10/11/2010

Mkutano wa Kampeni Peramiho - JK: Hatuwezi Kutoa Huduma za Jamii Bure!


Jakaya Mrisho Kikwete akimnadi mgombea ubunge jimbo la Peramiho Jenister Mhagama wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata mpya ya Mtyangimbole, jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma jana mchana


Na Joseph Mwendapole, Peramiho
 
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali haina uwezo wa kutoa huduma za jamii bure na amewashangaa wanasiasa wanaopita wakiwadanganya wananchi kuwa iwapo wakichaguliwa watatoa huduma hizo bure.

Aliyasema hayo katika kata mpya ya Mchangimbore jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma katika siku yake ya pili ya kampeni katika mkoa huo.

Kikwete alisema serikali ilishajaribu sera hiyo ya huduma bure lakini ilishindwa kwani bidhaa ziliadimika na huduma nyingi zilishindwa kutolewa.

Alisema licha ya maendeleo yaliyofikiwa tangu Uhuru, Tanzania bado ni nchi maskini na haiwezi kutoa huduma bure kama baadhi ya watu wanavyowaahidi wananchi katika kampeni zao.

“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu sana hiyo sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo hayati baba wa Taifa, Julius Nyerere akiwa mwenyekiti wa chama, tulikaa naye tukaona hilo haiwezekani tukaamua tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure,” alisema Kikwete.

Alisema CCM inaahidi mambo yanayotekelezeka na kwamba imejitahidi kuhakikisha yale yote yaliyoahidiwa mwaka 2005 katika Ilani yake yametimizwa.

Alisema hivi karibuni alishangazwa na mwanasiasa mmoja aliyedai kuwa ana uwezo wa kuanzisha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Mwanza kwa masaa matatu, jambo ambalo Kikwete alisema haliwezekani.

“Ndege ya Rais yenyewe inatumia masaa mawili kwenda Mwanza sasa hiyo treni ya masaa matatu inawezekana kweli kama si uongo wa mchana huu, Baba wa Taifa aliwahi kusema ukiona mtu mzima anadanganya wenzake ujue ana matatizo mawili, ama ana tatizo kichwani mwake ama anawadharau wale anaowadanganya,” alisema Rais Kikwete.

Alisema msemo wake wa ari, nguvu na kasi mpya alipoingia madarakani mwaka 2005 haikuwa wa maneno matupu kwani umewasaidia kufikia malengo waliyojiwekea.

Alisema serikali iliahidi kujenga shule za sekondari kila kata na imefanikiwa kufanya hivyo na sasa kila kata ina shule mbili za sekondari, jambo ambalo awali lilionekana kama haliwezekani.

Alisema serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa kuboresha elimu ya msingi na sekondari na hivi sasa wanafunzi wengi wanapata nafasi ya kwenda shule tofauti na ilivyokuwa mwaka 2005.

Alisema shule zote hizo za kata nchini zitajengwa maabara za kisasa za sayansi kwa mkopo wa benki ya maendeleo ya Afrika ADB, ikiwa ni pamoja na kuwekewa vifaa vya kisasa kwa ajili ya mazoezi ya wanafunzi.

Kikwete alisema serikali yake itaipa kipaumbele elimu kwa kuongeza fedha za bajeti hiyo kila mwaka maana ndio msingi mkubwa wa maendeleo na ndio ufunguo wa maisha.

Kuhusu afya, mgombea huyo alisema serikali itaipandisha hadhi hospitali ya Peremiho kuwa ya rufaa na aliagiza mipango ianze kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya na serikali Kuu itasaidia.

“Anzeni sasa kutengeneza mipango na serikali kuu itawasaidia maana tunafanya mipango ile ya Peramiho iwe ya rufaa,” alisema

Alisema hospitali ya Peramiho itakarabatiwa na kupewa vifaa tiba, kuongeza idadi ya madaktari na wauguzi.

Kikwete pia alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Jenister Mhagama kuwa ni mchapakazi hodari na anaheshima ndani ya Bunge hivyo wananchi wanapaswa kumrejesha bungeni kwa njia ya kura tarehe 31 mwezi huu.

“Huyu anaheshimika sana ndani ya Bunge, Spika na Naibu Spika wasipokuwepo yeye anaendesha Bunge,” alisema.

1 comment:

  1. Thanks for updating us.

    Surely no Government can manage to offer free social services to ALL as there is actually no such a thing as 'free service'

    Only targeting the poor (those who can't pay) by pragmatic exemption strategies is the solution.

    wa- Chirangi

    ReplyDelete