8/29/2010

Dk. Bilal aahidi barabara Mtwara *Ni ile itokayo Mtwara kwenda Masasi *Itajengwa kwa kiwango cha lami mwakani


Na Happiness Katabazi , Mtwara

CHAMA cha Mapinduzi(CCM)kimeahidi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mtwara kupitia wilaya za Tandahimba na Newala na kisha kuungana na ile itokayo Lindi kwenda Masasi kwa kiwango cha lami ifikapo mwakani.

Hayo yamesemwa jana na Mgombea Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk. Mohamed Bilal wakati akihutubia kwa nyakati tofauti katika uwanja wa shule ya Msingi Mtiniko katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini na uwanja wa michezo wa Nahyanga wilayani Tandahimba, ambapo pia alipata fursa ya kumnadi Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara Vijijini Hawa Ghasia na mgombea ubunge wa Jimbo la Tandahimba, Juma Njwayo .

Dk.Bilal alisema chama chake kitakamilisha ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Km 219 na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kuichagua CCM ili iweze kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo.

Kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami kutakuwa kunatanua biashara na kazi za kiuchumi katika mkoa wa Mtwara, mkoa ambao katika siku zijazo unaonekana wazi kuwa utageuka kuwa moja ya mikoa ambayo ni kichocheo cha maendeleo ya Tanzania.

“Wananchi wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini na Tandahimba nawaombeni sana mkipe kura za ndiyo CCM ili kiweze kushika dola na ikishashika dola kitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kutekeleza ahadi hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo “alisema Bilal na kuongeza kuwa;

“Ahadi hii ipo katika ilani ya uchaguzi na taarifa nilizopata ni kuwa fedha za ujenzi wa barabara hiyo zipo na kazi inaendelea. Kama mtakuwa wavumilivu na kutupatia kura katika uchaguzi ujao, ni wazi mtakuwa katika nafasi nzuri ya kuona mafanikio hayo. Hili tunawaahidi na tuna uhakika wa kulikamilisha.”

Dk. Bilal pia alifafanua kuwa, katika siku za hivi karibuni na hasa baada ya kuingia madarakani kwa Rais Kikwete, ukanda wa mikoa ya Kusini umebadilika kwa kasi na kwamba uchumi wake unakuwa kwa kasi sana kwa sababu wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakilima mazao tofauti ya biashara ambayo yamekuwa yakiwaingizia kipato na taifa kwa ujumla.

“Mkoa wa Mtwara ulizoeleka kwa wananchi wake kulima zao la Korosho lakini hivi sasa hali ni tofauti kwani wananchi wake wameanza kulima Mananasi, miti ya Miembe , Choroko na Karanga na Mbaazi,”alisema Dk. Bilal na kushangiliwa na wananchi wa eneo hilo ambao walisikika wakisema barabara hiyo imekuwa ni kikwazo kwao.

Hata hivyo msafara wa mgombea huyo uliendelea kusimamishwa na wananchi katika vijiji vya Mbawala Juu, na Manguluwe. Wananchi hao walikuwa wakishinikiza mgombea huyo ashuke katika gari lake ili awasalimie na wao wapate nafasi ya kumueleza kero zao.

mwisho

No comments:

Post a Comment