10/15/2010

Mkutano wa Kampeni Kisarawe- JK: Tumejipanga kuokoa wakina mama na Kansa ya Shingo ya uzazi

Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akisalimiana na wananchi wakati akiwasili kuhutubia mkutano wa kampeni huko Kisarawe mkoani Pwani jana asubuhi Oktoba 15, 2010.

Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, akiwa amembeba mtoto Viazi Hassan mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, wakati akiwasili kuhutubia mkutano wa kampeni huko Kisarawe mkoani Pwani jana asubuhi Oktoba 15, 2010.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema chanjo kwa kina mama kuzuia kansa ya shingo ya uzazi itaanza kutolewa nchini hivi karibuni.

Mheshimiwa Kikwete ameyasema hayo leo kwenye mkutano wa kampeni Kisarawe ambapo alikuwa ananadi sera za CCM na jitihada madhubuti za kupambana na maradhi makubwa yanayowasumbua Watanzania wengi. 

Kansa ya shingo ya uzazi ndiyo inayoongoza kwa kuua wakina mama wengi zaidi, ikifuatiwa na kansa ya koo na kansa ya matiti.

Mheshimiwa Kikwete alielezea jitihada za chama chake za kupambana na gonjwa hilo na kusema jitihada zimeshaanza ili kuhakikisha chanjo inapatikana.

"Tumeshajipanga sawasawa na kuanzia mwakani tutahakikisha wakina mama wote wenye umri unaostahili wanapatiwa chanjo ili kuwanusuru na kansa hiyo hatari". alisema Mheshimiwa Kikwete huku akishangiliwa na umati wa watu uliofika kwenye mkutano huo wa kampeni.

Mheshimiwa Kikwete pia alielezea jitihada mbalimbali za serikali yake inayoongozwa na CCM kutokomeza Malaria, ambapo alisema ifikapo mwaka 2015 angependa kuona Tanzania inatangaza duniani kwamba ni nchi ambayo haina malaria.

Pamoja na kuzungumzia mafanikio ya sera za CCM kwa miaka mitano iliyopita, Mheshimiwa Kikwete pia aliwanadi madiwani na mgombea ubunge wa Jimbo la Kisarawe Bwana Suleiman Said Jafo ambaye wananchi wa Kisarawe wanamuita Obama.

No comments:

Post a Comment