10/27/2010

Mkutano wa Kampeni Kiwalani Jimbo la Ukonga (Segerea): Mahanga ajivunia shule za sekondari za kata


Wafuasi wa CCM, wakishangilia hotuba ya mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete, wakati alipohutubia mkutano wa kampeni huko Kiwalani nje kidogo ya jiji la Dar es salaam leo tarehe 27.10.2010.


Mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga (na sasa Segerea) Mheshimiwa Makongoro Mahanga amejivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye miaka mitano iliyopita ya upanuzi mkubwa wa elimu jimboni hapo.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010 imefanikisha ujenzi wa shule za sekondari 34 na kufanya jimbo hili kuongoza nchi nzima kwa ujenzi wa shule nyingi mpya nchi nzima.

Aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni Kiwalani wa mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambapo leo yuko kwenye Mkoa wa Dar es salaam kwa ajili ya kunadi sera za CCM na kuomba wananchi ridhaa ya uongozi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, kabla ya kumkaribisha Mheshimiwa Kikwete kutoa hotuba yake ya kampeni, alichukua nafasi hiyo kuwasihi wananchi wa Kiwalani kuchagua CCM na wagombea wake. Pia alimuahidi Mheshimiwa Kikwete kwamba CCM mkoa watajitahidi ili CCM ishinde kwa kishindo, majimbo yote nane ya Mkoa wa Dar es salaam.

Kwenye hotuba yake ya kampeni Mheshimiwa Kikwete alisema CCM ni waaminifu na wakiahidi wanatekeleza ahadi zao hivyo wachague CCM iendelee kuongoza.

Aliongeza kuwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2005 - 2010, elimu ilipewa kipaumbele na kupewa asilimia ishirini ya bajeti ya serikali. Lengo la serikali ya CCM kutenga bajeti hiyo kubwa ni kukabiliana na changamoto zilizopo ili bajeti hiyo ikidhi mahitaji yaliyopo.

Akielezea mpango wa uboreshaji wa huduma ya afya, Mheshimiwa Kikwete alieleza kuwa mwaka 2005 CCM iliahidi Watanzania, itasogeza huduma za afya karibu na wananchi walipo na lengo ni kuwa Mtanzania asisafiri zaidi ya kilometa tano kufuata huduma ya afya. 

"Ndipo CCM ilipoanzisha mpango wa kujenga zahanati kwenye kila kata, na kwa kipindi cha miaka mitano inayokuja 2010 - 2015, zahati hizo zitapandishwa hadhi kuwa vituo vya afya, na kwa miji kama Dar es salaam, vituo hivyo vitakuwa hospitali ndogondogo". Alisema Mheshimiwa Kikwete. 

Mheshimiwa Kikwete pia alizungumzia mpango wa upatikanaji wa huduma ya maji ambapo alisema jiji la Dar es salaam lina upungufu mkubwa wa maji kutokana na ongezeko la watu mijini.  

Kwa upande wa miundombinu ya barabara, Mheshimiwa Kikwete alisema jitihada mbalimbali zimefanyika ili kukabiliana na changamoto iliyopo mijini kuwa na magari mengi kwa kufanya upanuzi wa barabara kubwa. "Lakini mpango mkubwa uliopo sasa ni wa kujenga barabara za juu "fly-overs" ambazo zitasaidia sana kupanga mji na pia kupunguza tatizo hili sugu. 

Mheshimiwa Kikwete pia alielezea jitihada mbalimbali za serikali yake kuwainua wananchi kiuchumi ikiwemo mifuko ya fedha na uwezeshaji wa vijana kupata ajira. 

Mwishoni Mheshimiwa Kikwete alimnadi Dkt Makongoro Mahanga ambaye ni mgombea ubunge wa jimbo la Segerea na madiwani wa kata zote jimboni hapo.  

No comments:

Post a Comment