Umati mkubwa wa wananchi wa mji wa Songea waliofurika katika uwanja wa Majimaji kwa ajili ya kusikiliza mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mgombea WA ccm Rais Jakaya Kikwete tarehe 10.10.2010. |
Mafiga Matatu |
Asema wanajaribu kutumia ngazi ya maiti za watu kuingia Ikulu
- Asisitiza kuwa damu ikianza kumwagika wao watakimbilia Ulaya
- Awashutumu ‘wanaochonga’ kuwa Tanzania haijapata maendeleo tangu uhuru
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) amewaonya Watanzania kuwakataa wanasiasa wanaohubiri umwagaji damu nchini kwa nia ya kutumia maiti za watu kama ngazi ya kwenda Ikulu.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa umwagaji damu ni jambo lenye maslahi tu kwa wanasiasa ambao damu itakapoanza kumwagika watapanda ndege kukimbilia zao Ulaya.
Vile vile, Rais Kikwete amewashutumu wanasiasa wanaotumia uongo katika kampeni za sasa za Uchaguzi Mkuu katika kupindisha mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa CCM akiwaita wanasiasa hao “watu wazima ovyo”.
Akihutubia mkutano mkubwa na uliochangamka wa kampeni kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea jioni ya leo, Jumapili, Oktoba 10, 2010, Rais Kikwete amewasuta ipasavyo wanasiasa ambao wamekuwa wanatishia umwagaji wa damu nchini kama hawakufanikiwa kushika nafasi za uongozi wanazozitaka.
“Sisi ni CCM. Sisi ni chama kisichohubiri umwagaji damu. Sisi ni chama cha amani. Umwagaji damu hauna maslahi yoyote na wala tija kwa yoyote isipokuwa kwa wanasiasa wanaotaka kutumia maiti za watu kama ngazi ya kuingilia Ikulu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hawa siyo watu. Hawana maana yoyote. Achaneni nao watu wa namna hii wanaotaka kupata madaraka kwa ngazi ya maiti za wananchi wasiokuwa na hatia.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Wanachochea watu wamwage damu na wao wapande ndege kwenda zao Ulaya na kuwaachia nyie mkitoana damu.”
Viongozi wa Chama cha CHADEMA, na hasa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wamekuwa wakihubiri umwagaji damu nchini endapo chama hicho kitashindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kuhusu madai ya uongo ambayo yamekuwa yanasambazwa na wanasiasa kuwa hakuna maendeleo yoyote ya maana yaliyopatikana Tanzania tokea uhuru mwaka 1961, Rais Kikwete amewaambia maelfu ya wananchi hao kwenye Uwanja wa Majimaji:
“Wanapitapita.. wakichonga sana kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana tokea uhuru wetu. Kwa nini watu wanakuwa waongo kiasi hiki…watu wazima ovyo”
Amesema kuwa ukweli utabakia pale pale hata kama wengine hawataki kuukubali kuwa CCM imeongoza Tanzania vizuri na chama hicho kimekuwa mbegu iliyozaa vyama vingine vyote vya siasa nchini. “Hiki ni chama imara, chama dume, dume la mbegu. Mbegu yetu ndiyo imezaa CHADEMA, ndiyo iliyozaa CUF na vingine vyote.”Rais Kikwete amewaelezea wana-Songea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita ya uongozi wake.
Aidha, Rais Kikwete ametangaza kuwa Serikali itajenga Chuo Kikuu cha Madaktari mjini Songea kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba.
No comments:
Post a Comment