10/16/2010

Kikwete aiteka Bagamoyo, Mlandizi na Chalinze

 
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dr.Jakaya Kikwete akihutubia maelfu ya wananchi katika mji mdogo wa Mlandizi, wilayani Kibaha leo mchana.
 Aahidi kumwaga mabilioni mengine ya mikopo.

Ataanza kusaka kura kesho Dar es Salaam.

Na Joseph Mwendapole, Bagamoyo.MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete, jana aliuteka kwa muda mji wa Bagamoyo kutokana na umati mkubwa wa watu, wengine wakiahirisha shughuli zao kwa muda kwenda kumsilikiliza katika mfululizo wa kampeni zake za kuwania kurejea Ikulu kwa awamu ya pili.

Kikwete leo alifanya mikutano mitatu akianzia Mlandizi, Bagamoyo na mwisho alimalizia jimbo la Chalinze ambako nako alipokelewa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kumpokea wakiwa na mabango mbalimbali ya kupongeza kutokana na juhudi zake za kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya ya CCM ya mwaka 2005.

Baadhi ya mabango yalisomeka hongera Kikwete kwa kudumisha amani, hongera Kikwete kwa kusimamia Ilani ya CCM, hongera Jakaya tuna imani na wewe, Kikwete karibu nyumbani na mengine yakisema kabidhi nchi kwenye mikono salama CCM, chagua Kikwete kwa maisha bora.

Alipoingia Mlandizi asubuhi jana, Kikwete alipokelewa na umati mkubwa wa watu wakiwemo waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda waliokuwa wakipeperusha bendera za CCM hadi uwanja wa mkutano katika jimbo hilo la Kibaha vijijini, ambako alifanya mkutano kabla ya kuelekea wilaya ya Bagamoyo.

Akiwa Mlandizi, Kikwete alisema serikali itaendelea kuimarisha mfuko wa uwezeshaji 'mabilioni ya JK' katika miaka mingine ijayo ili wananchi wengi zaidi waweze kupata mikopo hiyo nafuu na kujikwamua katika lindi la umaskini.

Alisema mifuko mingine ya kukopesha wananchi itaendelea kuimarishwa katika miaka mingine mitano ili iweze kufanya kazi ya kukopesha wananchi waweze kufanya biashara mbalimbali na kijikwamua kiuchumi kama walivyonufaika na mfuko wa uwezeshaji 'mabilioni ya JK'.

"Ndugu zangu mwaka 2005 tuliahidi mengi na tumetekeleza, tumefanya mengi mazuri na ahadi yangu kwenu ni kwamba mkituchagua tutazidi kufanya mengi mazuri, sisi ni waaminifu tukiahidi tunatekeleza, ombi lenu la kutaka kituo cha afya cha mlandizi kiwe hospitali ya Wilaya ni stahili yenu na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inawezekana," alisisitiza Kikwete.

Alisema wataalamu kutoka Israel watakuja nchini kwa ajili ya kuwafundisha watanzania kilimo cha mboga mboga hasa zao la nyanya ili walime kibiashara kwani soko la nyanya hivi sasa ni la uhakika.

Alisema kuwasili kwa wataalamu hao kutawasaidia wakulima wa nyanya hasa wa bonde la mto Ruvu kulima kwa nguvu zaidi na kwa utaalamu mkubwa na itakuwa rahisi kwao kuondokana na umaskini kwani nyanya zinahitajika kwa wingi zaidi maeneo mbalimbali duniani.

Kuhusu huduma ya maji na umeme, Kikwete aliwahakikisha wananchi hao kuwa serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi zaidi na kwa upande wa maji alisema Benki ya Dunia (WB) inashirkiana na serikali kusambaza maji katika vijiji 10 kwa kila Wilaya nchini.

Kwa upande wa kilimo, alisema serikali kwa miaka mitano ijayo itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo na kwamba wakulima wa korosho watakuwa wakiuziwa surphur kwa bei nafuu ili watu wasio na uwezo wamudu kuinunua.

Aizungumzia mifugo, Kikwete alisema serikali imeandaa mpango mkubwa wa kuendeleza mifugo ambapo wafugaji watalazimika kuwa na malisho ya uhakika kwa mifugo yao na kuachana na ufugaji wa kizamani wa kuhama hama ambao umekuwa ukisababisha migogoro.

"Huu ufugaji wa kuhama hama lazima ufikie kikomo, tabia hii imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro maeneo mbalimbali nchini tunataka kila anayefuga awe na chakula cha mifugo yake ili kuepusha migogoro baina ya wafugaji na wakulima, kama unafuga hakikisha una uwezo wa kulisha mifugo yako," alisisitiza Rais Kikwete.

Akihutubia katika uwanja wa Mwanakalenge mjini Bagamoyo, ambapo pia alipata mapokezi makubwa kama ilivyokuwa Mlandizi, Kikwete aliwaahidi wananchi kuwa wakiichagua CCM ataendelea kudumisha amani na utulivu na kusimamia utoaji wa huduma muhimu kwa jamii kama umeme, maji, barabara, elimu na afya.

Kikwete aliponda kejeli za wapinzani wanaopita wakiwarubuni wananchi kuwa serikali haijafanya kitu tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961 na aliwataka wananchi hao wawahoji watu hao maendeleo yanayoonekana sasa yameletwa na watu gani kama sio serikali ya CCM.

"Ndugu zangu haya yote mazuri mnayoona ni matunda ya uongozi thabiti na makini wa CCM na ukiona vyaelea vimeundwa na muundaji si mwingine ni CCM, hao wakipita na kuwadanganya kuwa hakuna maendeleo yaliyopatikana msiwaache hivi hivi waulizeni hizo huduma za jamii wanazotumia kama barabara, maji, shule, vyuo vikuu vimeletwa nanani, maana wasiwadanganye nanyinyi mkakubali tu," alisema Kikwete na kushangiliwa na wananchi hao.

Alisema utafika wakati Bagamoyo itasimama yenyewe kama mji wa viwanda na Bandari tofauti na ilivyo sasa ambapo mji huo uko chini ya kivuli cha Dar es Salaam.

Kikwete alisema mji wa Dar es Salaam haukutenga maeneo ya viwanda na sasa umeshajaa hivyo ni fursa nzuri kwa watu wa Bagamoyo kutenga maeneo na kuyapima kwa ajili ya uwekezaji.

"Hi ni fursa nzuri kwenu yapimeni maeneo hasa yale ya kandokando ya barabara na msipopima shauri yenu, yale maeneo yatakuwa na thamani kubwa sana kwenu mkiyapima lakini naamini hapa mnaviongozi thabiti wa kufanya kazi hiyo," alisema Kikwete.

Baada ya kuzunguka muda mrefu akisaka kura katika mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani, mgombea huyo wa CCM leo anatarajiwa kuanza kampeni katika majimbo ya Dar es Dalaam.

No comments:

Post a Comment