10/25/2010

Mkutano wa Kampeni Sumve na Ngudu Wilayani Kwimba, Mwanza


Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akipokea bendera ya CHADEMA, kutoka kwa mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho jimbo la Kwimba, Monika Jimotoli mara baada ya kutangaza kukihama chama hicho kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jimboni humo. Monika amehama chama hicho na wenzake 18.


Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akisalimia wananchi wakati akiwasili kuhutubia mkutano wa kampeni tarafa ya Nyamatala jimbo la Sunve wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

- Mwenyekiti wa Chadema Kwimba atinga CCM na wengine 18: Asema CHADEMA Kwimba imekufa!- Kikwete aainisha malengo ya CCM kwa miaka mitano ijayo


- Awasihi wana Kwimba kuchagua tena CCM

Mheshimiwa Kikwete amewasihi wananchi wa Sumve leo kuchagua CCM kwani hakuna Chama kama CCM kwa ubora wa sera, utekelezaji wa sera na mipango na jitihada za kuleta maendeleo kwa watanzania.

Japo Tanzania bado ni nchi maskini, alieleza Tanzania ya mwaka 1961 na ya sasa sio sawa. “Lakini cha msingi ni kwamba yale tuliyoyaahidi tutayafanya, tumeyatekeleza” alieleza Mgombea Urais wa CCM, Mheshimiwa Kikwete kwenye mkutano huo wa kampeni.

Kwa upande wa elimu, Mheshimiwa Kikwete alisema serikali ya CCM imekabiliana na changamoto kuu nne zilizojitokeza baada ya upanuzi mkubwa wa elimu nchi nzima.

Changamoto zilizopatiwa ufumbuzi ni ile ya upungufu wa walimu ambapo kila kata kuanzia mwakani itapata walimu wa tano. Changamoto ya nyumba za walimu zitajengwa za kutosha kwa sababu bajeti ya elimu imeongezwa mara tatu zaidi kukabiliana na tatizo hilo. Na tatu ni changamoto ya vitabu vya sekondari ambapo Mheshimiwa Kikwete alieleza mipango imefanywa kushirikiana na Serikali ya Marekani ambapo wamesaidia kuchapisha vitabu vya sayansi vya sekondari. “Kwa hivyo kuanzia mwakani, watoto wetu wa masomo ya sayansi watakuwa na vitabu vya kutosha kwenye shule zote nchi nzima” alieleza Mheshimiwa Kikwete.

Kwa upande wa huduma ya afya, Mheshimiwa Kikwete alieleza mikakati ya serikali ya CCM kupambana na maradhi makubwa kama Malaria, UKIMWI na kansa ya shingo ya kizazi kwa wanawake. Kwa kansa ya shingo ya uzazi, Mheshimiwa Kikwete alieleza kwamba kuanzia mwakani wanawake wote wenye umri wa kupata chanjo hiyo watachanjwa bure ili kukabiliana na gonjwa hilo sugu nchini.

Kwenye mikutano hiyo miwili pia Mheshimiwa Kikwete alieleza kuwa CCM iliahidi kuboresha utoaji huduma ya maji ili kufikia asilimia 60 vijijini na asilimia 90 mijini. Mheshimiwa Kikwete alieleza kwenye wilaya ya Kwimba, utoaji huduma ya maji kwa sasa umefikia asilimia 55.5, na bado jitihada madhubuti zinaendelea kuboresha hali hiyo.

Mheshimiwa Kikwete alieleza kuwa kwa msaada wa marafiki wa Tanzania wa maendeleo, vijiji kumi na mbili vya wilaya ya Kwimbavitapatiwa huduma ya maji kwenye mpango mkubwa wa usambazaji wa maji nchini unaodhaminiwa na benki ya dunia.

Kwa upande wa kilimo, Mheshimiwa Kikwete alielezea mpango mkubwa wa kilimo kwanza ambao unalenga kwenye kuboresha mambo makuu manane ambapo yatamsaidia mkulima kupata faida kwa kilimo chenye tija ikiwemo upatikanaji wa ruzuku na utafutaji masoko kwa ajili ya mazao ya wakulima.  

Mhehsimiwa Kikwete alieleza wakazi wa wilaya hii pia kwamba ilani ya CCM kwa mwaka 2010 – 2015 inaelekeza kipaumbele kwenye uvuvi wa samaki na kuendeleza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya wakulima.

Na kwenye mkutano wa kampeni huko Ngudu, aliyekuwa Mwenyekiti wa wanawake Chadema Wilayani Kwimba Mama Monica Jimotolo, amerudisha kadi ya chama hicho na kuingia rasmi CCM.

Mama Jimotolo alieleza sababu kuu iliyomfanya kuingia CCM ni kuchoshwa kwake na siasa za chuki na uchochezi ambazo zinalenga kuvunja amani na mshikamano wa nchi yetu.

Alieleza hadhara hiyo kuwa baada ya kufanya uamuzi huo, wengine kumi na saba wameongozana naye na kusema chama hicho kimekufa wilayani hapo. Wanachama hao walikaribishwa na Mwenyekiti wa CCM taifa na kupewa kadi za Chama Cha Mapinduzi.  

Mheshimiwa Kikwete aliwanadi wagombea udiwani na ubunge wa Chama Cha Mapinduzi. Aliwasihi wananchi wa Kwimba kupanga jozi iliyokamilika ya CCM ili kuleta maendeleo. Alitoa mfano wa kilimo cha punda na ng’ombe kwa kueleza kuwa unapoamua kulima utumie jozi ya punda au ya ng’ombe, lakini huwezi kuchanganya kwa kulima na ng’ombe na punda kwani punda atakapopiga mluzi, ng’ombe atasimama.

No comments:

Post a Comment