10/11/2010

Mkutano wa Kampeni Mbamba Bay, Mbinga - JK awadhihaki wanaopinga ahadi ya unuuzi wa meli


Mheshimiwa Kikwete akihutubia mkutano wa kampeni Mbinga

Maelfu ya wakazi wa wilaya ya mbinga mkoani Ruvuma wakisikiliza hotuba ya mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, alipohutubia mkutano wa kampeni jana wilayani humo.

Mgombea Urais wa Tanzania Mheshimiwa Kikwete akihutubia mkutano wa kampeni Mbinga

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na Muasisi wa TANU Mzee Ntimbanjayo John Millinga,89, walipokutana mjini Mbinga mara baada ya kuhutubia mkutano mkubwa wa kampeni Mbinga.

Umati wa wananchi ukimshangilia Mheshimiwa Kikwete alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni Mbinga

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Kikwete akimtambulisha rasmi mgombea ubunge wa jimbo la Mbinga Mashariki ndugu Gaudence Kayombo wakati wa mkutano wa kampeni alioufanya mjini Mbinga terehe 11.10.2010.

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) amewadhihaki wanasiasa wa upinzani ambao wanapinga ahadi yake ya kununua meli mpya tatu kwa ajili ya usafiri wa abiria na mizigo katika maziwa matatu makuu ya Tanzania.

Lakini Rais Kikwete amesisitiza kuwa hata wapinge kiasi gani, bado Serikali yake ikirudishwa madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwisho wa mwezi huu, itanunua meli za usafiri katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

“Mimi naahidi kununua meli kwa ajili ya kupunguza shida ya usafiri ya wananchi, wao wananipinga kiasi cha kunifikisha kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” Rais amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni uliofanyikia Mbamba Bay, Jimbo la Mbinga Magharibi, Mkoa wa Ruvuma, mchana wa leo, Jumatatu, Oktoba 11, 2010.

Rais Kikwete ameongeza, “Wenyewe wanaahidi kununua treni ya kusafiri kwa saa tatu kati ya Dar Es Salaam na Mwanza, wala mimi sisemi kitu, lakini nikiahidi meli kwa ajili ya usafiri wa wananchi naambiwa nimevunja maadili ya Uchaguzi Mkuu.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Tofauti kati ya ahadi zangu na za kwao ni kwamba wanajua kuwa za kwao ni za uongo na hazitekelezeki na za kwangu ni za ukweli na zinatekelezeka.”

Mwanzoni mwa kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, chama cha CHADEMA kilimfikisha kwenye NEC Mgombea huyo wa CCM kikilalamika kuwa Rais Kikwete alikuwa amevunja maadili ya uchaguzi kwa kuahidi kununua meli ya kuchukua nafasi ya MV Bukoba iliyozama katika Ziwa Victoria miaka 16 iliyopita. Hata hivyo, Tume ilitupilia mbali malalamiko hayo.

Lakini leo, Rais Kikwete amewaambia wananchi wa Mbamba Bay: “ Napenda kurudia yale ambayo nimeyasema kule kanda ya Ziwa kuwa tutanunua meli tatu – moja, meli yenye uwezo wa kubeba tani 400 ambayo tutaiweka katika ziwa hili la Nyasa kuchukua meli iliyozama, ya pili, meli ya kuziba pengo la MV Bukoba iliyozama katika Ziwa Victoria na ya tatu itakuwa ni meli itakayochukua nafasi ya MV Liemba katika Ziwa Tanganyika.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Ile meli ya MV Liemba imechoka sana. Ni meli iliyoachwa na Wajerumani na mimi niliisoma katika vitabu vya historia nikiwa darasa la tatu.”

Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haiwezi kukatishwa tamaa na maneno ya wapinzani katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo.

No comments:

Post a Comment