Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo ameeleza kuwa serikali ya CCM ikipewa tena ridhaa ya kuongoza miaka mitano ijayo itahakikisha tatizo la maji jijini Dar es salaam linakwisha.
Mheshimiwa Kikwete aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni Kata ya Kivule jimbo jipya la Ukonga jijini Dar es salaam ambapo maelfu ya wakazi wa maeneo hayo walijitokeza kwa wingi kumsikiliza.
Alisema tatizo la maji Dar es salaam limekuwa sugu kwasababu nyingi zikiwemo
- Uchache wa vyanzo vya maji ambavyo havitoshelezi mahitaji ya wakazi wa jiji
- Mtandao wa maji uliopo sasa ni wa zamani na hivyo unahitaji ukarabati wa mara kwa mara
- Maeneo mapya ya mji hakuna kabisa mtandao wa maji kutokana na ongezeko kubwa la watu Dar es salaam.
Aliongeza kuwa serikali ya CCM imeanza kushughulikia tatizo hilo ambapo utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa Kimbiji kuna maji mengi ya kutatua tatizo hilo. Baada ya uchimbaji wa visima kukamilika na mabomba kutandazwa, utafiti unaonyesha kuwa mita za ujazo 260,000 zitapatikana.
Mheshimiwa Kikwete pia alichukua muda mwingi kuelezea mafanikio yaliyopatikana miaka mitano iliyopita ikiwemo upanuzi mkubwa wa sekta ya elimu jimboni Ukonga. Alisema kuwa sasa hivi wanafunzi 42,120 wanaendelea na masomo ya sekondari ukilinganisha na miaka mitano iliyopita ambapo ni wanafunzi 10,000 tu waliokuwa wanaendelea na elimu ya sekondari.
Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea, aliongelea mafanikio hayo (jimbo jipya la Ukonga) na kusema kuwa kati ya shule 34 za kata zilizojengwa hivi karibuni, 22 zimejengwa jimbo la Ukonga.
Kwenye mkutano huo pia walinadiwa wagombea udiwani na ubunge wa Jimbo la Ukonga ambapo wananchi walisema bado wanaimani na CCM na wana imani na Mheshimiwa Kikwete hivyo wataipigia kura CCM na wagombea wake.
Kwenye mkutano huo pia walinadiwa wagombea udiwani na ubunge wa Jimbo la Ukonga ambapo wananchi walisema bado wanaimani na CCM na wana imani na Mheshimiwa Kikwete hivyo wataipigia kura CCM na wagombea wake.
No comments:
Post a Comment