9/04/2010

Mkutano wa Kampeni Ngerengere JK: "Jeshi litaimarishwa Miaka mitano ijayo"

Na Mgaya Kingoba, Morogoro

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema Jeshi nchini litaimarishwa na kufanywa la kisasa katika miaka mitano ijayo.
Rais Kikwete aliyasema hayo leo wakati akihutubia mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, uliofanyika Ngerengere katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki mkoani hapa.
Kijiji cha Ngerengere kiko jirani na kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), inayohusika na masuala ya anga.
Rais Kikwete alisema ni nia ya serikali yake katika miaka mitano ijayo kulipatia jeshi silaha za kisasa, wanajeshi wanaofundishwa vizuri, wanaotunzwa vizuri na wanakaa katika nyumba nzuri.
“Ninyi hapa mko jirani na kambi ya Jeshi. Katika miaka mitano iliyopita, tulidhamiria kuliwezesha jeshi letu kufanya kazi zake vizuri, na hilo limewezekana,” alisema Rais Kikwete.
“Katika miaka mitano ijayo kufikia mwaka 2015, tunadhamiria kulifanya Jeshi letu kuwa la kisasa, kulipatia silaha za kisasa, wanajeshi waliofundishwa vizuri, wanaokaa vizuri. Hili tumedhamiria.”
Alisisitiza dhamira ya serikali yake ya kuendelea kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wake, akiwaahidi wakazi wa Ngerengere kuwa watapata maji ya uhakika kutoka mradi wa maji wa Mto Wami, Chalinze mkoani Pwani.
Aidha, alisema wilaya za Morogoro zitaendelea kupatiwa umeme na kwa mwaka huu zitapatiwa Kilombero, Kilosa na Ulanga.
Aliwanadi wagombea wa udiwani katika kata za jimbo hilo pamoja na mgombea wa ubunge, Dk. Lucy Nkya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
“Dk. Lucy Nkya namwamini, kama ningekuwa simwamini, nisingemfanya Naibu Waziri. Msiniangushe,” aliwaeleza wananchi wa Ngerengere.
Mbali ya mkutano huo, mgombea huyo wa CCM alifanya mikutano katika miji ya Mvuha, Matombo, kabla ya kuhitimisha siku ya kwanza ya kampeni zake mkoani hapa kwa kuhutubia kwenye Uwanja wa Jamhuri.

(tamati)

No comments:

Post a Comment