisikia na atalishughulikia. "Hilo la maji niachieni, nawaahadi nitahangaika nalo" alimaliza Mheshimiwa Kikwete akishangiliwa na umati mkubwa wa watu.

Mkutano wa Kampeni Magu: Wana Magu wamshangilia

Msafara wa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete umewasili Magu Mjini wilayani Magu kwa mkutano wa kampeni.

Kabla ya Mheshimiwa Kikwete kuhutubia mkutano huo, katibu wa CCM Mkoa Bwana Alhaji Mwangi Kundya, alieleza kuwa wilaya hii ina majimbo mawili ya ubunge na wagombea wote ni madaktari. Changamoto iliyopo kwenye upande wa elimu ni ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita ili watoto wa Magu nao waweze kuingia elimu ya juu kupitia shule hizo.

Kwa upande wa afya alisema changamoto kubwa ni uhaba wa waganga na wauguzi na vifaa vya tiba. Katibu huyo aliomba kwa miaka mitano ijayo, suala hili lifanyiwe kazi.

Akizungumzia tatizo jingine la upatikanaji wa maji ambayo imekuwa ni kero ya muda mrefu, katibu huyo alimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kushirikiana shirika la Umoja wa Mataifa UN Habitat ambao wameshaanza kujenga matanki kwa ajili ya kuhifadhi na kusambaza maji Wilayani Magu.

Kwenye hotuba yake ya kampeni kwa wananchi wa Magu, Mheshimiwa Kikwete alifafanua mafanikio ya CCM kwa miaka mitano na kusema yote yaliyoahidiwa kwenye ilani ya 2005 yametimizwa. Hivyo CCM ni chama cha waaminifu kikiahidi kinatimiza.

Sababu nyingine aliyowasihi wana Magu kuchagua CCM ni kwamba CCM imeongoza nchi vizuri tangia uhuru hadi sasa. Alikiri kwamba nchi yetu bado changa na inaendelea kukua, lakini tulipo sasa hivi 2010 si sawa na tulipokuwa 2005, au 2000, au hata 1961 tulipopata uhuru.

Alizungumzia pia mpango mkubwa wa usambazaji wa maji kwenye mikoa ya kanda ya ziwa kwa kushirikiana na UN Habitat, shirika la Umoja wa Mataifa.

Mwisho aliwanadi wagombea udiwani wa Wilaya ya Magu na wagombea ubunge na yeye mwenyewe kama mwenyekiti wa CCM na mgombea Urais. Aliwasihi wasifanye makosa Oktoba 2010, kuchagua Chama Cha Mapinduzi.

Mkutano wa Kampeni Nyanguge Wilayani Magu

Msafara wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi taifa na Mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia chama hicho Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete umewasili Nyanguge mchana huu.

Akishangiliwa na umati mkubwa wa watu, Mheshimiwa Kikwete amewasihi wananchi wa hapo kuchagua CCM ili iweze kuendeleza kazi nzuri iliyokwisha kufanywa na chama hicho.

Alisema anayaelewa matatizo makubwa ya wananchi wa Nyanguge ikiwemo upungufu wa maji safi na salama. Aliongeza, serikali imesha kamilisha mipango na kwa miaka mitano ijayo, shida hiyo haitakuwepo tena.

Mwishoni aliwanadi wagombea udiwani na ubunge wa eneo hilo na kuwaomba wananchi wakipigie kura Chama Cha Mapinduzi na wagombea wake wote.

Mkutano wa kampeni Ukara - Ukerewe: JK atangaza wilaya mpya ya kipolisi Ukara

Na Mgaya Kingoba, Mwanza

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ametangaza kwamba katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika ziwa Victoria hususan wilayani Ukerewe, kunaundwa wilaya mpya ya kipolisi ya Ukara.

Amesema mipango imeanza na itakamilishwa karibuni na itasaidia kukabili vitendo hivyo vya uhalifu katika Ziwa Victoria ili liwe na amani na utulivu.

Rais Kikwete aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiomba kura za wananchi wa Ukerewe katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika miji ya Ukara na Nansio wilayani humo mkoani Mwanza.

Alisema serikali inatambua kuwapo kwa vitendo vya uhalifu katika ziwa hilo na ndio maana imechukua hatua kadhaa ikiwemo pia kutoa mafunzo maalumu kwa polisi na kuanzisha doria ziwani humo.

Aidha, alisema kutafanyika utafiti kuhusu zao la mihogo kukabiliwa na ugonjwa ambao umekuwa ukiwasumbua wakulima wa zao hilo.

Kwa upande mwingine, aliahidi kununua kivuko kipya cha Nyerere kwa ajili ya wakazi wa kisiwa hicho cha Ukara.

Katika hatua nyingine, ameahidi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Magu itaendelea kuboreshwa, na atafuatilia suala la upungufu wa dawa katika hospitali hiyo.

Alikiri pia kuwa maji bado ni tatizo kubwa mjini Magu na kwamba tayari Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat), litafanikisha mradi wa maji katika mji wa Magu na maeneo ya vijijini.

Akihutubia mikutano katika miji ya Kisesa katika Jimbo la Magu na Lamadi katika Jimbo la Busega, alizungumzia pia uboreshaji wa sekta ya mifugo na uvuvi wa kisasa ili kuwezesha wavuvi kuwa na maisha bora.

Mgombea huyo wa Urais wa CCM anatarajiwa kufanya mkutano mwingine mkubwa wa kampeni mjini Bariadi.

Kampeni za Mheshimiwa Kikwete Leo

Mkutano wa kwanza wa kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi leo utakuwa Bwisya Ukara na wa pili utakuwa Nansio, Wilayani Ukerewe.

Baada ya mikutano hiyo miwili, Mheshimiwa Kikwete na msafara wake utaelekea Kisesa na Nyanguge Wilayani Magu.

Mwishoni Mheshimiwa Kikwete atafanya mikutano ya kampeni Lamadi na baadae Bariadi Mjini ambapo utakuwa mkutano wake wa mwisho kwa siku hii ya leo.

9/25/2010

Manyinyi aiteka Musoma Mjini

Na Mgaya Kingoba, Musoma

MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Musoma Mjini, Mathayo Manyinyi ameahidi kutowaangusha wananchi wa jimbo hilo na kuwataka waachane na waigizaji na kumchagua tena baada ya kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Manyinyi alishangiliwa kwa nguvu na umati wa wakazi wa jimbo hilo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Mukendo katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mgombea Urais, Rais Jakaya Kikwete, wakati akifafanua utekelezaji wa Ilani.

Bila kusoma mahali popote, Manyinyi alifafanua kila sekta ilivyohudumiwa na Chama Cha Mapinduzi katika Ilani ya 2005-2010 na katika kuthibitisha kuwa maneno yake ni sahihi, umati uliohudhuria mkutano huo ulikuwa ukimwitikia kwa sauti ya juu kila alipotaja mafanikio yake.

“Mukendo lami…Nyasho lami…Majita Road…Bweri sekondari…Baruti sekondari,” alieleza mgombea huyo anayeomba kipindi cha pili bungeni.

Manyinyi aliyataja mafanikio mbalimbali katika sekta za elimu ukiwemo ujenzi wa shule nyingi za kata; ujenzi wa barabara nyingi za lami; ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na upatikanaji wa maji isipokuwa yanahitaji kuchujwa.
 
“Mheshimiwa Mgombea Urais hapa utekelezaji wa Ilani umekwenda vizuri. Nimekuwa nikipita katika mikutano ya kampeni, nimeahidiwa kura zote ni zangu. Hapa zimenyooka kama rula,” alieleza Manyinyi.

“Sitawaangusha, msihangaike na waigizaji,” alisema Manyinyi baada ya kunadiwa na Rais Kikwete. Kwa upande wake, Rais Kikwete alimuelezea mgombea huyo kuwa ni mbunge makini, mfuatiliaji hodari na kwamba yuko sawasawa katika kazi yake.

Mkutano wa Kampeni Musoma Mjini: JK bado alia na barabara ya Serengeti

Na Mgaya Kingoba, Musoma


MGOMBEA Ubunge wa CCM katika Jimbo la Musoma Mjini, Mathayo Manyinyi ameitaka serikali ijenge haraka barabara ya Mto wa Mbu hadi Mugumu, huku Rais Jakaya Kikwete akisisitiza kuwa haitapita ndani ya Hifadhi ya Serengeti.

Aidha, Rais Kikwete amesema serikali itawashirikisha wanaopinga ujenzi wa barabara hiyo, lakini kwa sharti kwamba hawatazuia kuijenga.

Manyinyi alitoa ombi hilo kwenye mkutano mkubwa wa kampeni katika Uwanja wa Mukendo mjini hapa wakati akielezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2005-2010 jimboni humo.

Katika ombi lake kwa Rais Kikwete, Manyinyi alisema Musoma Mjini inakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa kwa sababu ya gharama za usafirishaji zinazosababishwa na ubovu wa barabara kufika mjini humo.

“Kuna tatizo kubwa la mfumuko mkubwa wa bei hapa kwa sababu bidhaa zinatoka Dar es Salaam, Tanga, Shinyanga, hivyo gharama za usafirishaji zimekuwa kubwa…tunaomba barabara ya Makutano – Loliondo hadi Mugumu ijengwe haraka,” alieleza Manyinyi.

Alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutasaidia kupunguza gharama hizo na kutoa unafuu mkubwa wa maisha kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini.

Akiomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo, Rais Kikwete mbali ya kusisitiza ujenzi wa barabara hiyo, alieleza kuwa kamwe haitapita katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Barabara hiyo itajengwa kutoka Mto wa Mbu mkoani Arusha kupita maeneo ya Ngaresero, kando ya Mlima Oldonyo Lengai, Loliondo, Clains Camp geti la Serengeti, Tabora B hadi Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara.

“Tutaijenga barabara hii, ingawa kumekuwa na maneno mengi ya upotoshaji. Haitapita ndani ya Hifadhi ya Serengeti kama baadhi ya watu wanavyodai. Kilometa
hamsini na tatu zitajengwa nje ya hifadhi,” alieleza.

“Kuna mwandishi namheshimu, juzi ameandika habari ya kupotosha ndani ya gazeti (analitaja jina), anasema barabara itapita ndani ya hifadhi. Tutafanya tathimini ya athari za mazingira na tutawashirikisha wote, lakini kwa masharti kwamba hawatazuia kujenga barabara hii.”

Akiwa Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, Ijumaa iliyopita, Rais Kikwete alisema ujenzi wa barabara hiyo una umuhimu kwa maslahi ya wakazi wa mikoa hiyo miwili ambayo haijaunganishwa kwa lami.

Hata hivyo, wanaharakati wengi wakiwa wa nje ya nchi wakiwemo wa Kenya, wanapinga ujenzi wa barabara hiyo kwa madai kwamba uhamaji wa wanyama unaojivunia hifadhi hiyo utatoweka; wanyama wengi watagongwa na kufa na Ngorongoro inaweza kuondolewa katika urithi wa dunia.

Mgombea huyo wa Urais wa CCM alimaliza mikutano yake ya kampeni mkoani Mara na kesho anatarajiwa kufanya mikutano katika miji ya Ukara, Nansio (Ukerewe); Nyanguge, Magu, Lamadi (Magu) na Bariadi (Shinyanga).

Wana- Musoma wammwagia sifa Kikwete na CCM


Wana CCM wa Musoma Mjini wakimshangilia Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini Mathayo akitoa ushuhuda wa mafanikio ya CCM mbele ya Mwenyekiti wa CCM na Mgombea Urais wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Musoma Mjini yatia fora, maelfu wafurika uwanja wa Mukendo kumsikiliza Jakaya




Mapokezi ya kishindo kwa Kikwete Musoma Mjini

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiingia kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo tayari kwa kuzungumza na wananchi wa Musoma kwa ajili ya mkutano wa kampeni.

Mkutano wa Kampeni Bunda - Wasira: Utanunuaje Urais kwa 20,000/=

Na Mgaya Kingoba, Bunda



MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Bunda, Steven Wasira amewataka Watanzania wasifanye majaribio na kubahatisha katika kuchagua urais kwa sababu mamlaka hayo ni makubwa na yanastahili kukabidhiwa kwa mtu mwenye akili timamu na chama cha maana.

 
Aidha, amehoji kwa vipi Watanzania wanaweza kununua urais kwa Sh 20,000, akihusisha na kauli ya Mgombea Urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa aliyekaririwa akisema akishinda, atafuta ada katika shule nchini.

Kwa sasa, ada kwa shule za sekondari za kutwa za serikali ni Sh 20,000 wakati elimu ya msingi hakuna ada. Kwa elimu ya chuo kikuu, serikali inatoa mikopo.


Aizungumza kwenye mkutano wa kampeni mjini Bunda mbele ya Mgombea Urais kwa tiketi ya chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, Wasira alisema urais ni mamlaka makubwa ambayo Watanzania hawapaswi kuyafanyia majaribio.


“Mwisho nataka kutoa ushauri kwa watu wa Bunda, Mkoa wa Mara na kwa Watanzania wote. Kwa mujibu wa Katiba yetu, mamlaka ya kiongozi wa serikali huchaguliwa na wananchi. Rais ni mamlaka makubwa,” alisema.


“Ndiye anayetangaza vita, kwa hiyo usiende kubahatisha, wala msifanye mambo ya kubahatisha, kujaribu. Ni lazima mchague mtu mwenye akili timamu, anayetoka chama cha maana. Mwalimu Nyerere alisema rais anaweza kutoka chama chochote, lakini Rais bora atatoka CCM.”

Huku akishangiliwa na wananchi, mwanasiasa huyo ambaye pia ni maarufu kwa jina la Tyson, alisema Watanzania ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, hawapaswi kuchagua rais wa kubahatisha, wa kudanganya na msema uongo.


“Mtu anasema atauza saruji kwa shilingi elfu tano…kiwanda anacho? Bei ya mafuta inapangwa duniani na ina uhusiano na mataifa mengine katika masuala ya uchumi, yeye atamudu vipi,” alihoji Wasira ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.


Akimnukuu tena Baba wa Taifa, Wasira alisema kiongozi huyo aliwahi kuhoji kwamba ukiona mtu mzima anasema uongo, kuna mambo mawili; kichwani kwake kuna tatizo au anawadanganya watu kwa sababu anawadharau.


Alisema ahadi hizo za uongo ni pamoja na ile ya kutoa elimu bure, akieleza kuwa kwa Tanzania elimu ya msingi ni bure, ya sekondari ni Sh 20,000 na kwa vyuo vikuu kuna mikopo inatolewa, na kutaka wanasiasa waseme ukweli.


“Unaweza kununua urais kwa shilingi elfu ishirini? Ni ukweli daima ambao utaijenga Tanzania. Yapo matatizo na tunajua hayatakwisha baada ya uchaguzi, kwa sababu tatizo moja linazaa jingine,” alifafanua Wasira.

“Matatizo hayawezi kwisha, tunachosema ni kwamba tutaweza kuondoa vikwazo ili watanzania waende kasi katika kupata huduma za jamii na kujiletee maendeleo,” alisema Wasira ambaye wakati wote akieleza hayo, Rais Kikwete alikuwa akimfuatilia kwa makini na kumshangilia.


Akizidi kupiga vijembe kwa wapinzani, Wasira alisema katika harusi zote kuna wasindikizaji, na kuwataka wananchi wa Bunda kumwamini tena na kumpa ubunge, kuchagua madiwani wa CCM na kumrejesha Ikulu Rais Kikwete.
 
Akimnadi Wasira, Rais Kikwete alisema ni mbunge mzuri, anayemwamini, mchapakazi hodari, anayejituma na anamsaidia akiwa Waziri.

Mbali ya mkutano wa kampeni mjini Bunda, Rais Kikwete alifanya mikutano Kibara (Mwibara); Mkunyu (Musoma Vijijini) na Musoma Mjini. Leo atafanya mikutano Magu mkoani Mwanza na Bariadi mkoani Shinyanga.

Mkutano wa Kampeni Kibara - Picha

 Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akifunikwa na mikono ya mashabiki wa CCM na wananchi wa Kibara, Bunda Mkoani Mara leo alipohutubia mkutano mkubwa wa kampeni mchana huu.
 Wana CCM wakiimba kumpokea Mheshimiwa Kikwete alipowasili Kibara kwa ajili ya mkutano mkubwa wa kampeni kabla ya kuelekea Bunda na Musoma Mjini.
Umati mkubwa wa wananchi wa Kibara wakimsikiliza Mheshimiwa Kikwete akihutubia mkutano wa kampeni

Kampeni za Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Leo

Msafara wa kampeni wa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo utaanzia Kibara, Mkoani Mara.

Kwa mujibu wa ratiba, baada ya Kibara Mheshimiwa Kikwete atafanya mkutano mkubwa wa Kampeni Bunda na baadaye Mkunyu.

Mkutano wa mwisho wa kampeni kwa siku ya leo utafanyika Musoma Mjini.

9/24/2010

Mkutano wa Kampeni Loliondo: JK aahidi kupunguza tatizo la maji Wilayani Ngorongoro

 Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Kikwete akimpa mkono mtoto mdogo aliyefika katika uwanja wa ndege wa Loliondo na baba yake kwa ajili ya kumpokea huku mtoto mwingine naye akijitahidi kunyosha mkono wake ili naye
 amsalimie Rais Kikwete

 Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mgombea Urais kupitia CCM akinadi sera zake kwa wananchi wa mji wa Loliondo ambao ni makao makuu ya wilaya ya Ngorongoro katika mkoa wa Arusha


Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kwa miaka mitano ijayo, serikali imenuia kumaliza tatizo la maji Ngorongoro.

Akihutubia wananchi wa Loliondo wilayani hapo, Mheshimiwa Kikwete alisema vijiji vya Malambo, Masusu, Digodigo, na vingine saba vimeanza kuhudumiwa ili kuhakikisha wananchi wa huko wanapata maji safi na salama. Mradi huu wa kuhudumia vijiji kumi kila Mkoa unafadhiliwa na Benki ya dunia.

Mipango mingine ya CCM kwa miaka mitano ijayo ni katika usambazaji wa umeme Mji wa Loliondo na ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Kikwete alisema miaka mitano iliyopita, CCM iliahidi kuongeza pesa kwenye mfuko wa barabara. Hivi sasa halmashauri ya mji wa Loliondo imeshapewa bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha barabara za halmashauri.

Akizungumzia upotoshwaji wa ujenzi ya barabara ya lami  kwenye hifadhi ya Serengeti, Mheshimiwa kikwete alisema yeye anaamini kuwa kujenga barabara ya lami maeneo yanayozunguka hifadhi ya serengeti ni wajibu wa serikali ili kuhakikisha mikoa yote inaunganishwa kwa barabara ya lami. Sehemu ya barabara hiyo itakayopita kwenye hifadhi ya serengeti, halitajengwa kwa kiwango cha lami, kama walivyoshauri wana mazingira.

Alionya wanaopotosha jitihada hizo za serikali hawaitakii Serengeti mema.

Kuhusu suala la migogoro baina ya wakulima na wafugaji, Mheshimiwa Kikwete alisema serikali ya CCM itahakikisha suluhu inapatikana. Jitihada zimeshaanza na anaamini hivi karibuni jawabu la kudumu la migogoro ya ardhi litapatikana

"Tumeagiza ardhi ya kila kijiji ipimwe, igawanywe na hati zitolewe kwa kila kijiji. Hadi sasa vijiji 37 vimeshaanza mpango huu". Alisema Mheshimiwa Kikwete.

Baada ya Mkutano huo wa Loliondo, Mheshimiwa Kikwete na msafara wake ulielekea Mugumu kwa mkutano mwingine wa kampeni.

Mkutano wa Kampeni Tarime: Wana Tarime wamkubali JK: Picha

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Tarime uliuoko katika mkoa wa Mara katika mkutano wa kampeni.


 Kijana mmoja ambaye ni mshabiki wa Chama Cha Mapinduzi katika mji wa Tarime aliamua kujichora mwili wake wote kwa rangi ya kijani na manjano wakati wa mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Mgombea wa Urais kupitia chama hicho Mheshimiwa Jakaya Kikwete akimtambulisha mgombea ubunge wa jimbo la Tarime ndugu Nyambare Nyangili wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika mji wa Tarime

Mkutano wa Kampeni Utegi: Picha





Mkutano wa Kampeni Loliondo, Ngorongoro: JK afafanua ujenzi wa Barabara ya Serengeti

Na Mgaya Kingoba, Ngorongoro

 
RAIS Jakaya Kikwete amesema hifadhi za Taifa za Ngorongoro hazitaathirika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mto wa Mbu mkoani Arusha hadi Mugumu mkoani Mara, kupitia katika hifadhi hizo.

Amesema licha ya baadhi ya watu kulalamikia ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa maslahi ya wakazi wa mikoa hiyo miwili.

Rais Kikwete aliyasema hayo mjini Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati akiomba kura kwa wananchi katika mkutano wa kampeni.

“Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusu ujenzi wa barabara hii, na kuna aupotoshaji mwingi umefanywa. Kana kwamba barabara hii itapita kwenye hifadhi, si kweli.

Tutaijenga lakini kupita katika eneo ambalo si la hifadhi,” alifafanua mgombea huyo wa Urais kupitia tiketi ya CCM.

“Bila ujenzi huo, ninyi mtabaki wenyewe na ni mikoa miwili tu ya Mara na Arusha ambayo haijaunganishwa kwa lami. Tunaipenda sana Serengeti, hatuaacha iathirike, na tutaangalia athari zote za mazingira.”

Kumekuwapo na kampeni za baadhi ya wanaharakati wakitaka barabara hiyo kutoka Mto wa Mbu kupitia Ngarasero hadi Mugumu, Serengeti mkoani Mara, isijengwe kwa kiwango cha lami kwa madai itafukuza wanyama.

Akizungumzia umeme, alisema mji wa Loliondo na vijiji viginne vya wilaya ya Ngorongoro vitapata umeme kwa kuwa kuna mradi wa kuupatia nishati hiyo na tayari mkandarasi amepatikana.

Baada ya mkutano wa Loliondo, mgombea huyo alikwenda Mugumu kuanza ziara ya mkoa wa Mara na huko anatarajiwa kuhutubia Mugumu, Shirati, Ingri Juu, Utegi na Tarime Mjini.

Kampeni za Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Leo

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameanzia kampeni zake leo mkoani Manyara, wilaya ya Ngorongoro, Loliondo.

Baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni Ngorongoro, msafara wa Mheshimiwa Kikwete utaelekea Mkoani Mara ambapo atafanya mkutano wa kampeni Mugumu na Shirati.

Kutokea hapo atasimama maeneo  ya Ingri kusalimiana na wananchi na kufanya mkutano wa kampeni kabla ya kuendelea Utegi na hatimaye Tarime Mjini.

Pia akiwa Tarime Mjini, Mheshimiwa Kikwete anatarajiwa kufanya kikazo za wazee wa Tarime, ambapo itakuwa ndio mkutano wake wa mwisho wa kampeni kwa siku ya leo, ambapo atakuwa amehutubia Mikoa ya Manyara na Mara.

9/23/2010

Mkutano wa Kampeni Makambako: JK Amnadi Jah People

Na Mgaya Kingoba, Njombe



MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Njombe Kaskazini, Deo Sanga, ameelezwa kuwa atakuwa mwakilishi mzuri wa wananchi wa jimbo hilo kwa sababu ametokana na

wananchi hao baada ya kusota nao katika dhiki.



Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo jioni katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika mjini Makambako na kumnadi mgombea huyo.



Rais Kikwete alisema Sanga ambaye ni maarufu kwa jina la Jah People, ni mtu aliyetokana na wananchi hao kwani ameishi maisha ya dhiki hadi kufika hapo alipo sasa akiwa ni mfanyabiashara maarufu mjini Makambako.



“Huyu ni mtu wa watu, mtu wa kazi. Ni mwenzenu, ni mtu aliyetokana na nyie, amepita katika dhiki hadi kufikia hapo. Atakuwa mwakilishi mzuri anayejua matatizo yenu,” alisema Rais Kikwete akimueleza Jah People.



“Ni mtetezi thabiti wa matatizo yenu. Anaweza kuwa mbunge mzuri. Namwamini, CCM inamwamini, mchagueni awe mwakilishi wenu.”



Kwa upande wake, Jah People ambaye pia aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Makambako na sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, alisema anaona kama anachelewa kuwawakilisha wananchi hao wa Njombe Kaskazini.



Akionekana mwenye furaha pengine kutokana na umati mkubwa uliojitokeza kwenye ‘uwanja wake huo wa nyumbani’, alisema “nashindwa niseme nini, mimi ni mtu wa kazi kwa vitendo.”



Aliwataka watu wa Makambako kumchagua Kikwete kuongoza tena Tanzania kwa sababu anawapenda Watanzania na amefanya kazi kubwa nzuri katika miaka mitano iliyopita.



Lakini zaidi akavigekia vyama vya upinzani na kueleza, “tusibabaike na vyama vya upinzani, havina mbele wala nyuma. Kazi yao ni matusi, hawana jipya. Tusikubali
kukipoteza chama kinachowajali watu.”



Awali, akihutubia mkutano huo, Rais Kikwete aliahidi kuwa Makambako itajengewa hospitali yake na watapata maji zaidi kwa sababu tayari kuna mradi mkubwa wa kuupatia maji mji huo maarufu.

Mkutano wa Kampeni Mbarali, Mbeya: Obama aipa chapuo Tanzania

Na Mgaya Kingoba, Mbarali

MAREKANI imesema kwamba Tanzania ni moja ya nchi inazozipigia mfano miongoni mwa nchi zinazoendelea, kwa uongozi bora na unaodumisha utawala bora na utawala wa
sheria.

Kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, Rais Barack Obama wa Marekani aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, nchini humo.

Rais Kikwete alisema wakati akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni kwenye Uwanja wa Barafu mjini Rujewa wilayani hapa katika Mkoa wa Mbeya, kuomba kura kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Alisema muda mfupi kabla ya kuhutubia maelfu ya wananchi uwanjani hapo, alizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Leonhadt, na kumuelezea jinsi Rais Obama alivyoimwagia sifa Tanzania katika hotuba yake UN.

“Kabla ya kupanda hapa jukwaani kuzungumza nanyi, mliniona nazungumza na simu…alikuwa Balozi wa Marekani, ananiuliza kama nimesikia hotuba ya Rais Obama jana usiku kwenye Umoja wa Mataifa,” alisema Rais Kikwete.

“Nikamwambia niko huku nahangaika, nitasikia saa ngapi? Wakati mwingine niko hoi bin taaban hata kusikiliza redio au televisheni huna muda.

“Ameniambia kuwa Rais Obama ameeleza misingi ya Marekani kusaidia nchi zinazoendelea, na mfano wake akatoa Tanzania. Akasema nchi yetu inaongoza kwa kujali utawala bora, utawala wa sheria, kuheshimu NGO,s, na tunatawala vizuri,” Rais Kikwete aliwaeleza wananchi.

“Kama siyo mimi na akina Mwandosya, nani mwingine anayemsifu,” alisema Rais Kikwete akimtaja Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, ambaye alikuwapo kwenye mkutano huo akiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kupitia Mkoa wa Mbeya.

Alisema kauli hizo za Marekani kuisifu Tanzania, hazitoi yeye, lakini kila anapofanya hivyo, baadhi ya watu huhoji kwani kila mara na Marekani.

“Nikisema sifa hizi zinazotolewa na Marekani, watu wanasema, ‘huyu naye na Marekani kila siku.’ Wanasema wenyewe, siyo mimi,” alifafanua Rais Kikwete.

Marekani imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania tangu Rais Kikwete aingie madarakani miaka mitano iliyopita, ikitoa ufadhili mkubwa katika miradi mbalimbali ya sekta za elimu, afya, miundombinu na nishati.

Chini ya Shirika la Milllennium Challenge (MCC), Marekani itafadhili miradi ya umeme katika mikoa sita nchini; itajenga barabara kadhaa ikiwemo ya Tunduma-Laela- Sumbawanga na hivi karibuni ilitoa vitabu 800,000 kwa ajili ya shule za sekondari nchini hasa kwa masomo ya sayansi.