9/26/2010

Mkutano wa Kampeni Magu: Wana Magu wamshangilia

Msafara wa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete umewasili Magu Mjini wilayani Magu kwa mkutano wa kampeni.

Kabla ya Mheshimiwa Kikwete kuhutubia mkutano huo, katibu wa CCM Mkoa Bwana Alhaji Mwangi Kundya, alieleza kuwa wilaya hii ina majimbo mawili ya ubunge na wagombea wote ni madaktari. Changamoto iliyopo kwenye upande wa elimu ni ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita ili watoto wa Magu nao waweze kuingia elimu ya juu kupitia shule hizo.

Kwa upande wa afya alisema changamoto kubwa ni uhaba wa waganga na wauguzi na vifaa vya tiba. Katibu huyo aliomba kwa miaka mitano ijayo, suala hili lifanyiwe kazi.

Akizungumzia tatizo jingine la upatikanaji wa maji ambayo imekuwa ni kero ya muda mrefu, katibu huyo alimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kushirikiana shirika la Umoja wa Mataifa UN Habitat ambao wameshaanza kujenga matanki kwa ajili ya kuhifadhi na kusambaza maji Wilayani Magu.

Kwenye hotuba yake ya kampeni kwa wananchi wa Magu, Mheshimiwa Kikwete alifafanua mafanikio ya CCM kwa miaka mitano na kusema yote yaliyoahidiwa kwenye ilani ya 2005 yametimizwa. Hivyo CCM ni chama cha waaminifu kikiahidi kinatimiza.

Sababu nyingine aliyowasihi wana Magu kuchagua CCM ni kwamba CCM imeongoza nchi vizuri tangia uhuru hadi sasa. Alikiri kwamba nchi yetu bado changa na inaendelea kukua, lakini tulipo sasa hivi 2010 si sawa na tulipokuwa 2005, au 2000, au hata 1961 tulipopata uhuru.

Alizungumzia pia mpango mkubwa wa usambazaji wa maji kwenye mikoa ya kanda ya ziwa kwa kushirikiana na UN Habitat, shirika la Umoja wa Mataifa.

Mwisho aliwanadi wagombea udiwani wa Wilaya ya Magu na wagombea ubunge na yeye mwenyewe kama mwenyekiti wa CCM na mgombea Urais. Aliwasihi wasifanye makosa Oktoba 2010, kuchagua Chama Cha Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment