Na Mgaya Kingoba, Njombe
MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Njombe Kaskazini, Deo Sanga, ameelezwa kuwa atakuwa mwakilishi mzuri wa wananchi wa jimbo hilo kwa sababu ametokana na
wananchi hao baada ya kusota nao katika dhiki.
Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo jioni katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika mjini Makambako na kumnadi mgombea huyo.
Rais Kikwete alisema Sanga ambaye ni maarufu kwa jina la Jah People, ni mtu aliyetokana na wananchi hao kwani ameishi maisha ya dhiki hadi kufika hapo alipo sasa akiwa ni mfanyabiashara maarufu mjini Makambako.
“Huyu ni mtu wa watu, mtu wa kazi. Ni mwenzenu, ni mtu aliyetokana na nyie, amepita katika dhiki hadi kufikia hapo. Atakuwa mwakilishi mzuri anayejua matatizo yenu,” alisema Rais Kikwete akimueleza Jah People.
“Ni mtetezi thabiti wa matatizo yenu. Anaweza kuwa mbunge mzuri. Namwamini, CCM inamwamini, mchagueni awe mwakilishi wenu.”
Kwa upande wake, Jah People ambaye pia aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Makambako na sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, alisema anaona kama anachelewa kuwawakilisha wananchi hao wa Njombe Kaskazini.
Akionekana mwenye furaha pengine kutokana na umati mkubwa uliojitokeza kwenye ‘uwanja wake huo wa nyumbani’, alisema “nashindwa niseme nini, mimi ni mtu wa kazi kwa vitendo.”
Aliwataka watu wa Makambako kumchagua Kikwete kuongoza tena Tanzania kwa sababu anawapenda Watanzania na amefanya kazi kubwa nzuri katika miaka mitano iliyopita.
Lakini zaidi akavigekia vyama vya upinzani na kueleza, “tusibabaike na vyama vya upinzani, havina mbele wala nyuma. Kazi yao ni matusi, hawana jipya. Tusikubali
kukipoteza chama kinachowajali watu.”
Awali, akihutubia mkutano huo, Rais Kikwete aliahidi kuwa Makambako itajengewa hospitali yake na watapata maji zaidi kwa sababu tayari kuna mradi mkubwa wa kuupatia maji mji huo maarufu.
No comments:
Post a Comment