10/15/2010

Mkutano wa Kampeni Kibaha Mjini: JK Asema Trekta ndogo ni kwa wakulima wadogo

Shabiki wa CCM akishangilia hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea Urais Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete huko Kibaha leo mchana

Mashabiki wa CCM wakiimba na kucheza kwenye mkutano wa kampeni wa Mheshimiwa Kikwete leo mchana Kongowe Kibaha Mjini Mkoani Pwani.

Mheshimiwa Kikwete akihutubia umati mkubwa wa watu kwenye mkutano wa kampeni Kibaha Mkoani Pwani leo tarehe 15.10.2010


Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akisikiliza, huku daktari wake, Profesa Janabi, akichukua maelezo ya mzee Msiani Msisi (Kushoto) ambaye ana matatizo ya mguu wa Kushoto. Mzee Msisi anatumia mguu wa bandia aliopatiwa na mgombea huyo wa CCM. Hapa ilikuwa ni baada ya Kikwete kuhutubia mkutano wa klampeni huko Kibaha mkoani Pwani jana.
Na Joseph Mwendapole, Kisarawe.


MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete, ameonya viongozi wasijiuzie matrekta madogo ambayo yananunuliwa na serikali kwa ajili ya kuwauzia wakulima ikiwa ni jitihada za kuwaondoa kwenye kilimo cha jembe la mkono.

Vile vile, Kikwete alisema serikali itaendelea kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi hadi umauti utakapowakuta kwani huo ni mzigo wa serikali.

Aliyasema hayo wakati wa mikutano ya kampeni Kisarawe mjini na Wilaya ya Kibaha katika mfululizo wa mikutano yake ya kampeni ya kuwnaia kurudi Ikulu ka awamu ya pili.

Alisema viongozi wanapaswa kuhakikisha trekta hizo zinawafikia wakulima badala ya kujiuzia wenyewe kwa wenyewe.

“Tulisimamisha ununuzi wa magari ya serikali kwa miaka miwili mfululizo ma lengo ikiwa ni kununua trekta hizi kwa wakulima, hivyo zikija ziwafikie walengwa ambao ni wkaulima wadogo maana zinaweza kuja hapa ukasikia wakubwa kwa wakubwa wanauziana, sisi tunawalenga wakulima wadogo ili waondokane na kilimo cha jembe la mkono,” alisisitiza Kikwete.

Kuhusu vyama vya ushirika, Kikwete alisema aliamua kununua madeni ya vyama hivyo ili vikopesheke ila aliwaasa wananchi hao wasiwarejeshe madarakani watu waliovifilisi.

“Ndugu wananchi lengo la kubeba mzigo wa madeni lilikuwa zuri sana, tulitaka vyama vile vikopesheke na viendelee na kazi zake maana vile ndio mkombozi wa wakulima dhidi ya wanyonyaji sasa na nyinyi mkibebwa shikamaneni msiwarejeshe wale viongozi waliowafikisha hapo,” alisisitiza.

Alisema bila vyama hivyo wanunuzi wa mazao ya wakulima wamekuwa wakilalia wananchi katika mazao yao kama walivyokuwa wakinunua korosho ka wa sh 160 kwa kilo.

Alisema baada ya serikali kuingilia kati na kuweka bei elekezi ya sh 800 kwa kilo, sasa zao hilo limepanda bei hadi kufikia sh 1700 kwa kilo mkoani Mtwara.

Vile vile, Kikwete alisema serikali inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha kutengenezea dawa ya kuulia mazalia ya mbu wilayani Kibaha mkoa wa Pwani.

Alisema serikali inatumia fedha nyingi kutibu ugonjwa huo hivyo imeamua kwa dhati kuua mazalia ya mbu kwa kunyunyuzia dawa nyumba zote nchini.

Alisema kwa kuanza tayari nyumba za mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza imeshanynyuziwa dawa hizo na kwamba baada ya hapo zoezi hilo litaendelea hadi mikoa yote nchini.

Kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, alisema Mkoa wa Pwani unamaambukizi makubwa ya ugonjwa huo hivyo aliwataka wawe wanafuata mafundisho ya viongozi wa dini na wasiyapuuze.

Alisema watu 17,989 mkoani humo wanatumia ARV na theluthi moja ya watu hao wanatoka wilaya ya Kisarawe.

“Maambukizi ni makubwa na tusifanye mzaha, sikilizeni na kufuata ya viongozi wa dini ila mkishindwa kabisa mtusikilize sisi wahubiri wa dunia tunaowashauri mtumie kinga,” alisema.

No comments:

Post a Comment