9/15/2010

Mapokezi ya mwaka kwa Mheshimiwa Kikwete Himo sasa hivi

Msafara wa Mgombea Urais wa CCM Mheshimiwa Jakaya Kikwete umepokelewa kwa kishindo kikubwa kwa maandamano ya pikipiki na magari kuanzia Kiracha, njia panda Holili nadi kwenye eneo la mkutano Himo.
Akiongea na umati mkubwa wa watu Mheshimiwa Kikwete alisema amewasili Himo kuomba kura kwani huu ni wakati wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Alichukua nafasi hiyo kuelezea mafanikio yaliyopatikana miaka mitano iliyopita kwenye utoaji wa huduma za jamii kama vile elimu, maji, afya, upatikanaji wa umeme, ujenzi wa barabara na changamoto zake.
Kwa upande wa afya na harakati za kupambana na maradhi sugu kama malaria, Mheshimiwa Kikwete alisema jitihada zilizowekwa 2005 za kugawa vyandarua kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano sasa utaboreshwa.
Kwa mwaka 2010 - 2015 mpango ni kugawa vyandarua viwili kwa kila kaya, ili kufidia yale makundi ambayo hayakuhusika na mpango wa awali. Mheshimiwa Kikwete aliongeza kuwa kama kuna nyumba ambayo haikujaliwa kuwa na mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, ina maana hawakupata chandarua. Na pia kama nyumba hiyohiyo hapakuwa na mama aliyejaliwa uzazi na kupata hati punguzo ya chandarua wakati wa ujauzito, basi mpango huu utawalenga wao.
Kwa kumalizia, Mheshimiwa Kikwete aliwanadi wagombea ubunge na udiwani wa eneo la Himo akisema, " mafiga matatu ndiyo yanayopika chakula" hivyo wana himo wachague wagombea CCM wote ili CCM iendelee kuwaletea mafanikio zaidi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Naye mgombea ubunge Ndugu Meela alimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kumnadi na kueleza kazi kubwa ya wana CCM Himo ni kuandaa ushindi wa kishindo mwezi Oktoba. Alielezea umati huo kuwa wanachama kumi wa Chadema na watano wa NCCR Mageuzi wamerudi CCM na kuahidi kushirikiana na wanachama wa CCM himo kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana.

No comments:

Post a Comment