10/07/2010

JK asheherekea miaka 60 ya kuzaliwa









Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo amesheherekea miaka 60 ya kuzaliwa kwa tafrija ya aina yake.

Ikiwa ni siku ya mapumziko kwenye ratiba ya kampeni zake, familia ya Mheshimiwa Kikwete kushirikiana na Clouds Media Entertainment waliandaa tafrija fupi ambapo Mheshimiwa Kikwete alipata fursa ya kusheherekea siku hiyo siyo tu na wanafamilia na viongozi wa nchi, bali aliburudishwa na bendi aliyokuwa anaipenda sana Sikinde Ngoma ya Ukae.

Mojawapo ya burudani iliyotawala sherehe hiyo ni pale Mheshimiwa Kikwete alipokuwa anajibu maswali yaliyokuwa yanaulizwa na mtangazaji machachari wa Clouds FM wa kipindi cha Power Breakfast Bwana Gerald Hando aliyesaidiana na mshereheshaji wa siku Ephraim Kibonde kama ifuatavyo: 

Swali: Ni chakula gani ambacho unakipenda sana
Jibu: Bambiko, chakula cha asili kutoka nyumbani Musoga.

Swali: Ulipokuwa kijana unasoma, ulikuwa unafikiria ungependa kuwa nani?
Jibu: Nilipokuwa mdogo tulikuwa tunaangalia pale kijijini nani alikuwa anaheshimika sana. Na vijana wote walitaka wakiwa wakubwa wawe kama huyo. Sasa kulikuwa na Karani ambaye alikuwa smart sana na anavaa shati na peni mfukoni. Hivyo nilipenda sana kuwa karani.

Swali: Kati ya watoto wako, ni mtoto yupi uliyefanana naye sana na amechukua tabia zako?
Jibu: (vicheko na makofi) Watoto wangu wote nawapenda sana, na wote nimefanana nao sana. Lakini kuna kitu kimoja ambacho nadhani wote wamenifanana, ni mapenzi yangu kwenye muziki. Na mimi nadhani nimerithi kutoka kwa baba yangu.

Swali: Ulikutana vipi na Mama Salma hadi mkaoana?
Jibu:(vicheko, makofi) Tulikutana Nachingwea, wakati nikiwa Mkuu wa Wilaya pale Nachingwea yeye alikuwa anasomea ualimu pale chuoni. (Ulikutana naye vipi?) Barabarani, alikuwa akitokea chuoni na nilipomsalimia aliniponda. (vicheko na makofi)  Lakini nikasisitiza (vicheko, makofi) eeh ndio, unang'ang'ania tu, unarudiam, unarudia, unarudia hadi akaanza kunisalimia na kunisemesha. (Makofi) Nikamwambia mojakwamoja, nataka kumuoa na nitatuma mshenga kwao. Alifikiri natania. Lakini baada ya muda nilituma mshenga na tukasubiri majibu na taratibu nyingine zikafuata. (makofi)

Swali: Je ulipokuwa jeshini, ni kosa gani kubwa ulilolifanya na ulipewa adhabu gani?
Jibu: (vicheko) Nilipokuwa jeshini nilikuwa msafi sana, hivyo mara kwa mara wenzangu walikuwa wakiitwa na kupewa adhabu na kuambiwa wafuate mfano wangu. Hivyo kwa kuwa nilikuwa natolewa mfano mara kwa mara, nilijitahidi sana kuwa na tabia ya kutokufanya makosa na hivyo kuepuka adhabu. Ila kuna zile adhabu za jumla zile, zile za ma-group, kombania nzima mnaweza kuambiwa leo mmeharibu ruka kichurachura. Hizo nilizipata, lakini mimi mwenyewe binafsi, labda nilipokuwa shule ya msingi. Kuna siku nilichapwa, tena yule mwalimu wangu yule aliyenichapa bado yupo, yupo Matombo pale Morogoro. Siku hiyo nilikuwa zamu kulinda kuku wa shule, na nyoka akaingia bandani na kumuua kuku mmoja. Basi nilichapwa viboko sana, japo naona kama vile yule mwalimu alinionea vile (alicheka na wageni wote walicheka). Hiyo ndio adhabu ambayo naikumbuka.

Swali:Ni comedians gani ama wachekeshaji watatu wanaokuvunja mbavu
Jibu:Ze Komedi ( Origino Komedi?) Ndiyo, kina Joti. Hawa nikiwaangalia huwa na cheka sana. Mwingine tulikuwa tunasoma naye nikiwa sekondari sasa ni marehemu, naye alikuwa mcheshi saaana. Hapo zamani alikuwa akituchekesha mno. (na mwingine wa tatu?) aaah wapo wengi kwa kweli ila sasa siwakumbuki, na Bambo pia ananichekesha sana. 

Kwa niaba ya familia, mtoto wa Mheshimiwa Kikwete Dr. Salama alimpongeza baba yake kwa kufikisha miaka 60 na alitoa salamu za upendo kumtakia kila la kheri na kushukuru kwa malezi mazuri anayoendelea kuwapa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Clouds Media Bwana Joseph Kusaga, alisoma risala fupi ya kumpongeza Mheshimiwa Kikwete na kueleza wageni waalikwa chimbuko la wana Clouds kuandaa sherehe hizo za siku ya kuzaliwa.

Alisema mwaka jana siku kama ya leo kwenye kipindi cha Power Breakfast, Mheshimiwa Kikwete alifanya mahojiano na watangazaji hao na walimuuliza kama wana Clouds wangeweza kupewa nafasi ya kumuandalia sherehe ndogo kwenye sherehe yake ijayo. "Naye alikubali, na kwa sasa napenda kuwaambia yule mtangazaji aliyeuliza hilo swali tumempandisha cheo" alimaliza Kusaga huku akishangiliwa na wageni wote na wale wa Clouds.

Akitoa shukrani zake, Mheshimiwa Kikwete alisema amefurahishwa sana na jitihada za familia yake na Clouds ya kuandaa sherehe hiyo. Alikiri kuwa yeye siku zote huwa hakumbuki siku yake ya kuzaliwa, na kwa kufikisha miaka 60 amefurahi sana kupongezwa kwa aina hiyo.

Alieleza kuwa ameshangazwa sana kuona kuwa licha ya kualikwa ndugu na jamaa wa karibu, waandaaji hao wameweza kuleta kikundi maarufu cha ngoma kutoka Msoga, na bendi yake aliyokuwa akiipenda sana ya Sikinde.

Akizungumzia jitihada za vijana nchini kujikwamua kiuchumi, Mheshimiwa Kikwete alisema Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba na mifano ya kuigwa na anashukuru kwa mchango wao kwa jamii katika kuendeleza nguvu kazi ya vijana kwa kupitia burudani na muziki.

3 comments:

  1. Hongera JK, NAKUTAKIA kila la kheri, Mungu akutie nguvu kuongoza Tanzania kwa kipindi kingine.

    ReplyDelete
  2. HAPPY BIRTHDAY JK TUNAKUTAKIA AFYA NJEMA NA MAISHA MAREFU NA MAFANIKIO ZAIDI KWA TAIFA LETU.

    ReplyDelete
  3. Ni furaha kuona kuwa umefikisha miaka 60. Mola Akujalie uwe na maisha marefu. Tunategemea mengi mema zaidi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Endelea kupambana na ufisadi kwa nguvu zako zote. Mungu Aendelee kuibariki nchi yetu!

    ReplyDelete