8/22/2010

Press Kikwete 2010: JK - Ni Matusi Kudai Sijali Wafanyakazi

Mgaya Kingoba, Mwanza

RAIS Jakaya Kikwete amesema ni matusi anapoambiwa kwamba hajali maslahi ya wafanyakazi nchini, wakati serikali yake imekuwa ikiboresha maslahi ya wafanyakazi mwaka hadi mwaka na kusisitiza kuwaheshimu wafanyakazi hao na itaendelea kuboresha stahili zao.

Aidha, amewaahidi mazuri zaidi Watanzania katika miaka mitano ijayo, akisema anataka kukumbukwa kwa mema katika uongozi wake, na si zaidi ya hayo.

Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akiomba kura za wananchi wa Jiji la Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ambako maelfu ya wakazi wa jiji hili walifurika kumsikiliza katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya mkoani Mwanza, ikiwa ni siku ya pili tangu azindue kampeni jijini Dar es Salaam.

Mgombea huyo wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema anaona hatendewi haki juu ya suala la maslahi ya wafanyakazi kwa sababu tangu aingie madarakani Desemba 2005, Serikali yake ya Awamu ya Nne imekuwa ikiboresha maslahi ya wafanyakazi mara kwa mara kadri uwezo unaporuhusu.

“Tumekuwa tukiboresha maslahi ya wafanyakazi tangu tuingie madarakani. Maslahi ya umma na sekta binafsi yamekuwa yakiboreka na tumeweka taratibu za kisheria na kuunda kamati za kisekta kushughulikia masuala ya maslahi.

Kuna watu walikuwa wanalipwa shilingi elfu arobaini na nane sasa wanalipwa zaidi ya shilingi themanini elfu,” alisema Kikwete na kuongeza: “Tulipoingia tulikuta kima cha chini ya mshahara ni shilingi elfu sitini na tano, tukapandisha hadi shilingi sabini na tano; kisha shilingi laki moja, na baadaye laki moja na nne na majuzi kimefika shilingi laki moja na thelathini na tano.

Kwa kweli tumeboresha maslahi hayo kila mara uwezo unaporuhusu. “Kwa hiyo, nikiambiwa mimi sijali maslahi ya wafanyakazi, ni matusi, naona sitendewi haki.”

Rais Kikwete alisema tofauti kati ya Serikali na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA) ni suala la kutaka kima cha chini kiwe Sh 315,000; jambo alilosisitiza kwamba kwa uwezo wa serikali sasa, haiwezekani.

“Mwenye grosari hawezi kulipa shilingi laki tatu, atakwambia nenda kajiajiri mwenyewe, vivyo hivyo kwa mwenye baa. Ndiyo tulichosema kwa Tucta, msemakweli mpenzi wa Mungu, hatukiwezi, mapato hayatoshi, leo hii ukilipa hivyo, utapata wapi fedha za ruzuku kwa wakulima, dawa, kununua vivuko,” alisema Rais Kikwete.

“Ndio maana tumesema si haki, haiwezekani… na ndipo msuguano wetu na Tucta. Tumewaambia haiwezekani. Lakini sasa wameyapindua, wanasema sizitaki kura za wafanyakazi.

Lakini wanasahau kauli zao za Dar es Salaam wakati wa Mei Mosi mwaka huu…walisema watamchagua kiongozi atakayewalipa shilingi laki tano na elfu kumi na tano. Na mabango yao yaliandikwa hivyo. Mla kunde anasahau, lakini mtupa maganda, hasahau.”

Rais Kikwete alisema kwamba kauli yake aliyoitoa haikuwahi kukataa kura za wafanyakazi, bali alieleza kuwa kama sharti ni hilo la kuongeza kima cha mshahara na kufikia Sh 315,000, “basi kura hizo tumezikosa.”

“Nilieleza kuwa kama sharti ni kuweka kima hicho cha chini, basi kura hizo tumezikosa. Hatutaweza kulipa kiwango hicho. Leo mbaya mie, wazuri wao, kweli akutukanaye hakuchagulii tusi.

“Tunawaheshimu wafanyakazi, ni watu muhimu, tutaendelea kuwaongeza maslahi kwa kadri ya uwezo wetu wa mapato na wajibu wa serikali. Hatuna ugomvi nao wala kinyongo.

Kura hata moja kwangu ni muhimu, siwezi kuikataa, lakini kama sharti ni hilo, kura hizo tumezikosa. Watatupa wengine.

“Hata hivyo, naamini katika wafanyakazi wapo wanachama wazuri wa CCM, wapenzi wa CCM, wanaojua chuya au pumba na mchele. Hivyo, tunaamini na sisi CCM tutapata kura za kutosha, kuongoza nchi hii.”

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya miaka mitano iliyopita, aliwaambia maelfu ya wananchi hao wa Mwanza kwamba imetekelezwa kikamilifu na ushahidi ni ujenzi wa vivuko mbalimbali; barabara za lami za jiji hilo na zinazokwenda mikoa mingine; uwezeshaji wa wananchi na uwekezaji.

“Kwa mtaji huo, nawaahidi mambo mazuri zaidi katika miaka mitano ijayo kwa kuwaachia nchi iliyo nzuri zaidi, kwani nataka Watanzania wanikumbuke kwa mema, sitaki nikumbukwe kwa lolote jingine,” alisema Rais Kikwete katika mkutano uliopambwa na burudani za aina mbalimbali hasa za muziki wa kizazi kipya.

No comments:

Post a Comment