Wananchi wa kabila la Wairaq kutoka katika kijiji cha Galapo wa wakicheza ngoma wakati wa mkutano wa kampeni kijijini hapo ambapo Mgombea Urais kupitia CCM Rais Jakaya Kikwete alishiriki
Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mgombea Urais kwa Chama Cha Mapinduzi,CCM, akimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Babati vijijini kwa tiketi ya chama hicho Bwana Jitu Soni katika kijiji cha Galapo
Mamia ya wananchi wenye shauku na bashasha kubwa wa kijiji cha Galapo kilichoko katika jimbo la Babati Vijijini wakitafuta kila mbinu ya kushikana mikono na Rais Kikwete wakati alipotembelea kijijini hapo kwa ajili ya mkutano wa kampeni.
Wananchi wakulima wa Galapo, Babati vijijini Mkoani Manyara wamemzawadia Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Kilo 60 za mchele na lita 40 za mafuta ya alizeti kwa ajili ya chakula wakati wa kampeni.
Pamoja na zawadi hiyo ya chakula, wazee wa Galapo wamemkabidhi fimbo maalum ambayo wazee wa Mkoa huu huishika kama ishara ya uongozi. Nao wanawake wa mkoa huo wamemkabidhi mgolole kwa ajili yake na vitenge kwa ajili ya Mama Kikwete.
Alikabidhiwa zawadi hizo alipokuwa kwenye mkutano wake wa kampeni Galapo, ambapo ni kituo cha kwanza kwa siku ya leo lakini ndio kituo cha mwisho kwa Mkoa wa Manyara. Baada ya Galapo Mheshimiwa Kikwete ataingia Mkoa wa Dodoma na kuendela na mikutano ya kampeni mkoani Dodoma.
Akipokea zawadi hizo, Mheshimiwa Kikwete aliwashukuru wananchi wa Galapo na wa Mkoa mzima kwa ujumla kwa mapokezi mazuri na ukarimu wa hali ya juu kipindi chote cha kampeni.
Alifafanua pia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita akisema CCM ni Chama kinachotekeleza ahadi zake. Kwenye upande wa elimu sasa Babati ina shule za sekondari 32 ukilinganisha na shule 11 mwaka 2005. Sasa watoto 12,967 wanaenda sekondari ukilinganisha na wanafunzi 4800 mwaka 2005.
Kwenye upande wa malengo ya kuleta maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, Mheshimiwa Kikwete alizungumzia mpango wa kusambaza maji nchi nzima ambapo kwa hapa Babati vijijini utanufaisha vijiji 13.
Alizungumzia matarajio mengine 2010-2015 ni usambazaji wa umeme, utoaji wa huduma za afya, na uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji na utoaji ruzuku kwa wakulima.
Akizungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Mheshimiwa Kikwete alieleza jitihada za kurasimisha mali za wanyonge ambapo hadi sasa vijiji 72 vya Wilaya hii ya Babati vimekwisha pimwa. Utoaji hati za umiliki ardhi umewezeshwa kwa uongozi wa vijiji na hivyo kuwawezesha wananchi moja kwa moja.
Mwisho kabisa Mheshimiwa Kikwete aliwanadi wagombea wa CCM wa udiwani na ubunge na yeye mwenyewe kwenye kiti cha urais.
No comments:
Post a Comment