10/03/2010

Mkutano wa Kampeni Dodoma - "Nina Kila sababu ya kurudi Ikulu, Nichagueni" JK

Na Joseph Mwendapole, Dodoma

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete, amesema ana kila sababu ya kurudi Ikulu kwa awamu ya pili kwani amewafanyia mengi watanzania na katika miaka mingine mitano ijayo amedhamiria kuwafanyia mambo makubwa ambayo yanaonekana kama hayawezekani.

Aliyasema hayo katika mikutano mbalimbali ya kujinadi mkoani Dodoma ambapo alifanya kampeni katika majimbo ya Mtera, Chilonwa, Bahi na Kongwa akiwa katika harakati zake za kuomba kura kurejea Ikulu kwa mara nyingine.

Kikwete alisema katika Ilani ya mwaka huu kumejaa mambo mengi mazuri hivyo watanzania wasiwe na wasiwasi kwani wakimchagua yeye watarajie mambo mazuri mengi kwa miaka mitano ijayo.

“Ilani ya mwaka 2005 si mnaiona ilivyo ndogo lakini tumefanya mambo mengi kwa kutumia Ilani hii na sasa oneni hii ya mwaka huu ilivyo bonge, hii imejaa mambo mengi mazuri ambayo tunakusudia kuwafanyia, vyama vingine havina kitu kama hiki wao wakija hapa wanapiga porojo wanaondoka tu, ndugu zangu tumefanya mengi kwa miaka mitano iliyopita na tutafanya mengi zaidi miaka mitano ijayo mkituchagua” alisema Kikwete.

Kikwete alisema ana sababu nyingi za kuwaomba watanzania wamrudishe Ikulu kwani chini ya uongozi wake mambo mengi yamefanyika kama ujenzi wa barabara, zahanati, hospitali, uchumi kuimarika licha ya msukosuko wa dunia na kupambana na maradhi ya Ukimwi na Malaria.

Aliwataka wananchi wasikubali kuhadaiwa na maneno ya wapinzani kuwa serikali ya CCM haijafanya lolote tangu Uhuru na kwamba wanapokuja kusema hayo wananchi wawahoji maendeleo yanayoonekana yameletwa na nani.

“Maendeleo yanaonekana ila hawa wenzetu wana mtima nyongo tu, wakija hapa wakasema uongo wao msiwaache hivi hivi wakaondoka tu lazima muwahoji hizo barabara nzuri wanazopita, hospitali na huduma zote wanazofaidi zimeletwa na nani kama sio CCM, waambieni ukiona vyaelea vimeundwa na muundaji ni CCM “ alisema Kikwete

Aidha, alisema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali nchini pamoja na huduma za afya ili wananchi wengi waweze kupata huduma hizo karibu na maeneo yao na kwa urahisi kama ambavyo imeweza kufanya katika awamu ya kwanza ya miaka mitano.

Alisema wakati akijinadi kwa wapiga kura mwaka 2005 kuomba ridhaa ya kuingia Ikulu aliahidi kuendeleza kudumisha amani na utulivu na kwamba akichaguliwa kwa mara nyingine tena nchi itatulia zaidi ya ilivyo sasa.

“Niliahidi amani, hebu tuulizane amani ipo haipo, “ alihoji na wananchi kuitikia kuwa ipo.

Kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, Kikwete alisema serikali imeendelea kutoa bure dawa za kurefusha maisha ARVs kwa wagonjwa nchini ila aliwashauri watu waache ngono isiyo salama.

Alisema watu wengi wanapata Ukimwi kwa kujitakia kwani wanafanya hivyo kwa starehe zao na kwa viherehere na ni matokeo ya kutosikiliza mafundisho ya viongozi wa dini.

Alisema walioko kwenye ndoa wanapaswa kuheshimu ndoa zao na ambao hawajaolewa wanapaswa kusubiri hadi wakati wao utakapofika lakini suala la kusubiri limeonekana kuwa ni tatizo kubwa kwa watanzania wengi.

“Mkizingatia mafundisho ya viongozi wa dini hampati Ukimwi maana wanakataza zinaa, ila mkishindwa kuwasikiliza wao tusikilizeni sisi wahubiri wa dunia, mkienda kufanya lile tendo mkumbuke kutumia kinga na imethibitishwa na wataalamu kuwa mkitumia kinga hamtapata Ukimwi,” alisema.

No comments:

Post a Comment