Mgombea ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mheshimiwa Lazaro Nyalandu amemmwagia sifa Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa kuleta neema kubwa Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Nyalandu aliyasema hayo wakati akisoma kwa kifupi mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2005 - 2010 kwa kuorodhesha mafanikio hayo.
Elimu: Shule za sekondari 9 mwaka 2005 na 28 mwaka 2010. Madarasa ya shule ya awali 89 mwaka 2010 na shule za msingi 88 2010. Walimu 886 wa shule za msingi. Shule za kidato cha tano na sita sasa ziko mbili ambapo 2005 kulikuwa hakuna shule hizo.
Mheshimiwa Nyalandu pia aliongelea jitihada kabambe zilizowekwa na CCM ili kuhakikisha wananchi wa Singida Kaskazini wanapata maji ya kutosha. Alisema visima virefu sasa viko 101 na visima vifupi viko 155.
Kwa upande wa barabara, Mheshimiwa Nyalandu alisema mwaka 2005 kulikuwa na kilometa kumi tu za lami zilizopita katika jimbo hilo. Lakini sasa kuna zaidi ya kilometa 30 za lami zinazopita Singina Kaskazini. "Si hivyo tu, bali sasa Mkoa wa Singida umeunganishwa kwa lami na Mikoa ya Arusha, Dodoma na kilometa kama kumi hivi zitakamilika miezi michache ijayo" alisema mgombea huyo.
Katika upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, Mheshimiwa Nyalandu alisema malambo na mabwawa makubwa yameongezwa na hivyo hata idadi ya mifugo imeongezeka kutokana na neema hiyo.
"Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM taifa, jisikie uko nyumbani kwani uko Singida Kaskazini. Kina mama hawa, vijana hawa, wazee hawa na wananchi wote wa hapa ni wana CCM, kura asilimia zote zitapatikana hapa, Ilongero Oyyeee!" Alisema Mheshimiwa Nyalandu kwa kutamba.
Naye mgeni rasmi, Mgombea Urais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alisema kwenye hotuba yake kwa wananchi hao kuwa wamefanya jitihada kubwa haswa kwenye utelezaji wa ahadi za CCM 2005.
Alihoji kwenye shule za kata kama ni kweli zilijengwa kama ahadi ilivyowekwa mwaka 2005. "Kuna watu walisema sekondari kila kata haiwezekani na hivyo kuiita ile ni ahadi hewa" Alisema Mheshimiwa Kikwete huku umati mkubwa wa watu ukikiri kuwepo kwa sekondari hizo za kata.
Aliwasifu wananchi wa Singida Kaskazinikuwa kwenye upande wa afya, zahanati zao zote zina umeme wa mwanga wa jua. Alisema hiyo ni jitihada kubwa na kwa upande wake na serikali, wataendelea kusaidia pale watakapoweza.
Pia Mheshimiwa Kikwete alielezea upande wa afya kuhusu jitihada za muda mrefu za kupambana na magonjwa sugu kama kansa ya shingo ya kizazi kwa wakina mama ambapo alieleza chanjo itaanza kutolewa mwaka ujao.
Kwa upande wa malaria alisema mpango wa kugawa vyandarua viwili kwa kila kaya utaanza hivi karibuni. Na mwisho kwenye vita dhidi ya UKIMWI, Mheshimiwa Kikwete alisema ni jitihada ya watanzania wote kukataa kupata UKIMWI, hiyo ndio kinga pekee.
Kabla ya kufanya mkutano huo mkubwa wa Ilongero, msafara wa Mheshimiwa Kikwete ulifanya mikutano Mdida na Mtinku Singida Kaskazini na hatimaye Ilongero.
Kutoka hapa Mheshimiwa Kikwete ataelekea Singida Mjini kwa mkutano mkubwa wa kampeni.
No comments:
Post a Comment