10/23/2010

Mkutano wa Kampeni Gairo: Wagombea udiwani na mbunge wamshukuru JK

Mgombea udiwani wa Kata ya Gairo wilayani hapa Mama Juliana Mwenda leo amemwagia sifa kem kem Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa jitihada zake binafsi za kuleta maendeleo Gairo.

Mama Mwenda ameyasema hayo wakati akiomba kura kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi kwenye mkutano mkubwa wa kampeni ambao Mheshimiwa Kikwete alitoa hotuba yake ya kampeni.

Mama Mwenda ambaye anatetea kiti hicho cha udiwani alisema anamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwaletea Wilaya mpya ya Gairo kwani kwa kufanya hivyo kunaharakisha kasi ya maendeleo mahali hapo.

Kwenye upande wa elimu, Mama Mwenda alipongeza sera za upanuzi wa elimu ya sekondari zilizotekelezwa na CCM chini ya uongoze wa Mheshimiwa Kikwete. Alisema kwamba ndani ya Kata yake sasa kuna shule za sekondari tatu na mwaka huu wa 2010 zaidi ya watoto mia sita wamefaulu kuendelea na masomo ya sekondari.

Mama Mwenda pia alimpongeza Mheshimiwa Kikwete kwa kuipa kipaumbele afya ya wakina mama wajawazito na watoto ambapo kwa kushirikiana na wafadhili, wana Gairo wameweza kupatiwa wakunga waliopata mafunzo ya viwango. Na sasa wakina mama wengi wanajifungua salama kwa utaalamu wa wakunga hao.

Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Bwana Ahmed Shabibi aliwasihi wananchi wa Gairo wasifanye makosa na wachague CCM iendelee kuleta maendeleo Gairo.

No comments:

Post a Comment