9/15/2010

JK aiteka Manispaa ya Moshi, apokelewa kwa kishindo

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mgombea urais kupitia tiketi ya CCM akiingia kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi tayari kuanza mkutano wa kampeni.

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwapungia maelfu ya wakazi wa mji wa Moshi wakati alipokuwa akiingia katika uwanja wa Mashujaa mjini Moshi na kuhutubia katika mkutano mkubwa wa Kampeni
Mheshimiwa Kikwete akihutubia maelfu ya wananchi waliojitongeza kumsikiliza alipokuwa anahutubia mkutano wa kampeni mjini Moshi.






Na Mgaya Kingoba, Moshi

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete amepata mapokezi makubwa kwenye mji wa Moshi Mjini, ambao kwa miaka 15 umekuwa ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na akakiri kuhemewa na ‘kutapika’ kwa uwanja aliofanyia mkutano.

Aidha, mbali ya mapokezi hayo makubwa, jana aliwapokea wanachama wa upinzani
zaidi ya 700 waliojiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete aliingia kwenye mji wa Moshi saa 11.07 jioni kwa ajili ya kuwahutubia wananchi, waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini hapa, na alipata mapokezi makubwa pengine kuliko alivyotarajia.

“Nimehemewa,” lilikuwa neno la kwanza kwa Rais Kikwete alipopanda jukwaani ili
kuhutubia. “Leo ni full, nakuja hapa kila mara lakini haijapata kutokea kama hii. Uwanja wa Mashujaa leo umetapika.”

Akihutubia wananchi na kuomba kura, aliwabeza viongozi wa upinzani wanaodai kuwa CCM haijafanya lolote tangu Uhuru akihoji, “wakienda Karatu wanapita katika barabara zilizojengwa na CCM, na wengine ni maprofesa waliosomeshwa na Serikali ya CCM.”

Alieleza utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuelezea mafanikio makubwa yaliyofanyika
Moshi Mjini ikiwemo ujenzi wa barabara za lami; upanuzi wa sekta ya elimu na ukarabati wa Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Akiwa Vunjo, mbali na kuwataka wapinzani kutumia vema uhuru wa kutekeleza demokrasia, aliwapokea wanachama 750 kutoka Tanzania Labour Party (TLP); 10
kutoka Chadema na watano kutoka NCCR-Mageuzi.

Mgombea Ubunge wa CCM katika Jimbo la Vunjo, Crispin Meela alisema amewazoa wapinzani hao hasa baada ya kauli ya mgombea ubunge wa TLP, Augustino Mrema,
kumfananisha na kuku mtetea.

Katibu Kata ya Vunjo kupitia TLP ambaye alikuwa miongoni mwa waliojiunga na CCM, Valerian Mosha alisema amejiunga na chama tawala kwa sababu Rais Kikwete
ametekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi kwa kufanya mambo mengi mazuri, na
anastahili kupewa nafasi ya kuongoza tena nchi.

Naye mgombea ubunge Jimbo la Moshi Mjini ambalo kwa miaka 15 limekuwa chini ya
Philemon Ndesamburo wa Chadema, alisema wakati umefika kwa wakazi wa Moshi Mjini
kuirejesha CCM kuongoza jimbo hilo, kwani kwa miaka waliyoongoza na upinzani,
imewarudisha nyuma kiuchumi ikiwemo kufa kwa viwanda vingi na kudorora kwa
biashara, kiasi cha vijana wengi kuwa vijiweni.

No comments:

Post a Comment