7/16/2010

Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Bungeni Leo

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIAGANA NA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, DODOMA, JULAI, 2010

Mheshimiwa Spika,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kuishuhudia siku hii ya kihistoria ambapo Bunge la 9 linamaliza kipindi chake cha miaka mitano. Nimekuja hapa kutimiza wajibu wa Kikatiba wa kuhitimisha shughuli za Bunge hili ili kufungua njia kwa mchakato wa uchaguzi wa kupata Wabunge na Rais kwa kipindi kijacho kuanza rasmi.



Mheshimiwa Spika,
Katika kuagana na Wabunge wa Bunge lako Tukufu, ambalo nami ni sehemu yake, ninayo mengi ya kushukuru, na ninao wengi wa kuwashukuru na kuwapongeza. Wa kwanza, ni Watanzania wenzangu wote, walionipa fursa hii adhimu ya kuwatumikia katika nafasi hii ya juu kabisa ya uongozi wa nchi yetu. Nawashukuru kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu, kwa Serikali yangu na kwa Bunge letu tukufu katika kipindi chote hiki cha miaka mitano. Nawashukuru pia kwa kutimiza wajibu wao wa kiraia wa kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuijenga nchi yetu. Natambua na kuthamini uvumilivu na uelewa wao wakati nchi yetu ilipokuwa inapita katika vipindi vigumu. Nawashukuru sana kwamba hata wakati huo, Watanzania wenzangu wameniunga mkono, wameiunga mkono Serikali yetu na kutusaidia. Asanteni sana.



Pili, napenda kuwashukuru viongozi wenzangu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali na mashirika yake. Napenda kuwatambua kwa ajili hiyo, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein; Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume; Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda; Waziri Mkuu aliyemtangulia Mheshimiwa Edward Lowassa na Waziri Kiongozi, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha. Aidha, nawashukuru Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Ndugu Phillemon Luhanjo, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wengine waandamizi na wafanyakazi wengine wa umma wa ngazi zote. Msaada wao, ushirikiano wao na uchapa kazi wao ndivyo vilituwezesha kupata mafanikio tunayojivunia leo.


Tatu, Mheshimiwa Spika, natoa shukrani kwako na Wabunge wa Bunge lako Tukufu. Nakushukuru wewe kwa uongozi wako mahiri. Nawapongeza Wabunge wote kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kuwawakilisha wananchi waliowachagua. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu kwangu na kwa Serikali yetu. Bunge letu limekuwa kielelezo kizuri cha ustawi wa demokrasia nchini. Mmetoa hoja nyingi nzuri za kukosoa na kuishauri Serikali. Ingawaje kuna baadhi ya nyakati maneno yalivuka mipaka ya staha, lakini, napenda kuamini kuwa ilikuwa ni kwa nia njema! Isitoshe elimu haina mwisho na wakati mwingine kukosea ndiyo kujifunza.
Shukrani zangu za mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu, ziwaendee wakuu wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na wanajeshi na watumishi wote wa vyombo hivyo. Tunamaliza nchi yetu ikiwa salama: mipaka iko salama na usalama wa maisha na mali za raia ni wa uhakika.


Changamoto na Mafanikio
Mheshimiwa Spika,
Nilipokuja kuzindua Bunge hili tarehe 30 Disemba 2005, nilielezea na kufafanua kwa kina dira, mwelekeo na malengo ya Serikali ya Awamu ya Nne. Niliahidi kwamba Serikali yangu ingeongozwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ilitoa majukumu mahsusi kwa Serikali kufanya. Kupitia kwenu, Waheshimiwa Wabunge, niliwaahidi Watanzania mambo kumi yafuatayo katika miaka mitano ya Serikali yetu. Naomba kwa ruhusa yako, Mheshimiwa Spika, niyakumbushe mambo hayo:

1) Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa;

2) Serikali ya Awamu ya Nne itadumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi leo;

3) Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi, tena kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya;

4) Serikali ya Awamu ya Nne itatimiza ipasavyo wajibu wake wa utawala na maendeleo, na itaendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu;

5) Serikali ya Awamu ya Nne itaimarisha uwezo wake wa kulinda maisha na mali za raia wake. Tutapambana na uhalifu wa kila aina, na majambazi hayataachwa yatambe yatakavyo;

6) Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha mipaka ya nchi yetu ipo salama. Hatutamruhusu mtu au nchi yeyote kuchezea mipaka ya nchi yetu na uhuru wetu;

7) Serikali ya Awamu ya Nne itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania ina mahusiano mazuri na mataifa yote duniani, pamoja na mashirika ya kimataifa na kikanda;

8) Serikali ya Awamu ya Nne itajali sana maslahi na mahitaji ya makundi maalum katika jamii kama vile wanawake, vijana, watoto, wazee, walemavu na yatima;

9) Serikali ya Awamu ya Nne itaongoza mapambano mapya ya kuhifadhi mazingira ili vizazi vijavyo virithi nchi nzuri, na msingi imara wa maendeleo endelevu; na

10) Serikali ya Awamu ya Nne itaendeleza michezo, na shughuli za utamaduni na burudani.

Mheshimiwa Spika;
Leo, naona fahari kusema kuwa tumepiga hatua kubwa katika kutekeleza malengo yetu hayo. Tumefanikiwa pia mambo mengine mbalimbali tuliyoahidi katika ilani ya Uchaguzi ya Chama tawala au kujitokeza kwa nyakati au mahali mbalimbali. Viwango vya mafanikio vinatofautiana kwa kila sekta, hata hivyo, tumesonga mbele kwa kasi ya kuridhisha, japo bado tuna safari ndefu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania.


CHANGAMOTO TULIZOKABILIANA NAZO
Mheshimiwa Spika;
Ninapoangalia mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi hiki na kulinganisha na changamoto tulizokabiliana nazo, huwa nastaajabu na kujiuliza tumewezaje? Mimi siyo Sheikh na wala siyo mwanazuoni wa dini yangu. Ni mcha Mungu wa kawaida tu hivyo naamini kuwa ni rehema za Mwenyezi Mungu ndizo zilizotuwezesha kupata mafanikio tunayojivunia sote hii leo.
Kama mnavyojua tulianza kazi, nchi ikiwa katikati ya ukame mkubwa wa aina yake kutokea tangu uhuru. Kukawa na upungufu mkubwa wa chakula, takriban watu wapatao 3,776,000 walipatiwa chakula na Serikali. Ukame huo pia ulikausha maji katika mabwawa yetu ya kuzalisha umeme hivyo kukawa na upungufu mkubwa wa umeme na tukalazimika kukodi vinu vya kufua umeme kutoka nje.


Mheshimiwa Spika;
Kuanzia katikati ya mwaka 2007, bei za mafuta zilipanda kwa kasi sana na ilipofikia Juni, 2008 bei zilifikia kiwango cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa duniani. Mafuta yanagusa nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Hivyo gharama za usafiri, uchukuzi, uzalishaji mashambani na viwandani na utoaji wa huduma mbalimbali zikapanda. Hali hiyo ilisababisha mfumuko wa bei na gharama za maisha kupanda sana nchini.
Katika nusu ya pili ya mwaka 2008, dunia ikakumbwa na tatizo jingine kubwa la machafuko katika masoko ya fedha na mitaji yaliyosababisha kudorora kwa uchumi wa dunia. Kudorora kwa uchumi wa dunia kulisababisha bidhaa zetu tunazouza nje kukosa masoko na bei zake kuporomoka sana na kuwatia hasara kubwa wazalishaji na wafanyabiashara wetu. Watalii kutoka nje wakapungua, wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza nchini waliahirisha kufanya hivyo. Utulivu wa uchumi wetu ulianza kuyumba. Ukuaji wa uchumi ukashuka, mfumuko wa bei ukapanda sana, mapato ya Serikali yakawa chini ya lengo, n.k. Ili kulinusuru taifa, Serikali ikalazimika kutengeneza mpango wa dharura wa kuunusuru uchumi ambapo shilingi trilioni 1.7 zilitumika. Hatua hiyo ndiyo iliyosaidia kupunguza makali ya athari za kudorora kwa uchumi hapa nchini.


Mheshimiwa Spika;
Wahenga walisema “kila msiba una mweziwe”. Katika baadhi ya mikoa hasa ile inayopakana na Kenya miaka ya 2008 na 2009 ilikumbwa na ukame mkali uliosababisha hata mifugo na wanyama pori wengi kufa na watu wake kuwa maskini na kukabiliwa na njaa kali. Serikali iliwapelekea chakula cha msaada na sasa tunaangalia namna ya kuwasaidia waanze upya maisha. Kule Kilosa na Mpwapwa kwa sababu ya mvua kubwa Mkoani, Dodoma, Desemba, 2009, sehemu nyingi za reli ya kati zikasombwa na maji na ilituchukua miezi sita mpaka treni zilipoanza tena kazi.
Matatizo yote hayo niliyoyataja yamekuwa na athari kubwa kwa ukuaji na ustawi wa uchumi wa nchi yetu. Umeturudisha nyuma kwa kiasi kikubwa kwani kama athari hizo zisingekuwepo tungekuwa tumefikia malengo yetu mengi na hata kuyavuka. Hata hivyo, tumepata mafanikio ya kutia moyo kwenye nyanja mbalimbali, jambo linalothibitisha kuwa sera zetu za uchumi ni sahihi kwani uchumi wetu umeweza kujenga kiwango kizuri cha kuhimili misukosuko mikubwa kama hii tuliyokumbana nayo.


HALI YA SIASA
Umoja na Amani
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imeendelea kuwa nchi tulivu, yenye amani na usalama na watu wana umoja licha ya tofauti zao za dini, makabila, rangi na ufuasi wa vyama vya siasa. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kulinda, kuendeleza na kuimarisha sifa hii ya nchi yetu. Nawashukuru sana Watanzania wote kwa kuelewa na kutambua kwa haraka na kuepukana na vihatarishi vya amani na umoja wa nchi yetu. Nawashukuru na kuwapongeza kwa kuwapuuza wale wanaotaka kuigawa nchi yetu kwa misingi ya udini, ukabila, Ubara na Uzanzibari na Upemba na Uunguja.


Muungano
Mheshimiwa Spika,
Umoja wa taifa letu una sura mbili. Kwanza, ni umoja baina ya Watanzania wa makabila, rangi na dini zote. Pili, ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano wetu umeendelea kuwa imara. Katika miaka mitano hii tumechukua hatua mahsusi za kuimarisha Muungano na mshikamano wetu. Tumeimarisha Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kumteua Waziri maalum katika ofisi hiyo kushughulikia masuala ya Muungano. Tumeboresha taratibu za majadiliano ya masuala ya Muungano kwa kumfanya Makamu wa Rais kuwa Mwenyekiti wa kikao cha pamoja cha Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi cha kujadili masuala ya Muungano. Vikao vitano vilifanyika na mambo mengi yalizungumzwa na kupatiwa ufumbuzi. Aidha vikao 75 vya ushirikiano kwa sekta zisizo za Muungano pia vilifanyika.


Mpasuko Zanzibar
Mheshimiwa Spika,
Siku ile ya tarehe 30 Disemba, 2005 nilieleza kusononeshwa kwangu na mpasuko wa kisasa uliopo Zanzibar. Niliahidi kufanya kila niwezalo ili hali hiyo ibadilike na Wazanzibari wawe wamoja, waishi kwa upendo, amani na utulivu. Bila ya shaka mtakubaliana nami kwamba tumefika mahali pazuri na ishara njema zinaonekana. Napenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wenzangu wa Chama cha Mapinduzi na wenzetu wa CUF kwa kukubali vyama vyetu vizungumze.
Nawashukuru na kuwapongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF kwa maridhiano yao ya tarehe 5 Novemba, 2009. Maridhiano hayo yamefungua njia ya kuwezesha kutekelezwa kwa makubaliano ya vyama vyetu. Nawapongeza kwa dhati Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kukubali kura ya maoni ifanyike ili wananchi wa Zanzibar waamue kuhusu kuundwa kwa Serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Naendelea kuahidi ushirikiano wangu na msaada wangu pale unapohitajika. Nawasihi ndugu zangu Wazanzibari tuitumie vyema fursa hii ya kihistoria kuzika siasa za uhasama na kushupaliana zilizowagawa wananchi katika makundi ya uadui, na badala yake Wazanzibari wawe watu wamoja, wanaoishi kindugu na kwa kushirikiana.


Demokrasia Imestawi
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imeendelea kuwa kielelezo kizuri cha utulivu wa kisiasa na ukomavu wa demokrasia barani Afrika. Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuhakikisha kwamba uhuru wa kisiasa, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kuabudu unaheshimiwa na kulindwa. Tumehakikisha kwamba wanasiasa pamoja na vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali na wananchi wote kwa ujumla wanafaidi haki zao za msingi.
Tumefanya jitihada ya kuhakikisha kwamba uwanja wa ushindani wa kisiasa unakuwa sawia zaidi. Kwa ajili hiyo, tumefanya Marekebisho ya Sheria zetu za Uchaguzi na tumetoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye madiwani kuanzia mwaka 2007. Sasa hivi chama kisichopata ruzuku ni kile tu ambacho kimeshindwa kupata hata diwani mmoja. Hali hii imedhihirisha ukomavu wa kisiasa nchini.


Mapambano Dhidi ya Rushwa na Maadili ya Uongozi
Mheshimiwa Spika,
Ahadi yangu ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka nchini tumeitimiza. Tumekemea vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na kuchukua hatua za kisheria na za kinidhamu kwa wahusika pale ilipobidi kufanya hivyo. Tumetunga Sheria mpya na kali zaidi na tumepitisha mkakati mpya wa kupambana na rushwa. Tumeunda upya chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU). Sasa TAKUKURU ina ofisi katika kila wilaya na tumeiongezea uwezo wa kibajeti na rasilimali watu na vitendea kazi.
Juhudi hizo, zinadhihirisha utashi mkubwa wa kisiasa tulionao wa kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Kwa sababu hiyo, katika miaka mitano hii, tuhuma nyingi zimechunguzwa, kesi nyingi zimefikishwa Mahakamani ikiwa ni pamoja na zile za rushwa kubwa. Mapambano bado yanaendelea. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumepeleka Mahamani kesi za rushwa 780. Idadi hii ni kubwa kuliko kesi zote za rushwa zilizopata kupelekwa Mahakamani katika kipindi cha miaka 20 kabla ya hapo, ambazo zilikuwa 543. Kati ya kesi hizo 780 Serikali imeshinda kesi 160. Katika kipindi cha miaka 20 kabl a ya hapo (yaani kuanzia 1985 – 2005) Serikali ilishinda kesi 58 tu. Mapambano bado yanaendelea.


Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeimarishwa kiutendaji na kisheria. Mwaka 2008, Bunge lako tukufu lilitunga Sheria mpya inayotoa uwezo na uhuru mkubwa zaidi wa kutenda kazi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na ofisi yake.
Nilianzisha utaratibu mpya wa viongozi na watendaji wakuu wa Wizara, Halmashauri za Wilaya na Miji, Idara za Serikali na Wakala mbalimbali, kusoma na kujadili taarifa za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu maeneo yao na kuchukua hatua za kurekebisha kasoro alizozigundua. Utaratibu huu unazifanya taarifa hizo ziwe na thamani na imesaidia kuleta ufanisi wa hesabu za Serikali. Siku hizi wanaopata hati chafu wamepungua sana.


Mheshimiwa Spika;
Nampongeza sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ofisi yake kwa kazi nzuri wanayofanya. Nampongeza pia kwa uamuzi wa kufanya ukaguzi wa thamani ya fedha kwa maana ya kulinganisha fedha iliyotumika na kazi iliyofanyika. Hii ni hatua muhimu itakayosaidia kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika vizuri na kwa shughuli iliyokusudiwa.
Katika kipindi hiki pia tumeanza utaratibu mzuri wa kuwawajibisha wale wote wanaohusika na wizi na ubadhirifu wa fedha za umma mara unapogundulika na wakaguzi. Tofauti na zamani ambapo hatua husubiri baada ya taarifa ya ukaguzi kuwasilisha Bungeni. Hatua hii itasaidia kujenga nidhamu na kunusuru fedha nyingi za umma zinazoibiwa na kutumiwa vibaya.
Tumejitahidi kusimamia vyema Sheria ya Manunuzi ili kupunguza mianya ya rushwa katika manunuzi ya Serikali na hasa mikataba. Tumefanya mapitio ya Sheria hiyo na kuainisha maeneo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ili kuboresha usimamizi na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika sekta za umma. Nasikitika kwamba kwa sababu ya ufinyu wa muda haikuwezekana Sheria hiyo kujadiliwa na kuamuliwa katika Bunge hili. Ni makusudio yetu kuiwasilisha mapema Bunge lijalo litakapoanza kazi.


Maadili ya Uongozi
Mheshimiwa Spika,
Niliahidi kulipa msukumo mpya suala la maadili ya uongozi. Tumeruhusu mijadala ya wazi miongoni mwa wananchi, vyombo vya habari, taasisi zisizo za kiraia, na hata hapa Bungeni, kuhusu maadili ya uongozi wa umma.
Tumeimarisha Tume ya Maadili ya Viongozi, kwa kuijengea uwezo zaidi wa kisheria na kifedha. Tume ya Maadili ya Viongozi sasa ina mamlaka siyo tu ya kupokea fomu za mali walizojaza viongozi bali pia ina uwezo wa kuhakiki mali hizo ili kuthibitisha ukweli wa taarifa zinazotolewa kila mwaka.
Tumebadilisha utaratibu na kuamua kwamba mali za familia za viongozi nazo zijumuishwe kwenye fomu na pia zikaguliwe. Kwa kufanya hivyo viongozi wasio waadilifu watapata tabu kuficha mali zao. Naamini, tukiendelea na mwenendo huu, maadili ya viongozi wetu yatakuwa yamejengewa msingi mzuri.


Mheshimiwa Spika,
Niliahidi kwamba tutatafuta utaratibu wa kudhibiti mapato na matumizi ya fedha katika uchaguzi ili uongozi usiwe bidhaa ya kununuliwa. Tayari Sheria ya Kudhibiti Gharama za Uchaguzi imepitishwa na Bunge lako Tukufu na itaanza kutumika katika uchaguzi wa mwaka huu. Mimi naamini kwamba, pamoja na upya wake itasaidia kupunguza na hata kukomesha vitendo vya rushwa katika uchaguzi, iwe wa ndani ya vyama vya siasa au nje miongoni mwa umma. Tuko tayari kufanya marekebisho yoyote yatakayojitokeza katika utekelezaji kwa nia ya kuiimarisha. Aidha, mchakato wa kutenganisha shughuli za biashara na siasa unaendelea na utakamilika mapema katika uhai wa Bunge lijalo.


Utawala Bora
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumefanikiwa kuimarisha utawala bora katika utendaji kazi wa serikali. Tumeendesha shughuli za serikali kwa kuheshimu mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mikuu ya dola, yaani, Bunge, Mahakama na Utawala. Sisi katika Serikali tumeendelea kutimiza wajibu wetu wa uwezeshaji kwa mihimili hiyo.


Bunge
Mheshimiwa Spika,
Kama mtakavyokumuka Mfuko wa Bunge tayari umeanzishwa kama yalivyo matakwa ya Katiba ya nchi yetu. Bajeti ya Bunge tumendelea kuiongeza na sasa ni mara mbili ya ile iliyokuwepo mwaka 2005. Maslahi ya Wabunge nayo yameboreshwa. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo umeanzishwa ili kuwawezesha Wabunge kushughulikia matatizo madogo madogo yanayowakabili wananchi wao.
Mazingira bora tuliyoyajenga yameliwezesha Bunge letu katika miaka mitano hii kufanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na ufanisi mkubwa zaidi na limekuwa kielelezo kizuri cha ustawi na ukomavu wa demokrasia nchini mwetu. Katika kipindi hiki, changamoto zilizojitokeza katika utendaji na mahusiano baina ya mihimili hii mikuu ya dola tumezitatua kwa maelewano yanayozingatia maslahi ya taifa. Huu ni uthibitisho kuwa demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria unaendelea kuota mizizi.


Mahakama
Mheshimiwa Spika,
Uimara na ufanisi wa mahakama zetu na vyombo vingine vya kusimamia haki ndiyo msingi wa amani ya nchi yetu. Ni, ukweli ulio wazi kuwa amani na utulivu hustawi kama haki inatendeka na inaonekana kutendeka kwenye jamii.
Tumetimiza ahadi yetu na wajibu wetu wa kuiwezesha Mahakama kufanya shughuli zake kwa ufanisi zaidi. Mahakama imendelea kuwa huru na kamwe Serikali haikuiingilia Mahakama katika kazi zake. Tumeongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na Mawakili wa Serikali, na nafurahi kwamba tumezingatia uwakilishi wa kijinsia. Katika kipindi hiki pia nimeteua Majaji wapya 12 wa Mahakama ya Rufani kati yao 4 wakiwa wanawake na Majaji 51 wa Mahakama Kuu, wanawake wakiwa 24. Tumeajiri Mahakimu Wakazi 256 wanawake wakiwa 117 na Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo 394 kati yao 134 ni wanawake. Majaji na Mahakimu wanawake wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu. Hii ni kutekeleza ahadi yangu na ya Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za maamuzi. Kwa jumla kitaifa tumefikia asilimia 31 kutoka asilimia 26 mwaka 2005. Hii leo tuna wanawake wengi katika nafasi za Ubunge, Uwaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Watendaji n.k. Nafurahi na kushukuru kwamba wanawake hawa wengi hawajaniangusha. Wanachapa kazi vizuri.


Mheshimiwa Spika;
Tumeendelea kuboresha bajeti ya Mahakama ingawaje bado kiasi kinachotengwa ni kidogo ukilinganisha na mahitaji. Tumeboresha maslahi ya Majaji na Mahakimu na tunakusudia kufanya zaidi siku za usoni. Hivi sasa tunaendelea na mchakato wa kuiwezesha Mahakama nayo kuwa na Mfuko wake Maalum, kama inavyotaka Katiba ya nchi.


Utendaji Serikalini
Mheshimiwa Spika,
Ufanisi wa utendaji wa Serikali unategemea kuwepo kwa rasilimali watu wenye ari ya kuchapa kazi na wenye vitendea kazi stahiki. Katika hotuba yangu ya kufungua Bunge Desemba 30, 2005 nilielezea pia kwamba tutachukua hatua za kuboresha mishahara na maslahi yao kwa ujumla. Tuliunda Tume maalum ambayo ilitupatia mapendekezo kadhaa. Tumekuwa tukiyafanyia kazi mapendekezo hayo na kuyatekeleza kulingana na uwezo wetu wa kibajeti.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumewapandisha vyeo watumishi 140,797 ambao hawakuwa wamepewa haki yao hiyo kwa muda mrefu. Tumelipa fidia ya stahili za watumishi kwa gharama ya shilingi bilioni 108. Aidha, Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 45.1 kulipia malimbikizo na madeni yote halali ya walimu; walimu wa shule za msingi shilingi 32.2 bilioni na sekondari shilingi 12.9 bilioni. Kuna rufaa za madai ya walimu yapatayo shilingi bilioni 6 ambazo zinaendelea kushughulikiwa na Kamati ya Maofisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Uchumi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Katika kipindi hiki pia tumepandisha kima cha chini cha mshahara ya watumishi wa umma kutoka shilingi 65,000 mpaka shilingi 135,000 sawa na ongezeko la asilimia 107. Ahadi ya kuendelea kuongeza iko pale pale. Tumeboresha mafao ya uzeeni kwa watumishi wa Serikali kwa kuhuisha ukokotoaji wa mafao ya LAPF na PSPF na kuboresha ukokotoaji wa mafao ya Mfuko wa PPF.


Mheshimiwa Spika;
Tumeboresha utendaji wa Halmashauri zetu kimuundo, kifedha na kiutumishi ili ziweze kuchochea kasi ya maendeleo ya watu wetu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumeongeza ruzuku kwa Halmashauri kwa zaidi ya mara tatu kutoka shilingi bilioni 780 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 2,728 mwaka huu. Tumeajiri wahasibu 795; wakaguzi wa ndani 447; maafisa kilimo na mifugo 455; wahandisi wa maji 95; na watumishi wa kada mbalimbali za afya 6,437. Watumishi hawa na ruzuku tunayotoa imechangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Kazi ya kuboresha utendaji wa Halmashauri bado ipo kubwa mbele yetu na hasa ile ya kuzuia wizi na ubadhirifu. Tumeanza Awamu ya Pili ya Maboresho ya Serikali za Mitaa na ni matumaini yangu kuwa suala hilo litapewa uzito unaostahili.


Ulinzi na Usalama
Mheshimiwa Spika,
Ulinzi na Usalama wa nchi yetu uliendelea kuwa agenda yetu kuu katika miaka mitano iliyopita. Nilipokuja kulifungua Bunge letu mwaka 2005, niliahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Nne itajenga mazingira mazuri ya kazi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Kazi hiyo tumeifanya na tunaendelea nayo. Tumeviwezesha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kifedha na kivifaa ili viweze kumudu majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Tumeendelea kuboresha makazi ya wanajeshi na askari wetu kwa kujenga nyumba bora kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na Magereza. Kazi hiyo inaendelea. Bado kuna changamoto kubwa mbele yetu. Hata hivyo, tutaendelea kuimarisha vyombo vyetu ili viendelee kutekeleza majukumu yake vizuri zaidi.


Mheshimiwa Spika,
Niliahidi kuwa tutaanza kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani duniani iwapo tutaombwa kufanya hivyo. Nafurahi kusema kuwa tumepeleka walinzi wa amani huko Lebanon na Darfur. Vilevile, mwaka 2008 Jeshi letu liliongoza kwa ufanisi mkubwa majeshi ya nchi za Umoja wa Afrika kukirejesha katika Umoja wa Jamhuri ya Visiwa vya Comoro Kisiwa cha Anjouan kilichokuwa kikitawaliwa kwa mabavu na kiongozi muasi Kanali Mohamed Bakar. Umoja wa nchi hiyo umerejea na kuimarishwa.



Uhalifu
Mheshimiwa Spika,
Uhalifu, hasa wa kutumia silaha, bado ni changamoto kwa usalama wa watu wetu na mali zao. Tulipoingia madarakani tulikuta wimbi kubwa sana la uhalifu, na nikaahidi hapa Bungeni kwamba hatutawaacha majambazi watambe. Jeshi la Polisi lilifanya kazi kubwa kututoa katika wimbi lile la uhalifu. Uhalifu upo, lakini sio kama ilivyokuwa wakati ule.
Jeshi letu linaendelea kudhibiti kuzagaa kwa silaha na kukusanya taarifa za uhalifu na wahalifu na kuvunja mitandao yao. Hatuna budi kutambua kwamba uhalifu unaozuiwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika. Na, siku hizi tofauti na mwaka 2005, tukio likitokea haichukui muda mrefu wahusika kutiwa nguvuni na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria. Napenda kulipongeza Jeshi letu la Polisi kwa kazi nzuri.



Wakimbizi
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2005, niliahidi kwamba tutaongeza kasi ya kuwarudisha kwao wakimbizi waliopo nchini mwetu. Ahadi hiyo tumeitimiza. Katika miaka mitano hii, tumewarejesha kwao wakimbizi 483,804 na tumefunga kambi 12 za wakimbizi. Vilevile, kwa kutimiza wajibu wetu wa kihistoria, tuliwapa uraia wa Tanzania wakimbizi 1,423 kutoka Somalia na 160,000 kutoka Burundi walioamua kuomba uraia wa nchi yetu. Wengi wa ndugu zetu hawa hawajui pa kwenda huko Burundi.


Mheshimiwa Spika,
Niliahidi pia kwamba katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, tutaanza kutoa vitambulisho vya uraia. Bahati mbaya hatukufanikiwa kuanza kutoa vitambulisho hivyo, lakini tumefikia hatua nzuri. Ni matarajio yangu kwamba mapema kipindi kijacho lengo hilo litatimizwa.


HALI YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika;
Tuliwaahidi Watanzania kwamba katika miaka mitano ya uongozi wetu, tutaendeleza jitihada za kukuza na kujenga uchumi wa kisasa na ulio endelevu ili kupunguza umaskini na kuboresha hali zao zao za maisha. Katika miaka mitano iliyopita tumeendelea kusimamia vizuri sera za uchumi jumla (macro-economic policies). Pia tumetunga na kuboresha sera za kisekta, na sheria mbalimbali ili kurahisisha ushiriki wa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla katika shughuli za kiuchumi.
Pato la Taifa liliongezeka kutoka shilingi 15.9 trilioni mwaka 2005 hadi shilingi 28.2 trilioni mwaka 2009 kwa bei za miaka husika. Kwa ajili hiyo pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi 441,030 mwaka 2005 hadi shilingi 693,185 mwaka 2009. Kasi ya wastani ya ukuaji wa pato la taifa ilikuwa asilimia 6.9 katika kipindi hicho. Kasi ingekuwa kubwa zaidi kama uchumi wetu usingekabiliwa na matatizo ya ukame, upungufu mkubwa wa umeme, kupanda sana kwa bei za mafuta duniani na kudorora kwa uchumi wa dunia. Kuharibika kwa reli ya kati kulikuwa pigo lingine kubwa kwa ustawi wa uchumi wetu.
Pamoja na hayo hatuna budi kujipongeza kwani uchumi wetu kukua kwa asilimia 6 mwaka 2009 na wastani wa asilimia 6.9 kwa miaka mitano hii ni mafanikio ya aina yake. Ni kielelezo cha uimara na uhimilivu wa uchumi wetu na kuthibitisha kuwa hatua tulizochukua kuuhami uchumi wetu zilikuwa sahihi. Mtakumbuka kuwa tulitumia shilingi trilioni 1.7 kwa ajili hiyo. Vile vile inathibitisha kuwa mageuzi ya kiuchumi tuliyoendelea kuyatekeleza tangu miaka ya 1990 yamezaa matunda tuliyoyatarajia.


Mheshimiwa Spika;
Kwa jumla uchumi uliendelea kuwa tulivu. Karibu viashiria vyote muhimu isipokuwa mfumuko wa bei vilikuwa imara. Mapato yetu ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje yaliongezeka kutoka dola milioni 2,994.9 mwaka 2005 hadi dola milioni 4,693.6 mwaka 2009. Akiba yetu ya fedha za kigeni iliongezeka kutoka dola bilioni 2.21 mwaka 2005 hadi dola bilioni 3.55 mwaka 2009 ambazo zinatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa karibu miezi 6. Katika miaka mitano hii, kudhibiti mfumuko wa bei ilikuwa changamoto kubwa hasa kuanzia mwaka 2007, ambapo bei za mafuta zilipanda sana na bei za vyakula pia zilipanda kupita kiasi kwa sababu ya upungufu uliosababishwa na ukame wa mwaka 2005, 2006 na wa 2009. Mfumuko wa bei ulipanda kutoka asilimia 5 mwaka 2005 hadi asilimia 12.1 mwaka 2009. Kutokana na juhudi tulizozifanya tukisaidiwa na hali nzuri ya chakula mwaka huu, mfumuko wa bei unaonyesha dalili ya kushuka. Kwa mfano, mwezi Juni mwaka huu mfumuko wa bei ulishuka na kufikia asilimia 7.2. Kama hali ya upatikanaji wa chakula nchini na kwa majirani zetu itaendelea kuwa nzuri na bei za mafuta hazitapanda sana mfumuko wa bei utashuka zaidi.


Mapato na Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii, tumeongeza Mapato ya ndani zaidi ya mara mbili kutoka wastani wa shilingi 177.1 bilioni kwa mwezi mwaka 2005/06 hadi shilingi 390.7 bilioni kwa mwezi mwaka 2009/2010. Hii imetupa uwezo wa kuongeza bajeti ya Serikali kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadi kufikia shilingi trilioni 11.6 mwaka 2010/11. Aidha, tumeendelea kupunguza utegemezi wa wafadhili katika bajeti ya Serikali kutoka asilimia 44 mwaka 2005/2006 hadi asilimia 28 mwaka huu, 2010/2011. Hivyo safari ya kupunguza utegemezi tunaifanya kwa mafanikio kama tulivyoahidi.


Nidhamu ya Matumizi ya Fedha za Umma
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio kwenye kukusanya mapato ni jambo moja, lakini kuyatumia vizuri mapato hayo ni jambo jingine. Kama nilivyoahidi, tumefanya jitihada kubwa katika kusimamia ufanisi katika matumizi ya serikali. Nimeeleza awali hatua tulizochukua kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuifanya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali isomwe na wahusika, kuzungumzwa na kuifanyia kazi. Pia tumechukua hatua za kubana mianya ya ubadhirifu na utekelezaji mbovu wa miradi ya Serikali. Nimeagiza kwamba TAKUKURU na Polisi wahusike mara moja pale Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anapogundua kuna wizi na ubadhirifu.


Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Mheshimiwa Spika;
Tulipokutana mara ya kwanza, tarehe 30 Desemba, 2005, niliainisha majukumu manane ya Serikali katika kutengeneza mazingira mazuri kwa uchumi kukua na biashara kustawi. Tumeandaa sera mbalimbali na kurekebisha baadhi ya sheria ili kuboresha mazingira ya uwekezaji, ukuaji wa uchumi, na mfumo bora wa fedha. Pia, tumeweka mifumo bora ya kusuluhisha haraka tofauti na migogoro baina ya wawekezaji au baina ya wafanyabiashara, au tofauti za kibiashara baina ya mtu na mtu au kampuni na kampuni. Kwa ajili hiyo tumeimarisha Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara. Aidha, tumeanzisha kitengo cha kusikiliza malalamiko ya wawekezaji na kuyatafutia ufumbuzi haraka (Investors’ Complaints Bureau) chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi. Ili kudhibiti na kusimamia viwango vya huduma na bidhaa tumeimarisha Tume ya Ushindani wa Haki wa Kibiashara, Wakala wa Chakula na Madawa na


Shirika la Viwango Tanzania.


Mheshimiwa Spika;
Katika kutambua ushiriki wa sekta binafsi katika masuala ya ubia, Serikali imeandaa Sera, na jana Bunge lako Tukufu limepitisha Muswada wa Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP). Lengo ni kuweka bayana mfumo na taratibu zitakazowezesha kufikiwa kwa ufanisi wa ubia kati ya sekta hizi mbili.
Vilevile, tumeendelea kuimarisha majadiliano kati ya Serikali na Sekta Binafsi. Kama nilivyoahidi hapa Bungeni, Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya yameshaundwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji na kuibua fursa za uwezeshaji kiuchumi. Tunaendelea kuchukua hatua za kisera na kisheria kwa lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Shabaha yetu ni kuona kwamba uwekezaji unaendelea kuongezeka nchini kama ilivyotokea kati ya mwaka 2005 na 2008 ambapo uwekezaji ulikua kutoka dola za Marekani 568 milioni hadi dola 744 milioni. Mwaka 2009 ulishuka na kuwa dola 550 milioni kutokana na msukosuko wa uchumi duniani.


Uwezeshaji wa Wananchi
Mheshimiwa Spika,
Uwezeshaji wa wananchi ni moja ya dhima kuu za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Tuliahidi kuwa Serikali itaendeleza mifuko na fursa zilizopo na kuanzisha nyingine mpya kwa nia ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Katika kutekeleza ahadi hiyo, tumeimarisha mifuko iliyopo kama vile Mfuko wa Vijana, Mfuko wa Akina Mama, Mfuko wa Uwezeshaji wa Wajasiriamali Wadogo (Small Entrepreneur Loan Facility –SELF), na Mfuko wa Dhamana wa Mikopo kwa Wafanyabiashara Wadogo (SME Credit Guarantee Scheme). Tumeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Mabilioni ya JK). Kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, tumechangia sehemu kubwa ya mtaji wa mwanzo wa uanzishaji wa Benki ya Wanawake ambayo tayari tayari imeanza kutoa huduma.


Mheshimiwa Spika,
Wakati Mfuko wa Akina Mama umekopesha zaidi ya wanawake 300,000, hadi Mei 2010 Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulikuwa umekopesha shilingi 45.2 bilioni na wajasiriamali 67,000 wamenufaika. Halmashauri za Wilaya 128 zimekopesha vijana jumla ya shilingi 1.16 bilioni kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Vijana.
Mipango ya Serikali ya uendelezaji wa sekta binafsi, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi imewezesha shughuli za kiuchumi kupanuka na hivyo kuchochea ongezeko la ajira nchini. Hivyo, utekelezaji wa ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuhusu kuzalisha ajira milioni moja umeenda vizuri, kwani hadi kufikia mwezi Juni 2010, ajira 1,313,121 zilikuwa zimezalishwa nchini kote.


Mheshimiwa Spika,
Vilevile, tumetimiza ahadi yetu ya kuimarisha ushirika nchini kama nguzo kuu ya kuunganisha nguvu za wanyonge kujiletea maendeleo. Chini ya uongozi wetu, idadi ya Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali nchini imeongezeka kutoka 5,730 mwaka 2005 hadi 9,501 mwaka 2010. Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa mfano, vimeongezeka kwa karibu mara tatu kutoka vyama 1,875 mwaka 2005 hadi 5,344 mwaka 2010. Aidha, akiba na amana za wanachama zimeongezeka zaidi ya mara tano kutoka Shilingi 31.4 bilioni mwaka 2005 hadi shilingi 174.6 bilioni mwaka 2010. Haya ni mafanikio makubwa.
Katika kipindi hocho Serikali ilibebea mzigo wa madeni ya Vyama vya Ushirika 38 vilivyokuwa vinadaiwa shilingi 26.8 bilioni ili kuviwezesha kupata mikopo kwenye mabenki. Kulipwa kwa madeni hayo kunatoa fursa kwa wanachama wa vyama husika kuchukua hatua sahihi za kuviimarisha Vyama vyao ili viweze kuwahudumia vizuri zaidi.


SEKTA ZA UZALISHAJI
Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Ahadi tuliyoitoa ya kutoa kipaumbele cha juu kwa maendeleo ya kilimo tumeitimiza na matokeo yake yanaonekana. Mara baada ya kuingia madarakani tukatengeneza na kuanza kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Programme - ASDP). Aidha, ili kuipa Programu hiyo msukumo na kuwashirikisha kwa karibu wadau wa sekta binafsi mwaka 2009 tulibuni mkakati ujulikanao kama Kilimo Kwanza ili kutoa msukumo zaidi wa kuleta mapinduzi ya kijani nchini. Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi 233.3 bilioni sawa na asilimia 5.8 ya bajeti yote ya Serikali mwaka 2005/06 hadi shilingi 903.8 bilioni sawa na asilimia 7.8 ya bajeti yote ya Serikali mwaka 2010/2011. Ni dhamira yetu kuendelea kuongeza bajeti ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 ya bajeti ya Serikali au hata kupita.


Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano iliyopita, tumetimiza ahadi niliyoitoa hapa Bungeni ya kuhakikisha kwamba upatikanaji na matumizi pembejeo kwa wakulima unaongezeka. Tumeongeza fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo nyinginezo kutoka shilingi 7.5 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 143.8 bilioni mwaka 2010/11.


Mbegu Bora
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki, tumefanya jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora na hasa kutoka hapa nchini. Kwanza, tulichukua hatua za kuimarisha vituo vya utafiti wa kilimo vinavyofanya uvumbuzi wa mbegu. Pili, tumechukua hatua za kuongeza uwezo wa kuzalisha mbegu baada ya uvumbuzi wa mbegu kufanyika. Miongoni mwa hatua hizo ni kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali na kuhusisha Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa. Kutokana na hatua hizi, uzalishaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 10,477.17 mwaka 2005 hadi tani 16,144.79 Desemba 2009. Tatu, kuhakikisha kuea usambazaji wa mbegu bora unakuwa rahisi na mbegu zinawafikia wakulima kwa bei nafuu. Aidha, tumeimarisha Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency - ASA) kwa ajili ya kusimamia uzalishaji wa mbegu kwa wingi na kuhakikisha zinasambazwa kwa urahisi na kuwafikia walengwa.


Zana za Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii tumeanza kuchukua hatua thabiti za kuhimiza matumizi ya zana bora za kilimo, hususan matrekta na ukulima wa kisasa nchini. Tumeendeleza sera ya kutokuwepo na ushuru wa forodha kwa matrekta. Kwa sababu hiyo, idadi ya matrekta yaliyoingia nchini katika kipindi cha 2006-2009 ni 1,737; yakiwemo makubwa 362 na madogo (power tillers) 1,379.
Baadhi ya matrekta yaliyoingizwa nchini yalinunuliwa kutokana na mkopo wa shilingi 16.3 bilioni kutoka Mfuko wa Pembejeo. Kwa ujumla Mfuko wa Pembejeo umeongeza utoaji wa mikopo ya zana na pembejeo za kilimo kutoka shilingi bilioni 4.9 mwaka 2005/06 hadi shilingi 30.1 mwaka 2009/2010. Vilevile, tunategemea kuongeza matrekta 3,000 madogo na makubwa kutokana na mkopo wa dola milioni 40 kutoka Serikali ya India. Hii itafanya idadi ya matrekta yaliyoingia nchini kuwa kubwa kuliko kipindi kingine chochote katika historia ya nchi yetu. Tumeimarisha huduma za ugani kwa kuajiri watalaam 1,802 wa kilimo katika Halmashauri, ambao wanafanya kazi ya kuwapatia wakulima mafunzo juu ya ukulima wa kisasa. Katika mwaka 2009/10 pekee, Halmashauri za Wilaya zimenunua matrekta madogo 2,154 na makubwa 53. Serikali ilizitaka Halmashauri za Wilaya kuwa chachu ya mapinduzi ya kilimo kwa kuagiza trekta na kuwauzia wakulima hasa kwenye vikundi vya uzalishaji.


Mifugo
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa mifugo, dhamira yetu imekuwa ni kuboresha mifugo na ufugaji wetu nchini ili wafugaji nao wafaidike na shughuli ya ufugaji tofauti na ilivyo sasa. Shabaha hizo ni sehemu kamili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa upande wa mifugo. Kwa ajili hiyo, katika miaka mitano hii, tumehimiza utumiaji wa madume bora ili kuongeza ubora wa mifugo yetu. Kwa vile si rahisi kupata madume ya kutosha, tumehamasisha matumizi ya uhamilishaji. Kituo cha Taifa cha Uhamilishaji kilichopo Usa River, Arumeru kimeimarishwa na vituo vidogo vitano vya kusambaza mbegu vimeanzishwa Dodoma, Mwanza, Lindi, Kibaha na Mbeya.
Tumeajiri maafisa ugani 1500 kusaidia kuelimisha wafugaji juu ya ufugaji bora na kusaidia kutoa huduma na ushauri wa kusaidia kuboresha mifugo na ufugaji. Wafugaji nao wamenufaika na mpango wa ruzuku ya pembejeo kwa kupata dawa za kinga na tiba. Katika kipindi hiki ng’ombe 11,134,000 wamechanjwa kinga ya homa ya mapafu na shilingi bilioni 13.5 zimetumika kwa ajili dawa za majosho. Aidha, majosho 543 yamejengwa, na juhudi zinaendelea za kujenga malambo, mabwawa na visima ili kuipatia mifugo maji ya uhakika. Vile vile, juhudi za kuimarisha ranchi za taifa zinaendelea kwa dhati ikienda sambamba na ujenzi wa viwanda vya kusindika nyama katika maeneo mbalimbali nchini. Katika juhudi hizi sekta binafsi inatambuliwa, inashirikishwa na kusaidiwa pale inapostahili au Serikali inapoombwa kufanya hivyo.
Kwa nia ya kutoa msisitizo maalum kwa maendeleo ya mifugo nchini, mchakato wa kuanzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Mifugo inayojitegemea umeanza.
Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Niliahidi hapa Bungeni mwaka 2005 kwamba Serikali nitakayounda itatoa kipaumbele kwenye sekta ya uvuvi. Ahadi hiyo tumeitimiza. Niliunda Wizara mpya ya Mifugo na Uvuvi ili kuupa uvuvi umuhimu unaostahili. Huko nyuma uvuvi ulikuwa umefichwa chini ya sekta ya maliasili. Vile vile tumeondoa kodi ya zana za uvuvi zikiwemo boti, nyavu, na injini ili kuwezesha wavuvi kupata zana za kisasa za uvuvi. Aidha, katika kipindi hiki pia juhudi za kupambana na uvuvi haramu ziliongezwa. Kati ya mwaka 2006 – 2009 tulivuna samaki wenye thamani ya shilingi 783.3 bilioni na kuuza nje ya nchi samaki wenye thamani ya shilingi 597.5 bilioni. Hivi sasa tumeelekeza nguvu zetu katika kuendeleza ufugaji wa samaki.
Viwanda na Biashara
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii, sekta ya viwanda iliendelea kustawi vyema. Kasi ya ukuaji wa sekta hii ulikuwa mzuri na wa kutia moyo. Kati ya mwaka 2005 na 2009 sekta ya viwanda ikihusisha ujenzi ilikua kwa wastani wa asilimia 8.8, wakati uzalishaji wa bidhaa za viwandani (manufacturing) uliongezeka kwa wastani wa asilimia 9.14. Viwanda vilivyochangia sana kwenye mafanikio haya ni vile vya sementi, vifaa vya umeme, vinywaji na usindikaji wa nafaka.
Tumechukua hatua thabiti za kuchochea uwekezaji kwa ajili ya kuendeleza viwanda nchini. Tulianzisha Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Ajili ya Mauzo Nje (Export Processing Zones Authority). Mamlaka hiyo imepewa dhamana ya kusimamia shughuli za Maeneo ya Uzalishaji kwa Ajili ya Mauzo Nje (EPZ) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Special Economic Zones – SEZ). Kati ya mwaka 2006 na 2008 viwanda 28 vya uzalishaji vimesajiliwa chini ya EPZ. Mwezi Mei, 2010, Eneo Maalum la Kiuchumi la Benjamin William Mkapa lilifunguliwa na tayari wawekezaji 12 wameshapatikana. Mauzo ya bidhaa kutoka kwenye maeneo ya EPZ kwenda nje ya nchi yalikuwa dola za Kimarekani 235 milioni.
Mheshimiwa Spika;
Utaratibu wa EPZ na SEZ utakuwa chachu ya kuchochea uwekezaji katika viwanda nchini. Ndiyo maana Mikoa na Wilaya zinahimizwa kutenga maeneo yanayoweza kutumika kwa ajili ya kuanzisha EPZ na SEZ. Baadhi ya mikoa imefanya hivyo na mingine bado. Nashauri wale ambao bado wafanye hivyo haraka kwa maslahi ya mikoa yao na nchi kwa jumla.
Madini
Mheshimiwa Spika,
Madini ni sekta muhimu sana hapa nchini. Ndiyo ya pili baada ya utalii kwa kuingiza pesa nyingi za kigeni na inatoa ajira kwa watu wengi. Thamani ya madini yaliyosafirishwa nje ya nchi mwaka 2005 ilikuwa dola 720.49 milioni namwaka 2009 iklikuwa dola 1,219.06 milioni. Ajira katika uchimbaji mkubwa iliongezeka kutoka wafanyakazi 7,000 mwaka 2005 hadi 13,000 mwaka 2008.
Hivyo, kuendeleza sekta hii kwa maana ya uchimbaji mkubwa na mdogo ilikuwa miongoni mwa vipaumbele vya juu vya Serikali yangu. Miongoni mwa mambo muhimu niliyoamua kufanya ni kuitazama upya mikataba ya madini, sera na sheria ya madini. Nia yetu ni kuhakikisha kuwa uwekezaji katika sekta hii unakua na wawekezaji na wananchi wananufaika sawia.
Niliunda Kamati chini ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini wakati ule Ndugu Lawrence Masha, kuitazama upya mikataba ya madini. Kutokana na ushauri wa Kamati, niliagiza kufanyike majadiliano kati ya Serikali na makampuni ya madini kuhusu kipengele cha nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa awali ambao haujarejeshwa (additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure). Kuwepo kwa kipengele hicho kulifanya makampuni yasilipe kodi ya mapato, hivyo kuifanya nchi isipate chochote mpaka mwisho wa uhai wa mgodi. Lengo letu lilikuwa kuondoa kipengele hicho ili makampuni husika yaweze kulipa kodi ya mapato mapema inavyostahili. Nafurahi kusema kuwa tulifanikiwa katika mazungumzo yetu na makampuni makubwa manne ya uchimbaji madini hapa nchini. Hivyo basi migodi ya Golden Pride, Geita Gold Mines na Tanzanite One imekwishaanza kulipa kodi ya mapato. Baadhi ya migodi ya Kampuni ya Barrick itaanza kulipa kodi hiyo muda si mrefu kutoka sasa.
Jambo lingine ambalo tulilifanya ni kujenga uwezo wetu wa ndani wa kukagua uzalishaji katika migodi mikubwa. Kazi hii ilikuwa inafanywa na Kampuni ya Alex Stewart baada ya mkataba wao kuisha na tulipoamua tusiendelee nao, tukaunda Wakala wa Kukagua Uzalishaji katika Migodi Mikubwa. Wakala unafanya kazi nzuri ya kubaini gharama halisi za uwekezaji na shughuli zinazoendelea migodini ili kodi stahiki zilipwe kwa Serikali. Kutokana na hatua hizi mbili mchango wa sekta ya madini kwenye mapato ya Serikali umeongezeka na utazidi kukua siku za usoni.
Kwa mfano, mwaka 2005 Serikali ilipata shilingi 457.4 bilioni na mwaka 2008 illipata shilingi 840.0 bilioni.
Mheshimiwa Spika;
Novemba, 2007 niliamua nijumuishe watu wengine kutoka nje ya Serikali katika kazi iliyokuwa inafanywa na Kamati ya Mheshimiwa Lawrence Masha. Ndipo, nikaunda Kamati ya Rais ya Madini iliyoongozwa na Mheshimiwa Jaji Mark Bomani ili kuangalia kwa upana zaidi namna gani tunaweza kuboresha shughuli za sekta hii muhimu kwa manufaa ya wawekezaji na taifa. Kamati hiyo mbayo baadhi ya Wabunge walishiriki, ilitoa mapendekezo mazuri ambayo yametusaidia kutengeneza Sera Mpya ya Madini ya Mwaka 2009 na kutunga Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2010.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Jaji Mark Bomani, Mheshimiwa Masha na wajumbe wa Kamati zao kwa mchango wao adhimu uliosaidia kujenga misingi mizuri ya kuwezesha taifa letu kunufaika na rasilimali yake iliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Spika;
Katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Serikali imeanzisha na kutoa leseni za uchimbaji mdogo (Primary Mining Licences), na kuwahamasisha waunde vikundi vya ushirika ili kuweza kuwasaidia vizuri zaidi.
Utalii
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa Utalii, tumeendelea na jitihada za kuiendeleza sekta hii muhimu na hasa kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu katika masoko makubwa duniani. Ni shughuli ya gharama, lakini faida yake ni kuongezeka watalii na mapato kwa nchi yetu. Tumetunga Sheria ya Utalii ya mwaka 2008 na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 kwa lengo la kuboresha huduma za utalii na kuziba mianya ya uvujaji mapato yatokanayo na utalii. Tumeimarisha pia miundombinu ya utalii kwa kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zaidi za kitalii. Nafurahi kwamba hoteli mpya zimejengwa katika kipindi hiki.
Kutokana na jitihada hizo, watalii wameongezeka na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola milioni 823.5 mwaka 2005 hadi dola milioni 1,198.76 mwaka 2008. Mwaka 2009 mapato yalishuka kidogo na kuwa dola milioni 1,162.8 kwa sababu ya kudorora kwa uchumi wa dunia na kusababisha watalii kupungua na kukaa nchini kwa siku chache. Sasa hali inaonekana kuanza kurejea kuwa ya kawaida hivyo tutegemee kuongezeka kwa watalii na mapato ya Serikali.
HUDUMA ZA UCHUMI
Barabara
Mheshimiwa Spika,
Hatuwezi kujenga mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi, kuongeza uzalishaji mali, na kuboresha maisha ya Watanzania kama miundombinu ya usafirishaji ni mibovu na haitoshelezi mahitaji.
Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2005 ilituagiza kwamba, ifikapo mwaka 2010, tuwe tumekamilisha kutekeleza miradi 17 ya barabara kuu. Leo hii, ninaposimama mbele yenu, kati ya miradi hiyo 17, tumekamilisha miradi 12 na miradi 5 iliyosalia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Barabara tulizozikamilisha ni: Singida – Shelui (km 110), Shelui – Igunga – Nzega (km 108), Nzega – Ilula (km 138), Muhutwe – Kagoma (km 24), Nangurukuru – Mbwemkuru – Mingoyo (km 190), Mkuranga – Kibiti (km 121), Pugu – Kisarawe (km 3.6), Chalinze – Morogoro – Melela (km 129), Tunduma – Songwe (km. 71), Kyabakari – Butiama (km 11.4), Dodoma – Morogoro (km 256), Dodoma – Manyoni (km 127), Buzirayombo – Kyamyorwa (km.120) na Buzirayombo – Geita (km.100).
Mheshimiwa Spika;
Ndani ya miaka hii mitano, tumekamilisha ujenzi wa miradi ya barabara 26 zenye urefu wa kilomita 2,237. Sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa miradi ya barabara 28 zenye urefu wa kilomita 2,208. Kwa jumla lengo la kuiunganisha Mikoa yote ya Tanzania kwa barabara za lami lina mwelekeo mzuri. Hivi sasa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Tabora kuna kazi ya ujenzi wa barabara inayoendelea au mchakato wa kuanza kazi hiyo umefikia hatua ya kuanza utekelezaji wake. Katika Barabara za Mikoa, kilomita 121 zimejengwa kwa kiwango cha lami; kilomita 1,979.4 zimefanyiwa matengenezo katika kiwango cha lami na kilomita 3,114 zimefanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe.
Katika kipindi hiki, pia madaraja 8,385 yalifanyiwa matengenezo ya kuzuia uharibifu na madaraja 660 kufanyiwa matengenezo makubwa. Aidha, Madaraja 53 yamejengwa likiwemo Daraja la Mpiji, Daraja la Ruvu na Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji. Usanifu wa kina wa baadhi ya madaraja umekamilika na kusubiri pesa zipatikane ili ujenzi uanze. Daraja la Mto Kilombero ni miongoni mwa madaraja hayo. Tumenunua vivuko vipya 5 na kukamilisha ujenzi wa vivuko 2. Nafurahi kwamba kero kubwa zilizokuwepo Kigamboni, Busisi, Pangani na Kome sasa zimeisha.
Mheshimiwa Spika,
Pesa nyingi tulizotenga katika mfuko wa barabara na kuzigawa kwenye Halmashauri za Wilaya zimesaidia kuimarisha barabara za Wilaya na Vijiji. Kwa jumla, jitihada na hatua zote hizi tulizochukua zimesaidia kuwezesha barabara nyingi nchini kupitika mwaka mzima.
Reli
Mheshimiwa Spika,
Nyote ni mashahidi kwamba tumehangaika sana na Reli zetu mbili za TAZARA na Reli ya Kati katika kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa miaka kadhaa Reli reli zetu hizi zilikuwa na matatizo mengi na kusababisha huduma za uchukuzi wa abiria na mizigo kuathirika. Kiini cha tatizo ni uendeshaji usioridhisha. Kwa ajili hiyo, Serikali ya Awamu ya Tatu iliamua kutafuta kampuni ya uendeshaji wa reli ije isaidie kuendesha Reli yetu ya Kati. Hivyo ikapatikana kampuni ya RITES ya kutoka India. Wakati ule iliaminika kuwa kampuni hiyo ingesaidia kupata jawabu kwa tatizo linaloisibu reli yetu. Bahati mbaya matarajio yetu hayakuwa, ndiyo maana tumelazimika kufanya uamuzi tulioufanya wa kuanza mazungumzo na wabia hao ili Serikali ichukue tena reli hiyo na kutafuta namna nyingine iliyo bora ya kuiendesha reli yetu.
Kwa upande wa reli ya TAZARA, mazungumzo kati yetu na Zambia yanaendelea kuhusu kupata ufumbuzi wa tatizo la uendeshaji wa reli hiyo. Katika mazungumzo hayo pia na marafiki zetu wa China waliotusaidia kuijenga reli hiyo tumewahusisha. Naamini baada ya muda si mrefu tutapata ufumbuzi.
Nishati
Mheshimiwa Spika,
Miaka mitano hii ilijawa na changamoto tele kwa upande wa sekta nzima ya nishati. Tulikabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa umeme kwa sababu ya ukame lililotufundisha kupunguza utegemezi kupita kiasi kwa umeme wa maji. Tumeongeza uzalishaji wa umeme kutokana na gesi asilia kwa megawati 145 pale Ubungo na Tegeta. Hivi sasa mchakato unaendelea wa kujenga kituo kingine cha MW 100 Ubungo kitakachotumia gesi asilia na cha MW 60 Mwanza kitakachotumia mafuta ya dizeli. Bahati mbaya mipango ya kuzalisha MW 300 Mtwara kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay haukuweza kutekelezwa kwa sababu wabia wetu walijitoa kutokana na msukosuko wa uchumi wa dunia. Umeme wa MW 200 kutokana na makaa ya mawe ya Kiwira umecheleweshwa na taratibu za milki ambazo karibuni zitamalizika.
Tarehe 12 Juni, 2008, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Umeme Na. 10 ya 2008 ambayo imetoa fursa pana kwa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Utaratibu huu mpya umepata mwitikio mzuri. Nimeambiwa kuwa tayari wawekezaji binafsi wanne (4) wameshafikia makubaliano na kuingia mikataba ya kuiuzia umeme TANESCO. Naamini katika miaka mitano ijayo wawekezaji wengi binafsi watajitokeza kuwekeza katika sekta hii, hivyo kupunguza hofu ya upungufu wa umeme.
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuyapatia umeme makao makuu ya wilaya za Serengeti, Ukerewe, Mbinga, Simanjiro, Ludewa, Mkinga, Kilolo, Uyui, Kilindi na Bahi. Mipango ya kuzipatia umeme Wilaya za Bukombe, Longido, Ngorongoro, Kasulu, Kibondo na Nkasi ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Jitihada za kuunganisha mikoa ya Ruvuma, Kigoma, Kagera na Rukwa kwenye gridi ya Taifa zinaendelea.
Mwaka 2007 Oktoba, tulianzisha Wakala wa Nishati Vijijini ukiwa na jukumu la kuongeza kasi ya kupeleka umeme vijijini. Tumepata mafanikio ya kutia moyo kama inavyothibitishwa na kazi ya kupeleka umeme kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Aidha, tangu Wakala ilipoundwa mwaka 2007 hadi sasa zaidi ya vijiji 180 vimepatiwa umeme kwa gharama ya shilingi 9.4 bilioni. Kazi inaendelea.
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa ardhi na makazi nako tumepiga hatua. Kati ya Januari 2006 na Mei 2010 tumefanikiwa kupima na kutoa hati kwa jumla ya vijiji 6,129. Kwa sababu hiyo idadi ya vijiji vilivyopimwa na kusajiliwa vimefikia 10,682. Hii ni sawa na asilimia 97 ya vijiji 11,000 nchini. Mtakubaliana nami kwamba haya ni mafanikio makubwa.
Vilevile, tumeendelea na mpango wa matumizi ya ardhi, wa kupima mashamba ya wanavijiji na kutoa Hatimiliki za Kimila. Jumla ya Hatimiliki za Kimila 54,393 zilitayarishwa na kutolewa kwa wananchi katika Wilaya za majaribio za Mbozi, Babati, Bariadi, Namtumbo na Manyoni. Wananchi wameanza kunufaika kwa kuzitmia hati hizo kama dhamana ya mikopo katika mabenki. Kwa mfano, hadi Desemba 2009, wananchi kadhaa wa Mbozi waliweza kukopa shilingi bilioni 10.38 kutoka benki kwa kutumia hatimiliki hizo. Hii ni habari njema kwa upande wa uwekezaji wa wananchi.
Mheshimiwa Spika;
Vilevile, kati ya Januari 2006 na Mei 2010, tumepima viwanja 37,458 katika maeneo ya miji mbalimbali. Ili kuharakisha utoaji wa hati za kumiliki ardhi, tumeanzisha kanda 6 za ardhi nchini zenye mamlaka ya kutoa hati hizo. Vilevile, chini ya Programu ya MKURABITA jumla ya nyumba 290,000 katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Tanga na Moshi zilitambuliwa na wamiliki kupewa leseni za makazi ambazo wanaweza kuzitumia kama dhamana kuombea mikopo katika taasisi za fedha. Huu ni mfano mwingine wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii tumeboresha mazingira ya kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini. Ujenzi wa mkongo wa taifa ulioanza Februari, 2009 unaendelea vizuri na kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa, ifikapo Juni, mwakani, Makao Makuu ya Mikoa na ya Wilaya zote yatakuwa yamefikiwa. Katika kipindi hiki, watumiaji wa simu za mikononi wameongezeka kutoka milioni 3.5 hadi milioni 16. Watumiani wa simu za mkononi wataongezeka na gharama za simu zitashuka baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mkongo kigae.
Mheshimiwa Spika;
Tumeanzisha mpango wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kuendeleza elimu nchini. Mpango uitwao Tanzania Beyond Tomorrow au “Tanzania Baada ya Kesho” chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, una lengo la kufanya hivyo. Katika mpango huo walimu na wanafunzi katika shule za sekondari watawezeshwa kupata na kutumia kompyuta. Mpango huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo tutafanya kila tuwezalo ufanikiwe.

HUDUMA ZA JAMII
Maji
Mheshimiwa Spika,
Mara tulipoingia madarakani, ili kuhakikisha tunaongeza upatikanaji wa maji mijini na vijijini tukaanzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inayotekelezwa kwa vipindi vya miaka mitano mitano kuanzia mwaka 2007-2025. Utekelezaji wa Programu hii umetuwezesha kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 53.7 mwaka 2005 hadi asilimia 60.1 mwaka 2010. Kwa mijini tumefikia asilimia 84 kutoka asilimia 74 mwaka 2005.
Katika kipindi hiki tumefanikiwa kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa upelekaji maji katika miji ya Shinyanga na Kahama na vijiji vinavyopitiwa na bomba hilo. Watu wapatao milioni moja wananufaika. Aidha, tumefanikiwa kuziwezesha Mamlaka za Maji katika Manispaa 13 kati ya Manispaa 19 zilizopo kujitegemea kwa gharama zote za uendeshaji na matengenezo. Bado tuko nyuma ya lengo la kufikia asilimia 65 vijijini na asilimia 90 mijini ingawaje kazi itakayofanyika mpaka mwisho wa mwaka katika bajeti yetu ya tano itatufikisha mahali pazuri kiasi.
Huduma ya Afya
Mheshimiwa Spika,
Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na watu kuwa na afya bora. Katika kipindi hiki tulitengeneza Sera Mpya ya Afya na kutengeneza Mpango wa miaka kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) kwa ajili ya kutekeleza sera hiyo. MMAM una malengo makuu yafuatayo:-
(a) Kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi wananachi, hivyo zahanati na vituo vya afya vitajengwa vijijini na kwenye kata. Hospitali za Wilaya na Mikoa zitaboreshwa ili matatizo mengi ya afya yamalizikie huko.
(b) Kuongeza wataalamu wa afya wa kada zote kwa maana ya kupanua fursa za mafunzo na ajira.
(c) Kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na mahitaji mengine.
(d) Kuongeza nguvu katika kupambana na maradhi hasa yale yanayoua na kusumbua watu wengi.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki bajeti ya afya imeongezeka kutoka shilingi 271 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 1,205.9 bilioni mwaka 2010/11, yaani kutoka asilimia 6 ya bajeti hadi asilimia 10.4. Zahanati 1,403, vituo vya afya 167 na hospitali 24 zimejengwa. Hospitali zote za Wilaya zimepatiwa X-ray na ultrasound isipokuwa wilaya 7 ambazo nazo zitapatiwa hivi karibuni. Karibu hospitali zote za Mikoa zina maabara za kisasa. Wanafunzi wa taaluma mbalimbali za afya wameongezeka kutoka 1,059 mwaka 2005 hadi 4,422 mwaka 2010. Madaktari bingwa wameongezeka kutoka 46 mwaka 2005 hadi 265 mwaka 2009. Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza kufundisha madaktari na mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu kipya cha Tiba pale Mloganzila karibu na Dar es Salaam umeanza.
Mheshimiwa Spika;
Mfumo wa upatikanaji wa dawa umeboreshwa. Hivi sasa vituo hupata dawa kulingana na mahitaji. Mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI yamezidi kuongezewa nguvu. Kutokana na kuongeza upatikanaji wa vyandarua vilivyotiliwa dawa bure kwa watoto wote wa chini ya miaka mitano na kwa hati punguzo kwa akina mama wajawazito, na matumizi ya dawa mseto, vifo kutokana na malaria vimepungua kutoka 80,000 – 100,000 kwa mwaka hadi 40,000 – 50,000. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kutokomeza malaria kwa maana ya kuua mbu wanaosababisha malaria. Kutokana na uhamasishaji wa kujikinga dhidi ya maradhi ya UKIMWI na upimaji wa hiari, kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 7.7 mwaka 2005 hadi aslilimia 5.6 mwaka 2009. Watu milioni 11 wamejitokeza kupima UKIMWI tangu kampeni ya upimaji wa hiari tuliyoizindua Julai, 2007.
Tumeanza kupata mafanikio kwa upande wa kujenga uwezo wetu wa ndani wa kupambana na maradhi ya saratani, moyo na figo. Juhudi zinaendelea kupanua uwezo huo na kuendeleza kwa maradhi mengine.
Elimu
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bungeni hili nilisema kuwa “Hakuna taifa lililopata maendeleo bila kuendeleza elimu. Hivyo kuendeleza elimu nchini itakuwa agenda muhimu ya serikali ya Awamu ya Nne.”
Mheshimiwa Spika,
Nasimama mbele ya Bunge hili nikiwa na faraja kubwa kutokana na mafanikio makubwa tuliyoyapata kwenye sekta ya elimu nchini. Tumepanua elimu ya awali na msingi. Wanafunzi wa awali wameongezeka kutoka 638,591 mwaka 2005 hadi 825,465 mwaka 2010. Shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 15,816 mwaka 2010 na wanafunzi wameongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,419,305 katika kipindi hicho. Upanuzi huu umewezesha asilimia 97 ya watoto wanaostahili kupata elimu ya msingi wameandikishwa na uwiano wa kijinsia wa 1:1 umezingatiwa. Tumeajiri walimu wapya 6,028 wa shule za awali na 49,694 wa shule za msingi.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kushirikiana na wananchi, katika kipindi cha miaka mitano hii, tumeweza kujenga shule za sekondari 2,171 ikilinganishwa na shule 1,202 zilizojengwa toka uhuru mpaka mwaka 2005. Lengo la sekondari moja kwa karibu kila kata limetekelezwa na baadhi ya kata zina shule zaidi ya moja. Shule za sekondari za binafsi zimeongezeka kutoka shule 531 hadi 856 katika kipindi hicho. Ongezeko hili limewezesha idadi ya wanafunzi wanaosoma sekondari kuongezeka toka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,638,669 mwaka 2010. Aidha, idadi ya wanafunzi wanaosoma kidato cha tano imeongezeka kutoka 9,710 mwaka 2005 hadi 33,169 mwaka 2010. Pia tumeajiri walimu wapya wa Sekondari 14,329. Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010 tumejenga nyumba 15,343 za walimu, ambapo nyumba za walimu wa shule za msingi ni 9,910 na nyumba za walimu wa Sekondari ni 5,424.
Mheshimiwa Spika,
Upanuzi huu mkubwa wa elimu ya sekondari umezaa changamoto zake hasa za upungufu wa walimu, vitabu, vifaa vya kufundishia, maabara na nyumba za walimu. Kuna mipango thabiti inayoendelea kutekelezwa kukabili kila moja ya changamoto hizo. Upanuzi wa mafunzo ya walimu katika vyuo vikuu umeongeza walimu wanaohitimu kutoka 500 mwaka 2005 hadi 5,339 mwaka 2009. Kuna mpango kabambe wa kukabili upungufu wa vitabu na vifaa vya kufundishia, maabara pamoja na uhaba wa nyumba za walimu. Nyongeza kubwa ya bajeti ya elimu kutoka shilingi 669.5 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 2,045.3 bilioni mwaka 2010/11 ni ushahidi wa utashi wa kisiasa wa kuboresha elimu nchini. Naamini katika miaka michache ijayo matatizo yatapungua sana na mengine yatakuwa yameisha.
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii tumeshuhudia upanuzi mkubwa wa elimu ya juu nchini. Azma yetu ya kujenga chuo kikuu kipya imetimia tena kwa mafanikio makubwa. Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza na ujenzi wa majengo ya Chuo hicho unaendelea kwa kasi kubwa. Chuo hiki ni fahari ya nchi yetu kwani tumekibuni wenyewe na kukijenga kwa kutumia fedha zetu wenyewe bila msaada kutoka nje. Katika miaka mitatu ya mwanzo ya Chuo hicho tayari kuna wanafunzi 15,000 na lengo la wanafunzi 40,000 litafikiwa.
Idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu vya umma na binafsi nchini imeongezeka kwa karibu mara tatu, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi 117,068 mwaka 2009. Katika kipindi hiki fedha za mikopo ya wanafunzi zimeongezeka kutoka shilingi 56.1 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 197.3 bilioni mwaka 2009/10 na kuwa shilingi 237 bilioni mwaka 2010/11. Wanafunzi wanaonufaika na mikopo wameongezeka kutoka 16,345 hadi 69,981. Tumeanza kuchukua hatua za kurekebisha kasoro za utoaji wa mikopo hiyo.
Hifadhi ya Mazingira
Mheshimiwa Spika,
Niliahidi kwamba tutafanya jitihada kubwa ya kuhifadhi mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi yetu. Niliunda Kamati ya Mazingira ya Baraza la Mawaziri chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais,. Tulitoa maelekezo kadhaa kuhusiana na uboreshaji wa mazingira kwa Wizara na Halmashauri za wilaya na miji kutekeleza. Nafurahi maelekezo hayo hususan yahusuyo mifuko ya plastiki na kutunza vyanzo vya maji yametekelezwa na yanaendelea kutekelezwa. Kwa jumla mwamko wa watu wa kuhifadhi mazingira unazidi kukua. Tumefanikiwa pia kuiongezea Wizara inayohusika na Mazingira uwezo na mamlaka ya usimamizi.
Michezo, Burudani na Utamaduni
Mheshimiwa Spika,
Tuliahidi kuendeleza shughuli za michezo na utamaduni. Tumerudisha michezo mashuleni ili tujipe fursa ya kubaini vipaji vya watoto wetu na kuviendeleza. Nimetimiza ahadi yangu ya kumgharimia mwalimu wa mpira wa miguu wa Timu ya Taifa Stars kutoka nje. Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil aliajiriwa na amesaidia sana kuinua kiwango cha soka hapa nchini. Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 172 Desemba 2005 hadi nafasi ya 108 Aprili 2010. Mimi naamini kama tutaongeza juhudi tupo karibu kufanikiwa zaidi.
Tumeshapata makocha wa riadha na ngumi. Nimekubali ombi la CHANETA kumlipia kocha wa mchezo wa netiboli. Hivi karibuni nilisaidia kugharimia kambi ya mazoezi na posho za wachezaji wa Twiga Stars ili waweze kushiriki vizuri katika mashindano ya soka la wanawake Afrika. Ushindi wao ni fahari ya nchi yetu. Tutaendelea kuwasaidia ili waendelee kupeperusha Bendera yetu kwa mafanikio makubwa zaidi.
Nafurahi kwamba kupitia Taifa Stars moyo wa uzalendo umezidi kuongezeka miongoni mwa Watanzania. Tofauti na ilivyokuwa zamani, ni jambo la kawaida kuwaona Watanzania wakivaa jezi za timu yetu ya taifa au wakienda uwanjani wakiwa wanapeperusha bendera yetu ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa wasanii hasa wa muziki, katika miaka mitano hii tumeshuhudia kukua na kustawi kwa muziki wa kizazi kipya na uigizaji wa filamu. Nasikitishwa sana na hali ya wasanii kutokupata malipo ya haki kwa kazi zao. Niliamua nijaribu kusaidia. Nilipokutana na baadhi ya wana muziki wa kizazi kipya wakanieleza haja ya wao kuwa na mastering studio yao ili waweze kumiliki kazi zao. Nimeshawanunulia mtambo huo uliogharimu shilingi 50 milioni. Hivi sasa tumelipia mtaalamu mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam asaidie kutengeneza njia bora ya kusambaza kazi za wasanii wa muziki na filamu ili wapate malipo halali kwa jasho lao. Mafanikio ya zoezi hili yatatufundisha namna ya kuwasaidia wasanii wa fani nyingine pia.
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Spika,
Katika miaka mitano hii, tumepata mafanikio makubwa katika medani ya Kimataifa. Uhusiano wetu wa kiuchumi na kisiasa na mataifa na mashirika ya kimataifa duniani umepanuka na kuimarika zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo tunaweza kuiita adui. Nchi rafiki na mashirika ya kikanda na kimataifa yameendelea kuunga mkono juhudi zetu za kujiletea maendeleo. Tumepata misaada mingi ya maendeleo na kupata misamaha ya madeni tunayodaiwa na hivyo kutupunguzia mzigo wa kulipa madeni hayo.
Uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umekuwa ukiongezeka, wigo wa masoko ya nje umekuwa unapanuka kwa bidhaa zetu na watalii kutoka nje wamekuwa wanaongezeka. Hakika diplomasia ya uchumi imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Hadhi ya Tanzania katika medani za kimataifa imepanda. Tunasikilizwa, tunaaminiwa, na tunathaminiwa. Kwa upande wa ajira katika mashirika ya Kimataifa, hakuna mafanikio makubwa kushinda yale ya dada yetu Dkt. Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ni heshima kubwa na fahari kwa nchi yetu na wanawake wa Tanzania. Hakika wanawake wakipewa fursa wanaweza.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tulibahatika kutembelewa na wageni wengi mashuhuri na wengine ni wa kihistoria kutembelea nchi yetu. Tulitembelewa na Rais George Bush wa Marekani, Rais Hu Jintao wa China, Rais Abdullah Gul wa Uturuki, Rais wa Ireland, Mary McAleese, ambaye alipata pia fursa ya kulihutubia Bunge hili, Waziri Mkuu wa Zamani wa nchi hiyo Bertie Ahern, Rais Innancio Lula da Silva wa Brazil, Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, Waziri Mkuu wa Canada, Bw. Stephen Harper, Waziri Mkuu wa Norway, Jens Stoltenberg, Malkia wa Denmark, Margrethe II, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-moon, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa, Dkt. Asha-Rose Migiro na Gavana wa Australia. Tumepokea Marais wengi wa Afrika kuja kututembelea. Yote haya yanadhihirisha kiasi gani diplomasia ya Tanzania imefanikiwa.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imeendelea kushiriki vyema katika Umoja wa Afrika, SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa upande wa Umoja wa Afrika tumepata heshima kubwa mwaka 2008 ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja huo. Tuliifanya kazi hiyo vizuri kiasi cha kufanya baadhi ya viongozi wenzangu kufikiria tuendelee kwa mwaka mmoja zaidi. Nilikataa kwa kusisitiza kanuni ya kila kiongozi kuwa Mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja.
Kwa upande wa SADC, tumeendelea kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli zote za Jumuiya hiyo ambayo inazidi kuimarika.
Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika miaka mitano hii tumeshuhudia utangamano ukizidi kuimarika na manufaa ya kiuchumi kwa Tanzania yakishamiri. Umoja wa Forodha umefikia hatua yake ya juu Januari 1, 2010 baada ya bidhaa za kutoka Kenya nazo kuruhusiwa kuingia katika masoko ya nchi wanachama bila ya ushuru. Tarehe 1 Julai, 2010, Soko la Pamoja limeanza na matayarisho ya Umoja wa Sarafu yameanza.
Mheshimiwa Spika;
Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania kuliko vile tulivyotazamia wote. Mwaka 2005 Tanzania iliuza katika soko la Afrika Mashariki bidhaa zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 161. Mwaka 2008 iliuza bidhaa za dola milioni 353.1, na mwaka 2009 mauzo yalipungua hadi dola milioni 272.1 kutokana na mtikisiko wa uchumi. Na, ukweli ni kwamba bado hatujatumia ipasavyo uwezo wetu na fursa zilizopo. Tuendelee kujipanga vizuri kuna manufaa makubwa zaidi mbele yetu.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika,
Nimezungumza kwa muda mrefu, sasa naomba nifikie mwisho. Yapo mambo mengi muhimu ambayo ningependa kuyazungumzia, mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokabiliana nazo, lakini natambua kwamba wapo Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wanataka kuwasha magari jioni hii hii na kuwahi majimboni.
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, naomba kuwashukuru kwa kipekee viongozi wa nchi yetu walionitangulia. Tumeendelea kuongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa kwa sababu ya misingi madhubuti iliyojengwa na waasisi wa nchi yetu: Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume. Pia, natambua mchango, ushirikiano na msaada wa ushauri wanaonipa Marais Wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee Benjamin William Mkapa ambao nao wakati wa uongozi wao liendeleza juhudi za ujenzi wa taifa letu kwa umahiri mkubwa.
Aidha, ningependa kurudia shukrani zangu za dhati kwa Watanzania wenzangu, kwenu Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kazi nzuri tuliyoifanya kwa kushirikiana katika miaka mitano iliyopita. Watanzania hatuna hulka ya kuyashikia bango na kuyasheherekea mafanikio yetu. Lakini kwa mafanikio tuliyoyapata katika miaka mitano iliyopita, ukizingatia mazingira tuliyopitia, tuna kila sababu ya kujipongeza. Naamini wananchi watatambua na kutuamini tena tuwaongoze.
Mheshimiwa Spika;
Wenzetu katika mataifa mengine wanatuona kama mfano wa kuigwa barani Afrika na wako tayari kutusaidia katika jitihada zetu. Hata hivyo, tusibweteke na sifa hizo. Bado kazi kubwa ipo mbele yetu. Nina imani kabisa kwamba kama Mwenyezi Mungu akiendelea kutujalia, na akituepusha na majanga ya hali ya hewa na mengineyo, na akabariki kazi za mikono yetu na akili zetu, tutapiga hatua kubwa zaidi na kwa kasi zaidi kuisukuma nchi yetu kwenye neema tele na watu wake kwenye maisha yaliyo bora. La muhimu kwetu ni kudumisha amani na utulivu, tuendelee kupendana sisi kwa sisi, tuipende nchi yetu na tujenge umoja na mshikamano. Wote tufanye kazi kwa bidii na maarifa kwani maisha bora hayatadondoka kama mana katika Jangwa la Sinai.
Mheshimiwa Spika,
Tunaelekea kwenye uchaguzi. Wengi wenu hapa mnaingia kwenye kinyang’anyiro. Nataka niwatakie kila la heri. Nami mnitakie heri ili tukutane tena Bunge lijalo na kipindi kijacho. Wananchi sasa ndio wakati wao wa kuamua. Sisi katika Serikali tumejiandaa na vyombo vyote husika vimejiandaa kwa uchaguzi huu kuwa wa amani, huru na wa haki kama ilivyo sifa ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza!
Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment