9/30/2010

Mkutano wa Kampeni Urambo: S. Sitta aongoza Wana Urambo, Wammwagia sifa JK

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!!
Kidumu Chama Tawala!
 
Na hivyo vingine?
Vinatuudhi!!

Hivi ndivyo wakina mama wa Urambo walivyokuwa wanaitikia mara muhamasishaji aliposema kidumu Chama Cha Mapinduzi. Ni katika shamrashamra za kumpokea Mwenyekiti wa CCM taifa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Msafara wa Mheshimiwa Kikwete umefika hapa Urambo mnamo majira ya saa nane mchana ukitokea Kaliua na Uyowa Ulyakhulu.

Akisoma mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM, mgombea ubunge wa jimbo la Urambo na Spika wa Bunge lililopita la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samuel Sitta alisema kwenye upande wa elimu miaka mitano iliyopita kulikuwa na shule mbili na sasa kuna shule 15, karibu kila kata ina shule na kata nyingine shule mbili za sekondari.

Kwa upande wa huduma ya maji vimejengwa visima 56 ambavyo vimejengwa karibu na shule za Uramboili kuhakikisha huduma hiyo inafika kwanza mashuleni. Awamu ya pili ya ujenzi wa visima hivyo, vitanjengwa kwenye maeneo ya watu na vijijini.

Akizungumzia upatikanaji wa umeme, Mheshimwa Sitta alisema kwenye kipindi cha miaka mitano ya Mheshimiwa Kikwete, umeme umefika vijiji vya Mabatini, Block Q, kuelekea Seedfarm, Mbaroni, Motomoto, kuelekea Usoke Milimani na Yelayela.

Mheshimiwa Sitta alichukua fursa hiyo kuomba huduma ya maji ya kutosha na kulingana na shughuli za kilimo za Urambo ambapo aliitaja kama kitovu cha uzalishaji wa zao la tumbaku nchini.

Mheshimiwa Sitta pia alizungumzia ujenzi wa barabara kutoka Manyoni, Itigi, kupita Urambo hadi Kigoma.

Alimalizia kwa kumuombea kura Mheshimiwa Kikwete na kuwasihi wana Urambo kutoka tarehe 31 Oktoba 2010 kwenda kupiga kura. Aliongeza, yeye kama mwanasiasa mkongwe anajivunia uongozi wa Rais Kikwete na kwamba hana mpinzani hapa Tanzania. Amelelewa vizuri na Mheshimiwa Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere.




Mwisho aliomba kura kwake yeye binafsi na kusema kwamba yeye ni chuma cha pua, na anaelekea kwenye kustaafu siasa, hivyo anaomba wana Urambo wasimuangushe. Alisihi kura hizo zisizidi za Mheshimiwa Kikwete ambazo ni 100%, alisema zake ziwe 97%.

No comments:

Post a Comment