9/15/2010

Mkutano wa Kampeni Rombo: JK amnadi Mramba Rombo, naye aja na kauli mbiu mpya
Na Mgaya Kingoba, Rombo

MBUNGE mkongwe wa Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro, Basil Mramba, ameibuka na kaulimbiu ya kutetea kiti chake hicho, akijifananisha na panga la zamani, lakini
likiwa na makali mapya.
Mbali na hilo, mwanasiasa huyo amewaeleza wapiga kura wake kwamba wasiache mbachao kwa msala upitao na mcheza kwao hutuzwa.
Mramba aliyewahi kushika madaraka ya uwaziri katika serikali za awamu zote nchini, amejitetea pia kutokana na umbile lake fupi, akiwaeleza wananchi kwamba wanapaswa kuwachagua watu wafupi ili wakawasimamie warefu.
Waziri huyo wa zamani aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti alipotambulishwa kwa wananchi katika mikutano ya kampeni jimboni kwake, na Mgombea Urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
“Nyie mnanifahamu, kazi zangu mnazifahamu. Nia ninayo, nguvu ninazo na uwezo ninao. Panga la zamani, lakini makali yale yale…msiache mbachao kwa msala upitao na mcheza kwao hutuzwa,” alisema Mramba.
Akimnadi Mramba, Rais Kikwete alisema mwanasiasa huyo ni mbunge wao wa miaka mingi, lakini akammiminia sifa kuwa ni mzee kijana, ambaye amekuwa na mawazo mapya wakati wote.
“Huyu kwa maneno ya mjini, ni Mzee Kijana, kwani ni mwenye mawazo mapya yenye manufaa wakati wote…siyo wale wazee ambao wakichoka la mbele linawekwa nyuma, la nyuma linawekwa mbele. Huyu ubongo wake unajadidika (renewal), ni chimbuko la maarifa mapya,” alisema Kikwete.
Awali, akielezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010, Mramba alieleza mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali, na kumshukuru Rais Kikwete kwa kuipatia barabara za lami Rombo; maji ya uhakika; kuipatia vocha za ruzuku za pembejeo na umeme vijijini.
Alisema katika miaka mitano ijayo, kazi kubwa ya Rombo ni kupambana na umasikini
wa watu katika kaya, na nia yao ni kuwawezesha wananchi ili kuondokana na umasikini na kujipatia kipato.

No comments:

Post a Comment