8/30/2010

Uwanja Mpya wa Ndege Kujengwa Songwa

Na Mgaya Kingoba, Mbeya

UWANJA wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe mkoani Mbeya ambao ujenzi wake umekuwa ukisuasua, sasa unatarajiwa kukamilika Machi mwakani, wakati ndege zitakapoanza kuruka, imeelezwa.
Imeelezwa kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa uwanja huo kulitokana na kubadilishwa wazo la awali la kuwa na uwanja wa kawaida, na badala yake kujengwa uwanja wa kisasa wa kimataifa utakaohudumia watu wengi na hasa kupanua uwekezaji katika Ukanda wa Kusini.
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete alibainisha hayo leo alipowahutubia wananchi wa Mbalizi katika Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya kwenye Stendi Kuu ya Mabasi akiomba kura za wananchi ili kuongoza tena Tanzania.
Kikwete alisema wazo la awali la kujenga uwanja wa kawaida, lilibadilishwa na kuwa la kujenga uwanja wa kisasa wa kimataifa, lilibadilishwa na kuwa uwanja wa kimataifa, hivyo kazi ikabadilika na kusababisha ujenzi huo kuchukua muda mrefu kuliko ilivyopangwa awali.
“Novemba mwaka huu, kazi itakuwa imekamilika na kufikia Machi mwakani, ndege zitaanza kuruka. Zitaruka ndege kubwa za Boeing 747. Wachina wameshaanza kujenga jengo la kupokea abiria. Mbalizi itanufaika sana na ujenzi wa uwanja huu,” alisema Kikwete.
Alisema mbali ya wakazi wa Mbalizi na Mkoa wa Mbeya kunufaika na uwanja huo, pia watanufaika wafanyabiashara wa kilimo cha maua ambayo yatakuwa yanasafirishwa moja kwa moja kutoka uwanja huo wa ndege kwenda Ulaya, na hivyo maua hayo kutoharibika.
Akizungumzia upatikanaji wa maji katika mji huo wa Mbalizi, alisema kumaliza tatizo hilo, maji yatavutwa kutoka Mbeya Mjini, na kufikia Desemba mwaka huu, watapata meta za ujazo 45,000 ili kukidhi mahitaji ya mji huo na suala litakalobaki ni usambazaji wa mtandao wa maji.
Alizungumzia pia suala la umeme, akisema awamu ya kwanza itakuwa na vijiji vine na katika miaka mitano ijayo, vijiji vyote vya Mbeya Vijijini, vitakuwa vimepatiwa maji.
Akiwa amesimama katika mji wa Mlowo, aliahidi kumaliza tatizo la maji; kuhakikisha kunakuwepo na benki mjini humo; kupewa gari katika Kituo cha Polisi na kuongeza ruzuku ya pembejeo ya kilimo.
Mapema leo asubuhi, alihutubia mkutano wa kwanza katika Makao Makuu ya Wilaya ya Mbozi mjini Vwawa, ambako alisisitiza utulivu na amani nchini; kupeleka umeme vijijini na uwezeshaji wa wananchi.
Kesho Kikwete anatarajia kuzuru wilaya za Kyela, Rungwe na Mbeya Mjini.

No comments:

Post a Comment