8/30/2010

Dk Bilal amfagilia Mkapa *Amtaja kuwa kiongozi mahiri kuwahi kuwapo Tanzania *Afafanua kuwa aliacha kasma ya mabilioni hazina

Dk Bilal amfagilia Mkapa
*Amtaja kuwa kiongozi mahiri kuwahi kuwapo Tanzania
*Afafanua kuwa aliacha kasma ya mabilioni hazina

Na Happiness Katabazi, Masasi
MGOMBEA mwenza wa nafasi ya urais kupitia CCM, Dk. Mohamed Gharib Bilal amewaambia wananchi wa Masasi kuwa, rais mstaafu wa awamu ya tatu ambaye ni mkazi wa jimbo la Masasi, Benjamin William Mkapa alikuwa ni kiongozi mahiri ambaye Tanzania imewahi kupata na akafafanua kuwa atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya Tanzania.

Dk Bilal amewahi kufanya kazi na Rais Mstaafu Mkapa wakati wa awamu ya pili, wakiwa pamoja katika Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu.

Dk Bilal aliyepo hapa Masasi akitokea Newala mkoani Mtwara anafanya mikutano ya kampeni na baada ya mkutano wake wilayani Masasi, alifanya mkutano mwingine katika wilaya ya Nanyumbu eneo la Mangaka.
Mgombea huyo mwenza alifafanua kuwa, uongozi wa Mkapa uliingia madarakani katika kipindi cha mabadiliko ya uchumi hali iliyoifanya Tanzania kuwa katika kipindi kigumu, lakini alifanya kazi kubwa katika kipindi cha utawala wake, hali iliyoifanya Tanzania kubakia na kasma ya kutosha Hazina wakati anatoka madarakani.

“Kila nikifika hapa nakumbuka majina ya viongozi mahiri waliotoka hapa. Nafahamu jambo kubwa walilolifanya kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania. Kila siku nitawakumbuka mzee Mkapa na Mama Anna Abdallah. Wote hawa wamefanya makubwa ya kuenziwa katika Tanzania,”alisema na kuongeza;

“Wana Masasi mkipigieni kura chama cha Mapinduzi kwa kuwa kinawajali na kina ilani inayotekelezeka. Tena tambueni kuwa hiki ndicho chama pekee kinachogusa maendeleo ya wanyonge.”

Awali akinadi ilani ya chama cha Mapinduzi kwa mamia ya wakazi wa wilaya ya Masasi, Mgombea Mwenza Dk. Bilal alisema, kila anapoitazama Tanzania na kukitazama chama cha Mapinduzi anakumbuka namna njema ya utumishi uliotukuka uliomo miongoni mwa wananchi sambamba na viongozi wa chama hicho.

“Ndani ya chama chetu kuna viongozi mahiri ambao wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya maendeleo yetu. Wanajituma kwa nguvu zao zote na wana hakikisha kuwa kila jambo linalotakiwa na wananchi analipatia utatuzi,” alisema.
Dk. Bilal amekuwa katika kampeni katika mkoa wa Mtwara tangu juzi na leo anaanza kampeni katika mkoa wa Ruvuma. Tangu aingie katika mikoa yaKusini, amegeuka kuwa kivutio kwa wanachi ambao mara kwa mara wamekuwa wakisimamisha a msafara wake na kumtaka awasalimu.

Mwisho.

1 comment:

  1. dr. Ben, alituacha kenye running track 2005, in 2015 dege lita kuwa juuu. 2010 jk 4u

    ReplyDelete