8/21/2010

Kikwete azindua Kampeni Jangwani Leo

Maelfu ya wafuasi wa CCM wakiwasili kwa mbwembwe ndani ya Viwanja vya Jangwani Mjini Dar es salaam kushuhudia uzinduzi wa kampeni za Mwenyekiti wa CCM Jakaya Mrisho Kikwete.

Sehemu ya umati wa watu waliohudhuria uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi uliofanyika kwenye Viwanja vya Jangwani leo tarehe 21 Agosti, 2010.

Msanii wa kizazi kipya Diamond akiimba wimbo wake maarufu wa Mbagala ambao amegeuza maneno kuelezea mafanikio ya CCM tangu awamu ya kwanza hadi sasa.

Wasanii Chege na Mheshimiwa Temba nao walitumbuiza kwenye uzinduzi wa kampeni ambapo wao waligeuza wimbo wao wa TMK kuwa CCM Chama Kubwa.

Mwanamuziki Marlow na kundi zima la THT (Tanzania House of Talent) walikonga nyoyo za wana CCM pale walipoimba na kucheza staili ya KIDUKU wimbo wa Pipi CCM remix, wakiwaambia wapinzani wapishe njia Jakaya ndio Rais.
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika kwenye viwanja vya Jangwani kushuhudia uzinduzi wa kampeni zake.

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama tawala CCM (Chama cha Mapinduzi), na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amezindua kampeni zake leo kutetea nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi nchini Tanzania.

Kwenye hutuba yake fupi, Mheshimiwa Kikwete aliwaeleza wakazi wa Mkoa wa Dar es salaam waliofurika kwenye Viwanja vya Jangwani kwa maelfu, kwamba leo ni mwanzo wa kampeni zake na atapita kila jimbo kuelezea wananchi mafanikio ya serikali yake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na matarajio yake kwa miaka mitano ijayo iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi.

Akishangiliwa na umati mkubwa wa wafuasi wa chama chake na wakazi wengine wa mkoa huu, Mheshimiwa Kikwete alielezea ya kwamba CCM ni chama imara madhubuti na kina uzoefu wa muda mrefu. Hii ndio sababu vyama vingine vinalazimika kuiga mambo kadhaa kutoka CCM.

Akiwauliza wananchi wafuasi wa vyama vy upinzani, Mheshimiwa Kikwete alihoji maelfu ya wananchi wa mkoa wa Dar es salaam "Kwa nini mhangaike na photocopy na wakati original ipo? Chagueni CCM ndiyo original hawa wengine wote wanatuiga tu" alisema Mheshimiwa Kikwete alipokuwa akielezea sababu zake za kugombea Urais nchini Tanzania.

Hatahivyo Mheshimiwa Kikwete alilazimika kufupisha hotuba yake baada ya kuishiwa nguvu katikati ya hotuba hiyo. Baada ya kupumzika kwa dakika chache na kuchekiwa na daktari wake, Mheshimiwa Kikwete alirejea jukwaani na kuhitimisha hotuba yake iliyotuliza hofu ya wananchi waliofurika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam.

Mheshimiwa Kikwete anatarajiwa kuendelea na kampeni mikoani kesho akianzia mkoa wa Mwanza.

No comments:

Post a Comment