8/02/2010

Mwenyekiti wa CCM Taifa ahutubia umati mkubwa CCM Lumumba

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiwa kwenye mazungumzo mafupi na Mama Maria Nyerere muda mfupi kabla ya kuelekea Ofisi za CCM Lumumba jijini Dar es salaam na baadae kuchukua fomu.

Umati wa wanachama wa CCM walifurika kwenye viwanja vya ofisi ndogo ya CCM Lumumba wakimsikiliza Mwenyekiti akiwaasa kufanya kampeni makini lakini za kistaarabu.


Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea Urais kupitia CCM Mheshimiwa Jakaya mrisho Kikwete akiwahutubia wana CCM kuwa imara kipindi cha uchaguzi na kutokumpuuza adui. Alisema ni lazima kupata ushindi na hivyo kumtaka kila mwana CCM kufanya jitihada ya kuhakikisha ushindi wa "mafiga matatu" nchi nzima.

Msafara wa magari yaliyowabeba Mgombea Urais CCM Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Mwenza Mheshimiwa Gharib Bilal ukitokea ofisi za NEC kuelekea Lumumba.

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewahimiza wana-CCM kutumia mtandao wao mkubwa na mpana wa kisiasa kuhakikisha kuwa wananchi wanajitokeza kwa wingi kukipigia kura chama hicho Oktoba 31, mwaka huu, 2010.

Aidha, Mheshimiwa Kikwete amewatahadharisha wana-CCM dhidi ya hisia za kudharau wapinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hata kama CCM imetawala kwa miaka mingi.

Vile vile, Mheshimiwa Kikwete amewapongeza Wazanzibari kwa kufanikisha kura ya maoni ambayo imefungua njia ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja visiwani humo.

Mheshimiwa Kikwete pia amekemea tabia ya baadhi ya vyama vya siasa kutumia matusi, ubabe na vikundi vya wahuni wakati wa kampeni kwa nia ya kuruvuga mikutano ya vyama pinzani ama kuwatukana wanasiasa wapinzani.

Rais Kikwete ameyaeleza hayo leo, Jumatatu, Agosti 2, 2010 wakati alipowahutubia mamia kwa mamia ya wana-CCM na wananchi wengine kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es Salaam, waliojitokeza kumsindikiza na kupokea baada ya kuwa amechukua fomu ya kuwania tena urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mheshimiwa Kikwete amesema: “CCM ina mtandao mkubwa na mpana sana. Tuhakikishe watu wanajitokeza kwa wingi kukipigia chama chetu kura kwa kutumia mtandao wetu huu unaokwenda hadi chini kabisa katika jamii. Uhodari wa kiongozi utapimwa kwa kuhakikisha watu wake wanajitokeza kupiga kura. Tufanye kampeni nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa.”

Kuhusu dharau kwa vyama vya upinzani, Mheshimiwa Kikwete amesema: “Tusidharau wapinzani wetu hata kama tumetawala miaka mingi. Kwenye vita usidharau adui na tukumbuke kuwa uchaguzi wowote hauishi mpaka matokeo yametangazwa na washindi wamepatikana. Kwenye uchaguzi wa mwaka huu ni lazima tutumie nguvu nyingi kuliko adui. Tujitume usiku na mchana na tufanye kampeni kama vile tunaweza kushindwa,” amesema Mheshimiwa Kikwete na kuongeza:

“Tuache kudharau adui. Tuthibitishe nguvu zetu kwenye kura. Tunadi sera zetu. Wenzetu watapimwa kwa maneno yao tu, kwa kupepesa midogo. Sisi kazi yetu kubwa zaidi. Tutapimwa kwa mafaniko yetu ya miaka mitano iliyopita na hivyo lazima tufanye kampeni kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi.”

Kuhusu kura ya maoni ya Zanzibar, Mheshimiwa Kikwete amesema: “Napenda kuwapongeza Wa-Zanzibar kwa uamuzi wao wa busara wa juzi kwa kuamua kuchagua Serikali ya Umoja. Najua kuwa kila chama cha siasa hupenda chenyewe kushinda uchaguzi na kuunda Serikali, lakini yapo mazingira ambako lazima ushinde na mwenzio. Na hiyo ndiyo hali iliyoko Zanzibar.”

Mheshimiwa Kikwete ameeleza kuwa makubaliano ya kuunda Serikali ya Umoja yalikuwemo kwenye hata Mwafaka wa kwanza kati ya CCM na CUF. Pia ameeleza kwa urefu uzoefu wa nchi nyingine katika uundaji wa serikali za namna hiyo ikiwa ni pamoja na katika nchi za DRC, Afrika Kusini, Kenya na Zimbabwe.

Kuhusu tabia ya matusi, Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa yeye binafsi hasumbuliwi na ushindani wa kawaida wa kisiasa. “Wapo watu watatusema. Hili halinipi wasiwasi hata kidogo kwa sababu hata tufanyeje kuna watu wasiotupenda na watatusema tu. Na watu hawa muhimu wawepo ili demokrasia yetu iweze kukua. Hivyo tunahitaji kuwepo vyama vingi na vyenye nguvu.”

Lakini ameongeza: “Linalonisumbua mimi ni tabia ya kutukanana, kufanyiana fujo, kuandaa vikundi vya wahuni kuvunja mikutano ya wenzio, kupiga watu badala ya watu kunadi sera zao na kuwaachia wananchi nafasi ya kupima na kuamua wenyewe. Kuna watu wasiojua bado kuwa fujo hufukuza kura.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

02 Agosti, 2010

No comments:

Post a Comment