Msafara wa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo umeingia mkoani Morogoro wilaya na Jimbo la Kilombero.
Mheshimiwa Kikwete alianza Mkutano wake wa kampeni kwa kuelezea wananchi wa Kilombero kuwa hakuna Chama imara kama CCM na vyama vingine vyote vya CCM vina haki ya kuiga CCM kwasababu bado ni vyama vichanga na havina budi kuiga kutoka CCM.
"Lakini ndugu zangu kwa nini muhangaike na photocopy na wakati original ipo?" Aliuliza wananchi waliofurika kwa maelfu huku akishangiliwa kwa makofi na vigelegele.
Alisema kipindi hiki cha uchaguzi watanzania popote pale walipo wasikubali kuhubiriwa siasa za ubaguzi wa kidini, ukabila wala umwagaji damu kwa ajili ya tamaa za uongozi wa wanasiasa wachache ambao alisema "hawa siasa imewashinda"
akielezea utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005-2010, alisema anatambua matatizo yanayowakabili wananchi wa Mlimba, na hivyo aliomba Mwenyekiti wa Tarafa hii ya Mlimba kueleza kwa kifupi kero za eneo hili.
Maji ni mojawapo ya tatizo kubwa la Mlimba ikifuatiwa na tatizo la barabara haswa itokayo Kilombero hadi Mlimba. Mengine yaliyoelezewa na Mheshimiwa Kikwete ni la elimu ambapo kuna upungufu mkubwa wa walimu na maabara ya wanafunzi wa sayansi.
Mheshimiwa Kikwete alifafanua malengo ya CCM ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2010-2015 ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la maji kwa vijiji kumi vya wilaya ya kilombero ikiwemo Mlimba A na Mlimba B. Alisema mradi huu umeshaanza kutekelezwa na kwa sasa mkandarasi anaanza kazi ya kutandaza mabomba na kuweka miundombinu tayari kwa kazi kuanza.
Akielezea utatuzi wa tatizo la kituo cha afya ambapo aliwashauri wananchi wa Mlimba kufanya maamuzi kupitia halmashauri yao, ili kituo chao cha afya kipandishwe kuwa hospitali. Yeye aliahidi kuwasaidia kutafuta fedha pindi maamuzi hayo yakishapitishwa na wananchi wenyewe.
Mwishoni Mheshimiwa Kikwete aliwanadi wagombea udiwani na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kilombero Abduli Mteketa ambao wote waliomba wananchi wa Mlimba kupiga kura kwa mafiga matatu ili CCM ishinde kwa kishindo.
No comments:
Post a Comment