9/26/2010

Mkutano wa kampeni Ukara - Ukerewe: JK atangaza wilaya mpya ya kipolisi Ukara

Na Mgaya Kingoba, Mwanza

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ametangaza kwamba katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika ziwa Victoria hususan wilayani Ukerewe, kunaundwa wilaya mpya ya kipolisi ya Ukara.

Amesema mipango imeanza na itakamilishwa karibuni na itasaidia kukabili vitendo hivyo vya uhalifu katika Ziwa Victoria ili liwe na amani na utulivu.

Rais Kikwete aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiomba kura za wananchi wa Ukerewe katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika miji ya Ukara na Nansio wilayani humo mkoani Mwanza.

Alisema serikali inatambua kuwapo kwa vitendo vya uhalifu katika ziwa hilo na ndio maana imechukua hatua kadhaa ikiwemo pia kutoa mafunzo maalumu kwa polisi na kuanzisha doria ziwani humo.

Aidha, alisema kutafanyika utafiti kuhusu zao la mihogo kukabiliwa na ugonjwa ambao umekuwa ukiwasumbua wakulima wa zao hilo.

Kwa upande mwingine, aliahidi kununua kivuko kipya cha Nyerere kwa ajili ya wakazi wa kisiwa hicho cha Ukara.

Katika hatua nyingine, ameahidi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Magu itaendelea kuboreshwa, na atafuatilia suala la upungufu wa dawa katika hospitali hiyo.

Alikiri pia kuwa maji bado ni tatizo kubwa mjini Magu na kwamba tayari Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat), litafanikisha mradi wa maji katika mji wa Magu na maeneo ya vijijini.

Akihutubia mikutano katika miji ya Kisesa katika Jimbo la Magu na Lamadi katika Jimbo la Busega, alizungumzia pia uboreshaji wa sekta ya mifugo na uvuvi wa kisasa ili kuwezesha wavuvi kuwa na maisha bora.

Mgombea huyo wa Urais wa CCM anatarajiwa kufanya mkutano mwingine mkubwa wa kampeni mjini Bariadi.

No comments:

Post a Comment