Na Happiness Katabazi, Mtwara
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kivuko cha Kilambo kwenda nchini Msumbuji na kile Msangu Mkuu mkoani hapa vitakuwa vimeanza kutoa huduma ya usafiri.
Hayo yalisemwa leo na mgombea mwenza wa (CCM), Dk. Mohamed Gharib Bilal wakati akiwahutubia wakazi wa wilaya za Newala, Masasi na Nanyumbu mkoani hapa katika mikutano yake ya kampeni iliyofanika katika Kata ya Namionga wilaya ya wilaya ya Newala, uwanja wa SIDO uliopo katika kijiji cha Lukuledi wilayani Masasi na uwanja wa Mangaka wilayani Nanyumbu.
Dk.Bilal alisema anafahamu jinsi wananchi wa mkoa huu wanavyoteseka na ukosefu wa vivuko hivyo na ndiyo maana serikali ya CCM ilikwishatenga fedha ya kununulia vivuko hivyo na kuongeza kuwa tayari wataalamu wameishanunua vifaa vya kuunganishia vivuko hivyo na muda wowote vitaingizwa nchini kwaajili ya kuanza kuviunganisha.
“Tunawaomba wakazi wa Mtwara na wilaya zake muwe wavumilivu na mvute subira kwani ifikapo mwisho mwaka huu, vivuko hivyo vitakuwa vimeishaingia chini na kuanza kufanyakazi….na hiyo yote inatokana na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya CCM ambayo siku zote ina dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi wake,” alisema Dk.Bilal.
Mgombea huyo aliwakumbusha wananchi hao kwamba ifikapo Oktoba 31 mwaka huu, kwa amani wakipigie kura za ndiyo chama hicho ili kuweze kutwaa madaraka na kuweza kuwaletea maendeleo zaidi na kuongeza kwa kuwaomba wamchague rais Jakaya Kikwete, wabunge na madiwani wa CCM.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge wa Jimbo la Newala, George Mkuchika ambaye pia Waziri wa Habari na Utamadini, mgombea ubunge wa jimbo Nanyumbu, Danstan Mkapa na mgombea ubunge wa jimbo la Masasi Mariam Kasembe na kuwaomba wananchi hao wawapatie wabunge hapo kura za ndiyo. Jana Dk.Bilal amemaliza ziara yake mkoani hapa na leo anaanza ziara mkoani Ruvuma.
No comments:
Post a Comment