10/03/2010

Mkutano wa Kampeni Puma na Ikungi - Khambaku apasua jipu yaliyomkuta Chadema



Khambaku akiongea kwa hisia kwenye mkutano wa kampeni Ikungi kuhusu siku 29 alizokaa Chadema baada ya kuanguka kwenye mchakato wa CCM.

Wasanii Bushoke, Ray C na Flora Mbasha wakitumbuiza wananchi kwenye mkutano wa kampeni Ikungi leo tarehe 3.10.2010

- Alikaa Chadema siku 29
- Atoa siri, Chadema hakuna sera
- Wapinzani zaidi ya 50 warudi CCM
- Wasanii watoa buradani ya kishindo

Aliyeshindwa kura za maoni jimbo la Singida Magharibi na kuhamia Chadema kwa siku 29, Bwana Wilson Elisha Nkhambaku, ameeleza kilichomsibu akiwa kwenye chama hicho pinzani.

Akitoa ushuhuda kwenye mikutano ya kampeni Puma na Ikungi, Khambaku alikiri kughafilika na kukimbilia upinzani baada ya kuanguka kwenye kura za maoni.



Akishangiliwa na umati wa watu pale aliposema kwamba aliomba sera za Chadema kwa wiki moja bila mafanikio na hatimaye kushindwa kupata muelekeo wa chama hicho kwa ajili ya kampeni.



Alisema chama hicho ni matapeli kwani baada ya kumzungusha wiki mbili walimpa sera za matusi na kubeza mafanikio thabiti ya CCM.



Akiongelea mafanikio ya CCM kwenye upanuzi wa elimu ambapo hata Umoja wa Mataifa umetambua na kuipa Tanzania tuzo ya kukidhi malengo ya milenia kwenye upande wa elimu kwa asilimia 95.



Akizungumza kwa hisia kubwa, Khambaku alisema siku 29 alizokaa Chadema zilikuwa za mateso na upweke mkubwa, akizifananisha na nyumba yenye kunguni na chawa ambazo humuwasha mtu anayelala kwenye malazi yake.



Amesema sababu kubwa zilizomfanya yeye kurudi CCM ni amani na utulivu iliyodumishwa na CCM tangu uhuru hadi leo. Amewasihi wananchi wa Singida wasifanye makosa ya kuchagua upinzani, ni wasanii, wana chuki na wanabeza hata mafanikio halali ya CCM.



"Mwisho nawasihi msifanye makosa niliyofanya mimi, msihangaike na wapinzani. Hawana sera hao, nimejionea mwenyewe! Naomba mchague chama madhubuti, CCM"



Alimaliza Khambaku huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu.



Na kwenye mkutano wa kampeni wa Ikungi, wapinzani zaidi ya 50 kutoka Chadema na CUF walirudisha kadi zao na kuingia CCM.



Aliyehama kutoka Chadema, alitoa ushuhuda kwa kusema alipochukua kadi ya Chadema aliambiwa kwamba yeye ni mwenyekiti.



"Nikawauliza mwenyekiti wa nini, wakasema wa kijiji hiki. Nikawahoji nani kanichagua? na ninamuongoza nani? Sikupewa jibu, sasa narudi CCM" Alisema Mzee huyo akishangiliwa na umati wa watu.



Nao wasanii wa muziki hawakuwa nyuma kwenye kutoa hamasa kwenye mkutano huo. Mwanamuziki Flora Mbasha akisindikizwa na wanamuziki wengine mashuhuri Ray C na Bushoke walitoa hamasa kubwa kwa wananchi wa Ikungi waliohudhuria kwa wingi mkutano huo wa kampeni.



Naye mshairi maarufu kutokea hapa Singida alitumbuiza kwa shairi lake lililomshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kuleta wilaya mpya ili kusogeza shughuli za maendeleo karibu na wananchi.



Mshairi huyo alisifia umahiri wa Chama Cha Mapinduzi haswa kuwatayarisha viongozi wa nchi na utawala mzima wa chama. Alisema kutoka umoja wa vijana kuna jumuiya ya wazazi na wanawake ambazo zote zinalenga kuwalea wana CCM kuongoza chama na nchi. Alihoji wapinzani wanapikwa namna hiyo hadi kutaka kugombea uongozi wa juu wa nchi?



Akishangiliwa na umati wa watu, mshairi huyo alisihi pia kudumisha amani na mshikamano haswa kipindi cha uchaguzi. Aliwasihi wana Singida kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili mkoa uongoze kwenye kura nyingi kwa wagombea wote wa CCM.



Kabla ya Mkutano wa Ikungi - Singida Mashariki, Mheshimiwa Kikwete alifanya mkutano wa kampeni Puma Singida Magharibi ambapo mgombea ubunge wa jimbo hilo Mohamed Missanga alimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kuwapatia wilaya mpya na jimbo jipya la uchaguzi.



Baada ya hapa, msafara wa Mheshimiwa Kikwete utaelekea Itigi, Manyoni, Kitinku na hatimaye Dodoma Mjini kwa mkutano wa mwisho wa kampeni kwa siku ya leo.

No comments:

Post a Comment