9/17/2010

Mapokezi ya Kishindo ya Mheshimiwa Kikwete Namanga...












Msafara wa Mheshimiwa Kikwete umefika Mji wa Namanga eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya majira ya saa saba mchana.

Umati mkubwa wa watu waliofurika uwanja wa shule kumsubiri ulishangazwa kuona msafara wa magari unaingia na angani kukiwa na helikopta na hivyo kuwapagaisha wananchi waliokuwa wakishangilia kwa ngoma, na nyimbo za kusifu CCM na Jakaya Kikwete.

Msafara huo uliokuwa unatokea Longido, ulibadilisha utaratibu baada ya hali ya hewa kubadilika ghafla na hivyo kuamua kufika eneo hili kwa usafiri wa barabara.

Naye Katibu Mkuu wa CCM Wilaya Longido alielezea mafanikio ya serikali ya CCM kuwa upatikanaji wa umeme na maji safi yamepokelewa vizuri na wananchi wa kata, pamoja na sekondari ya bweni ya wasichana ambayo ni matokeo ya sera za CCM za ujenzi wa sekondari kwa kila kata.

Alielezea matarajio ya baadae ni kupanua mji wa Namanga hususan kwenye upande wa biashara ili iwe kama miji mingine kwenye maendeleo ya uchumi. Vilevile shule ya sekondari ya kata iendelezwe na kuwa shule ya kidato cha tano na sita ili wananchi wa kata ya Namanga wasitegemee tena shule za mijini kwa wanafunzi wa hapa.
Akihutubiwa wananchi wa Namanga, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea Urais wa CCM, Mheshimiwa Kikwete alisema wakazi wa kata ya Namanga wana kila sababu za kujivunia mafanikio ya sera za CCM kwa sababu yanawalenga wao.

Akizungumzia mipango ya kusambaza umeme, alisema mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kwamba kama nchi moja ina umeme hadi mpakani, hakuna sababu ya sehemu ya pili ya mpaka kutokuwa na umeme. Hivyo umeme wa Kenya ulipofika mpakani, mazungumzo yalifanyika na Rais Kibaki wa Kenya na umeme ukavutwa na kuingia Kata ya Namanga. Mheshimiwa Kikwete aliongeza kwamba muda si mrefu umeme utafika Longido na kata nyingine za jirani.

Kuhusu upatikanaji wa maji, Mheshimiwa Kikwete alisema maji limeendelea kuwa tatizo kwenye Wilaya ya Longido. Jitihada zimefanyika na sasa vimebaki vijiji vichache ambavyo maji hayajafika ambayo ni sawa na asilimia ishirini. Aliongeza ya kuwa vijiji kumi na mbili vya Wilaya ya Longido vimeingia kwenye mpango mkubwa wa kusambaza maji wa Benki ya Dunia.

Kwa upande wa afya, Mheshimiwa Kikwete alisema mji wa Namanga ni mji mkubwa na unastahili hospitali na sio Zahanati. Kwenye miaka mitano ijayo, wananchi wa Namanga wategemee upanuzi wa vituo vya afya kuwa Zahanati na Zahanati iliyopo kuwa hospitali ya wilaya ili kukidhi mahitaji ya mji mkubwa kama huu.

Matarajio mengine aliyoyaelezea ni upanuzi wa sekta ya ufugaji na kilimo ambapo mpango maalumu wa Kilimo Kwanza utahakikisha sekta hizo zinapewa kipaumbele kwenye maeneo haya.

Akizungumzia mila na desturi za wamasai na mtazamo wa wale wanaojiita wapigania haki za binadamu na za wamasai, aliwaambia wasikubali kugeuzwa vivutio vya picha kwa kuachwa vilevile walivyo. Wanaosema wamasai waachwe hivyo hivyo ni watu wabaya wasiopenda maendeleo.

Alionya kuwa mila na desturi tunaziheshimu na tutaendelea kuzienze, lakini zile zilizopitwa na wakati tuachane nazo.

"Sisi wakwere wanawake walikuwa wanatembea matiti nje, ni mila na desturi yetu, lakini tumeiacha kwa sababu haina tija" alisema Mheshimiwa Kikwete.

Aliwasihi wamasai wa Longido kuwa ni muhimu nao wasome, wakaendeshe ndege, wakafanye kazi za viwanda. Haitawezekana kufanya hivyo iwapo wataingia kwenye ndege na mgolole. "msidanganyike ndugu zangu!" Alisema.

Mheshimiwa Kikwete alichukua fursa hiyo pia kuwanadi wagombea mbalimbali wa CCM wa udiwani na ubunge. Alisema CCM ni watu waaminifu, wakichaguliwa watatimiza kama walivyofanya miaka mitano iliyopita. Alimnadi Baraka Solomon kama diwani wa Kata ya Namanga na Lekule kama mgombea ubunge, na yeye mwenyewe Mheshimiwa Kikwete kwa upande wa urais.

Baada ya Namanga, msafara wa Mheshimiwa Kikwete utaelekea Monduli, na baadaye Mto wa Mbu na Mbulu.

No comments:

Post a Comment