8/23/2010

Tuliahidi, Tumetekeleza - Geita, Mwanza

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dr.Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Geita jana jioni.

Mheshimiwa Kikwete leo ametangaza kuwa Geita itakuwa mkoa rasmi kuanzia Januari mosi, 2011. Pia ametumia nafasi hiyo kutangaza wilaya mbili mpya za Geita na Nyangwale zilizoanzishwa ili kurahisisha shughuli za maendeleo mkoani Geita.

Rais Kikwete amezungumza hayo alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara Wilaya ya Geita Mkoani Mwanza leo katika siku ya tatu ya mzunguko wa kampeni za Mheshimiwa Kikwete za kugombea urais kupitia tiketi ya CCM.

Mheshimiwa Kikwete alielezea mamia ya wananchi wa Geita kuwa katika kipindi cha urais wake amekuwa akifikiria njia rahisi ya kufikisha huduma za kijamii kwa watanzania wengi kwa sababu ya ukubwa wa nchi yetu. Alisema haswa mikoa ya Mwanza na Shinyanga peke yake ina watu zaidi ya milioni saba.


Hivyo serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete imefanya uamuzi wa kugawanya mkoa wa Mwanza na kufanya Geita mkoa na Wilaya ya Geita kuwa makao makuu ya Mkoa huo mpya ambao utaanza Januari 1, 2011.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana wilayani hapo, Mheshimiwa Rais alisema kwamba mwaka 2005 aliahidi kujenga barabara ambayo sasa imejengwa na imekamilika. Akasema akichaguliwa tena serikali yake itajenga barabara kwenda Nyamwale na Bukongo.

Kwenye upande wa elimu, Mheshimiwa Kikwete aliwapongeza wananchi wa Geita kwa kujenga shule nyingi za Sekondari. Alisema Geita ina kata 33 lakini ina shule za sekondari za kata zisizopungua 44. Haya ni maendeleo makubwa.

Mwisho kabisa Mheshimiwa Kikwete aliwatambulisha wabunge wa Sengerema na wa Geita ambao walishangiliwa kwa hamasa kubwa na umati wa watu waliofika kwenye mkutano huo.
Alipomtambulisha mgombea wa ubunge kutokea Geita, Donald Max umati wa wananchi wa Geita ulishangilia kwa shangwe kubwa wakinyoosha mikono kwamba watamchagua kwa kura zote.

Pia wote kwa pamoja waliwaomba wananchi kuwapigia kura CCM madiwani, wabunge na rais wa CCM. Kwa upande wake Mheshimiwa Rais ameawaomba wananchi wa Geita kuchagua CCM ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano.

No comments:

Post a Comment