10/22/2010

Mkutano wa Kampeni Malinyi: Kamanda wa UVCCM Njayaga Apiga Goti Kuombea CCM kura

Aliyekuwa mshindi wa pili kwenye kura za maoni za ndani ya Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Ulanga Magharibi Ndugu Yasin Njayaga na Kamanda wa UVCCM na mdau mkubwa wa CCM ameomba kura zote kwa CCM kwa staili ya kupiga magoti kwenye mkutano wa kampeni Malinyi.

Aliomba kura hizo wakati wa mkutano mkubwa wa kampeni wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa jimboni hapo leo mchana.

Wengine walioshiriki kwenye kinyang'anyiro hicho cha kura za maoni Ulanga Magharibi ni Dkt. Juma Ngasongwa, Eng. Simon Ngonyani na Dkt. Haji Mponda ambaye aliibuka mshindi, walisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu na kushikamana ili kukipatia Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo.

Kwenye hotuba yake ya kampeni hapa Malinyi, naye Mheshimiwa Kikwete alielezea azma ya CCM kutatua tatizo la upatikanaji wa huduma muhimu za maji, umeme na barabara katika eneo hili la Ulanga.

Alisema miradi imeshaanza ya kutandaza mabomba kwa ajili ya usambazaji wa maji kwa msaada wa Benki ya Dunia. Alizungumzia pia daraja la Mto Kilombero ambalo ujenzi wake utaanza hivi karibuni ambao utaruhusu pia barabara ya lami kujengwa.

Mwishoni Mhemiwa Kikwete alichukua nafasi ya mkutano huo kuwanadi wagombea udiwani wa kata zote za Ulanga, na mgombea Musa alizungumza kwa uchache kwa niaba ya wagombea wengine wote. Na baadaye mgombea ubunge nae aliwasihi wana Ulanga kuchagua CCM kwa mafiga matatu.


No comments:

Post a Comment