9/18/2010

Mkutano wa Kampeni za Mheshimiwa Kikwete Haydom

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na umati mkubwa wa watu alipowasili Haydom Wilayani Mbulu mkoani Manyara.


Mapokezi ya kishindo yamempokea Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Haydom wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara.




Msafara huo uliotekea Kata ya Dongobesh umeingia mnamo majira ya saa sita mchana na kupokelewa na msafara mkubwa wa magari na pikipiki hadi kwenye mji wa Haydom uwanja wa mkutano.




Akizungumzia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwenye kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbulu kupitia CCM Mheshimiwa Marmo alijivunia mitandao ya simu, TANROADS kwenye upande wa ujenzi wa barabara, ambayo yamerahisisha ufanywaji biashara kwa mazao ya biashara na vijiji jirani na hata mkoa jirani wa Arusha.




Mheshimiwa Marmo alizungumzia upanuzi wa huduma za afya ambapo alielezea zahanati zilizojengwa na vituo vya afya vilivyo imarishwa. Hospitali ya Haydom ya rufaa imeendelea kuhudumia wilaya zaidi ya nane na mikoa mitatu inayozunguka hospitali hiyo.




Naye Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi kwenye hutuba yake ya kampeni kwa wananchi wa Haydom, aliwasihi kuchagua CCM iendelee kuongoza kwa sababu ni chama imara kinachojali maendeleo ya watanzania wote.




Mheshimiwa Kikwete pia alielezea mafanikio ya elimu ya sekondari, ambapo azma ya CCM ya kujenga shule za sekondari kila kata, yamefanikiwa na kuvuka malengo. "inavyoelekea sasa tunaweza kuelekea sekondari moja kila kijiji maana kuna kata nyingine zina zaidi ya sekondari tatu kwa kata" alieleza.




Kwa upande wa afya, Mheshimiwa Kikwete alisema kuna hospitali saba zimetengwa na serikali kwa mpango maalum Haydom ni mojawapo. Nyingine ni St. Francis Itigi, Ndanda Mission Masasi, na nyingine nne, ziko kwenye mpango maalum ili ziwe kubwa na kuhudumia wakazi wa maeneo haya ya karibu na hospitali hizo.




Mheshimiwa Kikwete alieleza licha ya hospitali ya Haydom kuwa hospitali ya rufaa, hospitali kubwa ya mkoa itajengwa Wilaya ya Babati kwa ajili ya kutimiza azma ya serikali ya kujenga hospitali kwenye makao makuu ya kila mkoa.




Mengine yanayotarajiwa kufanywa na serikali ya CCM kwa miaka mitano ijayo ni utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya kilimo ili kuwasaidia wafugaji ili kuweza kupata na kutunza mifugo yao vizuri.




Kwenye upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Mheshimiwa Kikwete alisema japo serkali imevuka ahadi ya kutengeneza ajira milioni moja kwa vijana lakini tatizo bado ni kubwa. Jitihada zimeongezwa kufanya mengi zaidi kwenye upande wa utoaji mikopo na ajira kwa wananchi.




Mwishoni Mheshimiwa Kikwete aliwanadi wagombea wa CCM kwenye udiwani na ubunge.











No comments:

Post a Comment