10/30/2010

CCM Yahitimisha Kampeni Jangwani Leo. JK awasuta wanao beza maendeleo


 Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akihutubia maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, wakati akihitimisha mikutano yake ya kampeni kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam leo jioni Oktoba 30, 2010. Uchaguzi mkuu wa Tanzania utafanyika Jumapili Oktoba 31, 2010.

Wafuasi wa CCM wakishangilia hotuba ya mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete wakati akihitimisha mikutano yake ya kampeni kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam Oktoba 30, 2010.

- Asema hakuna mchawi wakati huu!
- Asema hakuna haja ya kuiba gari la vipodozi na kujaza makaratasi ya kura, CCM itashinda tu!

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi amewashukuru wana CCM leo kwenye hutuba yake ya kufunga kampeni kwa kukipigania Chama chake na kuwaandalia mapokezi mazuri kipindi chote cha kampeni.

Amesema ametembea nchi nzima na kufanya mikutano mikubwa kwenye majukwaa 280, na ile ya kusimama njiani na ya ndani 420 nchi nzima.

Aliongeza CCM ni chama pekee ambacho kimezunguka Tanzania nzima na kuzungukia majimbo yote 330 ya uchaguzi Tanzania nzima. Alisema yeye akishirikiana na mgombea mwenza Dr. Gharib Bilal wamezunguka kote ambako mmoja wao alishindwa kutembelea, mwingine alisaidia. Alisisitiza kuwa kuna baadhi ya maeneo mengine nchini ambapo yeye na mgombea mwenza walipita na kufanya mikutano mikubwa ya kampeni.

Akimshukuru Mama Salma kwa kuendesha kampeni kubwa kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Kikwete alisema Mama Salma ameonyesha ujasiri mkubwa na uwezo mkubwa wa kunadi sera za chama chake.

"Japo wapinzani hawakupenda jitihada hizo, lakini wao wengine hawana wake (hawajaoa), wengine wanataka kuingia Ikulu na "ma first lady" wa wenzao (wake za watu). Nasema Mungu atunusuru na viongozi kama hao". Alisema Kikwete huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliofurika viwanja vya Jangwani.

Mheshimiwa Kikwete alichukua nafasi hiyo pia kuelezea wana CCM na wananchi waliohudhuria mkutano huo mkubwa kuwa wakati anazunguka mikoani, aliwaeleza wananchi sera na malengo ya CCM na wao walikubali na kumuhakikishia watachagua tena CCM iendelee kuongoza.

Mwishoni Mheshimiwa Kikwete aliwaomba Watanzania wote kupitia mkutano huo wachague Chama Cha Mapinduzi kwani ni waaminifu na wanatoa ahadi zinazotekelezeka. "Hakuna chama kingine kama CCM" alisema.

"Mzee Mkapa ameeleza maneno ya busara, uchaguzi huu usitugawe...wanataka kuingia Ikulu kwa ngazi ya maiti za Watanzania? Tuwaepuke viongozi hao. Msiwasikilize, achaneni nao" Kikwete alisisitiza.

Aliahidi Watanzania kuwa yeye na Dkt Bilal wakichaguliwa, watatumia uzoefu wao wa miaka mingi kwenye utumishi wa umma, kulinda amani na utulivu, na kuendeleza maendeleo ya taifa la Tanzania.

Alisisitiza serikali yao itajali maslahi ya watu wote, wenye ulemavu, watoto, vijana, wazazi, wazee na watu wa matabaka yote. Kama serikali ya CCM inavyovyofanya sasa. Pia aliwasihi Watanzania wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi kwani ni haki yao ya msingi na ya kikatiba.

No comments:

Post a Comment