8/22/2010

Mkutano wa Kampeni Misungwi, Mwanza: JK - Sina Deni na Wana Misungwi

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Rais Jakaya Kikwete akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho wa Jimbo la Misungwi Mwanza Charles Kitwanga jana akiwa ni mbunge wa kwanza kunadiwa na Mwenyekiti huyo wa CCM ambaye kaanza rasmi ziara ya mikoani.

Na Richard Makore, Mwanza
MGOMBEA wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete amesema hana deni na wananchi wa wilaya ya Misungwi kwa mkoani Mwanza kwa kuwa ahadi zote alizozitoa mwaka 2005 amezitekeleza.
Kadhalika, amewataka wananchi kuwa makini na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi wanaotafuna fedha kama mchwa.
Aliwaomba wananchi hao kumuamini tena kwa miaka mitano ili aweze kuendeleza jitihada za kuwapatia maendeleo ya kweli.
Aliyasema hayo wilayani Misungwi katika mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na mamia ya wananchi.
Alisema kazi ya Chama cha Mapinduzi ni kuahidi na kutenda na kwamba ahadi hiyo ameweza kuitekeleza kwa vitendo.
Rais Kikwete ambaye alizungumza na wananchi hao kwa ukakamavu wa hali ya juu alisema anaomba wananchi hao wachague mafiga matatu yaani Madiwani, Wabunge na Rais kwa kuwa wasipofanya hivyo hawatakuwa wamekisaidia chama chake CCM.
Kuhusu matumizi mabaya ya fedha za serikali alisema viongozi wanatafuna fedha wao wanazidi kunenepa huku wananchi wakizidi kukonda.
Katika Uwanja wa CCM Kirumba Maelfu ya ya wapenzi wa Chama cha Mapinduzi CCM walifurika katika uwanja huo kwa ajili ya kumsikiliza mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Kiwete.
Kampeni hizo zilipambwa na wasanii mbalimbali wa muziki na kuwafanya wapenzi wa CCM kufurika katika uwanja huo.
Kabla ya kuhutubia maelfu ya wanachama hao, Rais Kikwete aliwashukuru wasanii mbalimbali walitumbuiza uwanjani hapo na kuvuta idadi kubwa ya wananchi.
Kwa upande wake, mgombea mwenza, Dk. Ghalibu Bilal aliwataka wananchi mkoani Mwanza kukiamini CCM ili kiweze kuwaletea maendeleo ya kweli.
Aliwaomba wananchi kutumia mawe matatu yaani madiwani, ubunge na urais kutoka Chama Cha Mapinduzi.
Baadhi ya wasanii hao ni pamoja na Malow, Flora Mbasha, Mheshimiwa Temba, Juma Nature, Tot ambapo walitumbuiza wananchi wengi waliongia uwanjani hapo.
Makundi ya watu wengine yaliyohudhuria kampeni hizo ni pamoja na umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyopo mjini hapa.
Rais Kikwete aliwatambulisha wagombea wa udiwani na ubunge katika majimbo ya Misungwi, Ilemela na Nyamagana.
Kwa mujibu wa ratiba ya kampeni hizo kesho Rais Kikwete ataendelea na kazi hiyo katika Wilaya ya Geita na Sengerema mkoani humu.
Wakati huo huo, Rais Kikwete aliahidi kuwa wataimarisha ulinzi katika ziwa Victoria dhidi ya ujambazi katika eneo hilo
Pia vivuko alisema serikali imejitahidi kuvijenga na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa malalamiko kuhusu vivuko kama yapo ili serikali ijiandae kuvijenga.
Alijivunia kuwa Rais wa kwanza kuonana na Rais wa Marekani mara alipoingia madarakani hatua ambayo alisema imesaidia kujenga urafi na ushirikiano na hatimaye kupatiwa misaada.
Alijivunia kujenga mradi wa Sh. Bilioni zaidi ya 200 kuvuta maji kutoka Mwanza hadi mkoani Shinyanga na kusema serikali ikidhamiria inaweza.

No comments:

Post a Comment