Mkutano wa kampeni Kiomboi leo jioni. |
Mheshimiwa Kikwete akiwasili Kiomboi kwa ajili ya mkutano wa kampeni. Mkutano huu utakuwa wa mwisho kwa siku ya leo na kesho anatarajiwa kuwa na mikutano Singida vijijini na Singinda Mjini. |
Na Joseph Mwendapole, Singida
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, amesema Rais wa Marekani, Barack Obama , ameahidi kuipa kipaumbele Tanzania katika kuimwagia misaada kuliko nchi zingine za Afrika.
Vile vile, amesema anajisikia fahari kubwa kuwa Rais wa kwanza wa bara la Afrika kukutana na Rais huyo wa Marekani.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa Iramba Magharibi mkoani Singida katika mkutano wa kampeni.
Kikwete alisema obama alitoa ahadi hiyo hivi karibuni katika mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Kikwete alisema kutokana na utendaji mzuri wa serikali yake, Rais Obama alimpa nafasi ya pekee ya kuwa Rais wa kwanza wa afrika kukutana naye ambapo walizungumza mambo mbalimbali.
Alisema hiyo imetokana na utendaji mzuri wa serikali yake katika kuwakwamua wananchi katika matatizo mbalimbali na kuwasogezea karibu huduma za jamii.
“Obama alianza kukutana namimi na alinieleza sababu za kuanza kukutana na mimi na si viongozi wengine wa bara la Afrika, juzi juzi tena akiwa UN aliahidi kuwa Tanzania itapewa kipaumbele kwa kupata misaada ya Marekani, ndiyo maana nawaambia sisi tunaaminika na tukiahidi tunatekeleza nawaomba muichague CCM iendelee kuwaletea maendeleo,” alisema Kikwete.
Alisema ingawa Tanzania bado ni maskini lakini maendeleo yaliyopatikana tangu uhuru hayapaswi kubezwa kwani maendeleo makubwa yamepatikana katika Nyanja za barabara, elimu, afya na miundombinu.
Kuhusu elimu, Kikwete alisema serikali iliahidi katika Ilani ya mwaka 2005 kujenga shule za sekondari kila kata na imefanikiwa kutekeleza ahadi hiyo hivyo aliomba achaguliwe kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Alisema upungufu wa walimu umetafutiwa majibu kwani vyuo vingi vikuu hivi sasa vimeanzisha vitivo vya kufundisha walimu na kwamba baada ya miaka mitatu tatizo hilo litabaki kuwa historia.
Alisema walimu wote watakaokuwa wakimaliza vyuo vya ualimu watakuwa wakichukuliwa na serikali na kugawanywa katika shule zote za sekondari hapa nchini.
Alisema bajeti ya elimu imeongezwa kutoka bilioni 669 hadi trilioni 2.45 na kwamba bajeti hiyo ndiyo kubwa kuliko bajeti zote kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2010/2011.
Kuhusu vitabu, Kikwete alisema amewaagiza maprofesa wa Tanzania waandike vitabu na wamarekani wamehidi kusaidia uchapishaji hivyo tatizo la vitabu litaisha kuanzia mwakani kwani kila mwanafunzi atakuwa na kitabu chake.
Alisema benki ya maendeleo ya Afrika ADB imeahidi kuikopesha serikali ya Tanzania dola za Marekani milioni 90 ambazo zitatumika kujenga maabara katika shule za sekondari na kukarabati maabara za zamani.
Kuhusu hospitali ya Wilaya ya Kiomboi mkoani Singida, kikwete alisema serikali itaendelea kuiboresha hadi ifikie viwango vya kimataifa na itakarabati zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment