9/29/2010

Mkutano wa Kampeni Nzega: JK akiri tatizo la maji Nzega, aahidi kuvuta maji kutoka Shinyanga kumaliza tatizo

Mipango imeanza ya kuvuta maji safi na salama kutoka Shinyanga ili kuhudumia wananchi wa Wilaya ya Nzega na vijiji vyake.

Hayo yamesemwa na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipowahutubia maelfu ya wananchi wa nzega kwenye mkutano mkubwa wa kampeni.

Akifafanua mpango huo mkubwa, Mheshimiwa Kikwete alianza kwa kukiri kuwa Nzega imekuwa ikisumbuliwa na tatizo hilo la maji kwa muda mrefu. "Nilipokuja mara ya mwisho niliahidi kulivalia njuga tatizo hili, na sasa mipango imekamilika ili mpate maji kutoka Shinyanga. Na hayataishia hapa, mabomba yatapita hadi Tabora Mjini" alisema Mheshimiwa Kikwete.

Ahadi nyingine alizozitolea ufafanuzi ni usambazaji wa umeme. Mheshimiwa Kikwete alisema japo Nzega Mjini kuna umeme, lakini baadhi ya vijiji bado umeme haujafika. Alisema kabla ya miaka mitano kuisha tatizo hilo litakuwa limeisha.

Mbali na umeme, Mheshimiwa Kikwete pia alisema barabara ya Nzega - Tabora Mjini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. 

Mheshimiwa Kikwete pia hakuacha kusisitiza janga la kitaifa la maradhi ya UKIMWI. Aliwaambia wana Nzega kuwa kwa sasa hapa Nzega watu 1,242 wanapata dawa za kurefusha maisha (wameathirika na maradhi ya UKIMWI). Aliwakumbusha watu wa Nzega kusikiliza ushauri wa viongozi wa dini ili kuupiga vita UKIMWI. Aliongeza ikishindikana kusikiliza mawaidha hayo, basi watumie kinga ili kuhakikisha wako salama.

Mwishoni Mheshimiwa Kikwete aliwaombea kura wagombea udiwani wa kata zote za Nzega, na baadaye kumnadi mgombea ubunge jimbo la Nzega, na yeye mwenyewe.

No comments:

Post a Comment