8/29/2010

Mkutano wa Kampeni Kate, Matai, Laela na Tunduma – JK Epukeni Vyama Vya Uchaguzi

Agosti 29, 2010


. Asema uchaguzi ukimalizika, havionekani tena


. Kulivalia njuga tatizo la watumishi kutoripoti mikoani


. Vijana wa Chadema wamshangilia, lakini…


Na Mgaya Kingoba, Sumbawanga


MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kutochagua vyama ambavyo vinaonekana wakati wa Uchaguzi Mkuu tu, badala yake wakichague chama hicho tawala kwa sababu kipo na wananchi wakati wote.

Amesema CCM imekuwa na wananchi wakati wote tangu enzi za TANU na ASP na zaidi, kimekuwa katika maeneo wanayoishi wananchi ambako wanaweza kupeleka shida zao kwa viongozi waliopo katika maeneo yao na shida hizo kutatuliwa.


Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mikutano ya kampeni ya kuomba kura kwa wananchi wa Rukwa katika maeneo ya Kate, Matai na Laela, kabla ya kuingia mkoani Mbeya alikohutubia Tunduma wilayani Mbozi na Itumba wilayani Ileje.

"Chagueni CCM, ni chama kilichoenea kila mahali, mnacho wakati wote na mkiwataka
viongozi wake mnajua wapi kwa kuwapata. Msichague vyama ambavyo mnaona wakati wa uchaguzi, na baada ya uchaguzi hamuonani tena. Hivyo ni vyama vya uchaguzi," alisema Kikwete.


Alisema CCM ni chama kilichopo wakati wote, mafanikio yake yanaonekana, kazi
iliyofanyika inaonekana na kwamba hakitoi ahadi kwa nia ya kuchaguliwa au
kuwadanganya watu.

"Tuliposema tutaleta maendeleo kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, haikuwa
ahadi ya uongo…ilikuwa ya dhamira ya dhati kutoka mioyoni mwetu, haikuwa ahadi
ya uchaguzi. Haikuwa kauli ya maneno, ilikuwa kauli ya dhamira ya dhati," alisema Kikwete anayeomba miaka mingine mitano Ikulu.


Akiwa Laela, aliwahakikishia wananchi wa mji huo kwamba serikali ya CCM italishughulikia suala la maji na tayari imeanza mipango na itachangia fedha baada ya wananchi kutoa Sh milioni sita.


Aliahidi pia kujenga lami katika miinuko mikali kwenye barabara za Nyangalua-Chome na Ilemba, na pia kuhakikisha umeme unafika katika maeneo ambayo hayana nishati hiyo kwa sasa.


Kuhusu watumishi wanaopangwa kufanya kazi mkoani Rukwa kutofika katika vituo walivyopangwa, alisema serikali italifuatilia kwa karibu tatizo hilo ili kuhakikisha mikoa ya pembezoni , haithiriki kiutendaji kwa watumishi wa umma kukataa kuripoti kazini.


Akihutubia mjini Matai, alisisitiza kuwa serikali itanunua tani 400,000 za mahindi kila mwaka nchi nzima, badala ya tani 150,000 za sasa, kwa sababu uzalishaji umekuwa mkubwa.


Aliwataka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuacha kutoa sababu alizoziita za kitoto za kushindwa kununua mahindi ya wakulima kwa madai kuwa hawana mizani za kutosha. Aliwataka wanunue haraka mahindi hayo ili yasikutwe na mvua.


Akiwa Tunduma, alikiri kuwa mji huo unakabiliwa na tatizo la maji, lakini limeanza kufanyiwa kazi ikiwemo kutengwa kwa zaidi ya Sh milioni 450, na katika miaka mitano ijayo, litamalizwa kabisa.


Kuhusu msongamano wa malori mpakani hapo yakiwa yanakwenda nchini Zambia, alisema amezungumza na Rais Rupiah Banda, na kukubaliana kuwa malori hayo yakishamaliza taratibu za forodha upande wa Tanzania, yaruhusiwe kuvuka kuingia Zambia, na hilo limekubaliwa.


Hata hivyo, katika mkutano huo uliofurika maelfu ya watu, kundi la vijana ambao baadhi yao walikuwa wameshika chupa zenye bia mkononi na wakiwa juu ya mapaa ya nyumba katika eneo la Uwanja wa CCM mjini Tunduma, walikuwa wakipiga kelele wakati mkutano huo ukiendelea.


Vijana hao walimshangilia mgombea huyo wa Urais wa CCM, lakini hawakuwa na makeke kama hayo wakati alipotambulishwa mgombea wa ubunge Mbozi Magharibi, Lukas Siyame.


Baada ya mkutano huo, vijana hao waliandamana mjini humo huku wakinyoosha juu vidole viwili vya mkononi; alama inayotumiwa na chama cha siasa cha Chadema, na baadhi yao waliwavamia watu waliovaa sare za CCM na baadhi ya magari ya watu waliofika kwenye mkutano huo.


Kesho mgombea huyo wa CCM atafanya mikutano katika Makao Makuu ya Wilaya ya Ileje mjini Vwawa na kuendelea na kampeni katika miji ya Chunya, Mbeya Mjini na Vijijini.

No comments:

Post a Comment