9/24/2010

Mkutano wa Kampeni Loliondo, Ngorongoro: JK afafanua ujenzi wa Barabara ya Serengeti

Na Mgaya Kingoba, Ngorongoro

 
RAIS Jakaya Kikwete amesema hifadhi za Taifa za Ngorongoro hazitaathirika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mto wa Mbu mkoani Arusha hadi Mugumu mkoani Mara, kupitia katika hifadhi hizo.

Amesema licha ya baadhi ya watu kulalamikia ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa maslahi ya wakazi wa mikoa hiyo miwili.

Rais Kikwete aliyasema hayo mjini Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati akiomba kura kwa wananchi katika mkutano wa kampeni.

“Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusu ujenzi wa barabara hii, na kuna aupotoshaji mwingi umefanywa. Kana kwamba barabara hii itapita kwenye hifadhi, si kweli.

Tutaijenga lakini kupita katika eneo ambalo si la hifadhi,” alifafanua mgombea huyo wa Urais kupitia tiketi ya CCM.

“Bila ujenzi huo, ninyi mtabaki wenyewe na ni mikoa miwili tu ya Mara na Arusha ambayo haijaunganishwa kwa lami. Tunaipenda sana Serengeti, hatuaacha iathirike, na tutaangalia athari zote za mazingira.”

Kumekuwapo na kampeni za baadhi ya wanaharakati wakitaka barabara hiyo kutoka Mto wa Mbu kupitia Ngarasero hadi Mugumu, Serengeti mkoani Mara, isijengwe kwa kiwango cha lami kwa madai itafukuza wanyama.

Akizungumzia umeme, alisema mji wa Loliondo na vijiji viginne vya wilaya ya Ngorongoro vitapata umeme kwa kuwa kuna mradi wa kuupatia nishati hiyo na tayari mkandarasi amepatikana.

Baada ya mkutano wa Loliondo, mgombea huyo alikwenda Mugumu kuanza ziara ya mkoa wa Mara na huko anatarajiwa kuhutubia Mugumu, Shirati, Ingri Juu, Utegi na Tarime Mjini.

No comments:

Post a Comment