9/25/2010

Mkutano wa Kampeni Musoma Mjini: JK bado alia na barabara ya Serengeti

Na Mgaya Kingoba, Musoma


MGOMBEA Ubunge wa CCM katika Jimbo la Musoma Mjini, Mathayo Manyinyi ameitaka serikali ijenge haraka barabara ya Mto wa Mbu hadi Mugumu, huku Rais Jakaya Kikwete akisisitiza kuwa haitapita ndani ya Hifadhi ya Serengeti.

Aidha, Rais Kikwete amesema serikali itawashirikisha wanaopinga ujenzi wa barabara hiyo, lakini kwa sharti kwamba hawatazuia kuijenga.

Manyinyi alitoa ombi hilo kwenye mkutano mkubwa wa kampeni katika Uwanja wa Mukendo mjini hapa wakati akielezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2005-2010 jimboni humo.

Katika ombi lake kwa Rais Kikwete, Manyinyi alisema Musoma Mjini inakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa kwa sababu ya gharama za usafirishaji zinazosababishwa na ubovu wa barabara kufika mjini humo.

“Kuna tatizo kubwa la mfumuko mkubwa wa bei hapa kwa sababu bidhaa zinatoka Dar es Salaam, Tanga, Shinyanga, hivyo gharama za usafirishaji zimekuwa kubwa…tunaomba barabara ya Makutano – Loliondo hadi Mugumu ijengwe haraka,” alieleza Manyinyi.

Alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutasaidia kupunguza gharama hizo na kutoa unafuu mkubwa wa maisha kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini.

Akiomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo, Rais Kikwete mbali ya kusisitiza ujenzi wa barabara hiyo, alieleza kuwa kamwe haitapita katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Barabara hiyo itajengwa kutoka Mto wa Mbu mkoani Arusha kupita maeneo ya Ngaresero, kando ya Mlima Oldonyo Lengai, Loliondo, Clains Camp geti la Serengeti, Tabora B hadi Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara.

“Tutaijenga barabara hii, ingawa kumekuwa na maneno mengi ya upotoshaji. Haitapita ndani ya Hifadhi ya Serengeti kama baadhi ya watu wanavyodai. Kilometa
hamsini na tatu zitajengwa nje ya hifadhi,” alieleza.

“Kuna mwandishi namheshimu, juzi ameandika habari ya kupotosha ndani ya gazeti (analitaja jina), anasema barabara itapita ndani ya hifadhi. Tutafanya tathimini ya athari za mazingira na tutawashirikisha wote, lakini kwa masharti kwamba hawatazuia kujenga barabara hii.”

Akiwa Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, Ijumaa iliyopita, Rais Kikwete alisema ujenzi wa barabara hiyo una umuhimu kwa maslahi ya wakazi wa mikoa hiyo miwili ambayo haijaunganishwa kwa lami.

Hata hivyo, wanaharakati wengi wakiwa wa nje ya nchi wakiwemo wa Kenya, wanapinga ujenzi wa barabara hiyo kwa madai kwamba uhamaji wa wanyama unaojivunia hifadhi hiyo utatoweka; wanyama wengi watagongwa na kufa na Ngorongoro inaweza kuondolewa katika urithi wa dunia.

Mgombea huyo wa Urais wa CCM alimaliza mikutano yake ya kampeni mkoani Mara na kesho anatarajiwa kufanya mikutano katika miji ya Ukara, Nansio (Ukerewe); Nyanguge, Magu, Lamadi (Magu) na Bariadi (Shinyanga).

No comments:

Post a Comment