7/11/2010

Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM umefungwaMkutano Mkuu wa Tisa wa Chama Cha Mapinduzi umekwisha rasmi leo jioni na kufungwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Mkutano huo wa siku mbili ulitanguliwa na vikao vya Kamati Kuu siku ya Alhamisi na Halmashauri Kuu siku ya Ijumaa ambapo Dr. Ali Mohamed Shein alichaguliwa kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM.
Baadhi ya mambo yaliyojiri kwenye Mkutano Mkuu ni hotuba za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2005 - 2010. Hotuba hizi zilisomwa na Waziri Kiongozi - Zanzibar Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda.
Aidha Mkutano huo ulitoa mwelekeo wa sera ya CCM kwa miaka kumi ijayo, yaani 2010 - 2020. Mwelekeo huo ulitolewa kwa kifupi na Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu walipata nafasi ya kupiga kura ili kumpitisha mgombea pekee wa Urais kupitia CCM, Jakaya Mrisho Kikwete. Mheshimiwa Kikwete ambaye alichukua fomu ya kugombea Urais, ameomba ridhaa ya kugombea tena na kukamilisha awamu yake ya pili ya uongozi wa juu kabisa nchini Tanzania.

Katika uchaguzi huo, Mheshimiwa Kikwete aliibuka mshindi kwa asilimia 99.16 na hivyo kuthibitishwa rasmi na Mkutano kuwa ni Mgombea wa Urais atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.

Baada ya kuwashukuru wajumbe kwa kumpitisha kama mgombea, Mheshimiwa Kikwete alitoa hotuba yake na kuainisha mambo yaliyofanywa na serikali yake kama yalivyoahidiwa kwenye ilani. Pia aliainisha mambo atakayotarajiya kuyatekeleza pindi atakapopata ridhaa ya wananchi ili kuwaongoza kwa kipindi cha pili.

Mwisho kabisa Mheshimiwa Kikwete alimtangaza Dr. Gharib Bilal ndiye atayemsaidia kuipeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu, yaani Mgombea Mwenza.
Mkutano huu ulihudhuriwa na watu zaidi ya efu mbili wakiwemo wajumbe kutoka kila mkoa na wageni waalikwa kutoka vyama rafiki vya nje ya nchi, mabalozi, na vyama vya siasa ndani ya nchi.
Mkutano huu wa CCM ulirushwa hewani na televisheni za TBC1, Star TV, ITV and Channel Ten. Radio Uhuru pia walirusha matangazo ya radio siku zote mbili za mkutano.

Aidha kwa kupitia tovuti ya CCM, watanzania walioko nje ya nchi waliweza kuangalia mkutano huu kwa kupitia mtandao. Aidha wengine waliweza kutoa mchango wa mawazo, kuangalia picha na kusoma yale yote yaliyoendelea kupitia mitandao ya Twitter, Facebook, Youtube, na Blogspot kwa kupitia anuani ya JakayaKikwete2010.

No comments:

Post a Comment