8/31/2010

Mkutano wa Kampeni: JK afunika mkoani Mbeya ateka maelfu
Na Joachim Mushi
Mbeya
MGOMBEA nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete jana alipokelewa kwa namna ya pekee na umati mkubwa wa wanachama na wapenzi wa chama hicho katika uwanja wa Sokoine mjini hapa.
Makundi ya wanachama na wapenzi walianza mapokezi kwa kujipanga pembezoni mwa barabara wakimsubiri kutokea Wilaya ya Rungwe ambapo alifanya mkutano wa kampeni kabla ya kuja Mbeya mjini.
Akiwa njiani polisi ndio kundi lililokuwa na kazi ya kuwazuia wanachama na wananchi wengine waliokuwa wakitaka kuzuia msafara wake kuelekea uwanja wa Sokoine, wakitaka asimame kuwasalimia.
Hata hivyo mgombea huyo akiwa njiani alilazimika kusimama baadhi ya maeneo kama vijiji vya Ntokela na Uyole ya Chini kuwasalimu na kuwaomba kura wananchi.
Katika uwanja wa Sokonine alipokelewa na maelfu ya wanachama na wapenzi wa CCM, maandamano makubwa ya pikipiki na baiskeli makundi ya akinamama, vijana pamoja na vikundi mbalimbali vya burudani.
Machifu wa Mbeya walimvisha shuka, kumkabidhi mkuki, kiti kama ishara ya heshima ya uchifu na kumtakia ushindi mkubwa na uongozi bora akiingia Ikulu.
Awali akiwahutubia wananchi wa Mjini wa Tukuyu wilayani Rungwe Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, alisema Serikali kwa sasa haitakuwa ikipeleka nje tena wagonjwa wa maradhi ya moyo baada ya huduma hiyo kuanza kutolewa nchini.
“Hatupeleki mtu nje sasa kwa matibabu kama haya kama ilivyokuwa hapo awali kwani tayari madaktari wetu wanafanya kazi hizo hapa hapa…pia tunafanya mazungumzo na madaktari bingwa wengine ili kuweza kushirikiana kuboresha huduma za afya,” alisema Kikwete.
Akizungumzia uboreshaji wa huduma kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi, Kikwete alisema Serikali ya CCM kwa kuwajali wagonjwa hao imehakikisha dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs) zinatolewa bure ili kuwasaidia waathirika.
“Kama kuna wagonjwa wowote wa Ukimwi ambao bado wanauziwa dawa hizo watoe taarifa kwa viongozi wa Serikali katika maeneo yao, kwani dawa hizi zinatolewa bure kwa wahusika,” alisema Kikwete.
Hata hivyo aliwataka wana-Rungwe kuwa makini na ugonjwa wa Ukimwi kwani unaweza kuzuilika endapo watafuata mafundisho ya viongozi wa dini anuai pamoja na wale wa Serikali.
“Kuupata ugonjwa huu si kwa dharura hata kidogo maana watu wanapanga siku, muda na sehemu…mimi naongeza linguine kama yametushinda ya viongozi wa dini basi tupange na kinga ya ugonjwa huo kabla ya kwenda kwenye tukio,” alieleza Kikwete.
Kikwete, ambaye wilayani Rungwe aliongozana na wagombea ubunge majimbo ya Rungwe Mashariki na Magharibi-Profesa Mark Mwandosya na Profesa David Mwakyusa aliahidi kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Katumba kwenda Mbambo na Tukuyu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment