8/02/2010

Mwenyekiti wa CCM achukua fomu za Urais




MGOMBEA urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 2010, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa wa CCM, leo, Jumatatu, Agosti 2, 2010, amechukua rasmi fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Mheshimiwa Kikwete ameanzia safari yake ya kwenda kuchukua fomu kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM mjini Dar es Salaam, Mtaa wa Lumumba, ambako yeye pamoja na Mgombea Mwenza, Dkt. Mohamed Gharib Bilal na viongozi wakuu wa chama hicho, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mzee Pius Msekwa na Katibu Mkuu Mzee Yusuf Makamba wameondoka kuelekea Makao Makuu ya Tume ya Taifa (NEC) kwa maandamano makubwa ya wana-CCM.

Maandamano hayo yamepitia mitaa ya Lumumba, Morogoro Road, Bibi Titi Mohammed, Ohio kabla ya kuingia Mtaa wa Ghana ambako ndiko ziliko ofisi za NEC.

Mheshimiwa Kikwete akiwa amesindikizwa pia na wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na familia yake, akiwamo Mama Salma Kikwete, na Mama Maria Nyerere, amewasili Makao Makuu ya NEC, Jumba la Posta, lililoko kwenye makutano ya Ghana Avenue na Ohio Street muda mfupi kabla ya saa sita mchana na kwenda moja kwa moja kwenye ofisi za Tume zilizoko ghorofa ya saba.

Mara baada ya kuwasili kwenye ofisi hizo amepokelewa kwenye chumba cha mikutano cha NEC na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Lewis Makame na Mtendaji Mkuu wa NEC, Bwana Rajab Kiravi na kuanza kuelezwa taratibu na masharti ya upokeaji fomu, urudishaji wake, na shughuli nyingine muhimu zinazotakiwa kufanyika ili kukamilisha zoezi hilo.

Miongoni mwa mambo mengine, Jaji Makame amemweleza Mheshimiwa Kikwete kuwa atahitaji kupata wadhamini wasiopungua 2,000 kutoka kila moja ya mikoa isiyopungua 10, ikiwamo miwili ya Tanzania Visiwani.

Ameelezwa vile vile kuwa fomu zilizojazwa ipasavyo zitatakiwa kurudishwa kwenye ofisi za NEC Agosti 19, mwaka huu, kabla ya saa 10 jioni.

Baada ya kuelezwa na kuelewa vizuri taratibu hizo, Mheshimiwa Kikwete alitia saini kitabu cha kumbukumbu kuthibitisha kuwa amekabidhiwa fomu hizo na akakabidhiwa nakala nne za fomu, nakala za fomu za maadili na kitabu cha maadili yatakayotawala shughuli nzima ya kampeni za mwaka huu.

Kufuatia maelezo ya Jaji Makame, Mheshimiwa Kikwete amemwambia Jaji Makame kuwa atafanya kila linalotakiwa na sheria katika kufanikisha zoezi hilo la kutafuta wadhamini na kurudisha fomu.

“Nakutakia kila la heri,” Jaji Makame amemweleza Mheshimiwa Kikwete baada ya hapo na Rais Kikwete akaondoka.

Mara baada ya kushuka kutoka ofisi za Tume, kwenye ngazi za Posta House, Mheshimiwa Kikwete na Dkt. Bilal wamezionyesha hadharani kwa mara ya kwanza fomu walizochukua na msafara wa wana-CCM, wapenzi na washabiki wa chama hicho ukaondoka kwa maandamano makubwa zaidi kuelekea tena Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM ambako kwa mara ya pili Mheshimiwa Kikwete amezionyesha tena fomu hizo.


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

02 Agosti, 2010

No comments:

Post a Comment