Mgombea ubunge wa CCM wa Jimbo la Rombo anayetetea kiti chake jimboni hapa Mheshimiwa Basil Mramba amemmwagia sifa nyingi Mheshimiwa Kikwete kwa kasi yake ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM na kuleta mafanikio mengi wilani Rombo.
Mheshimiwa Mramba aliyasema hayo kwenye mkutano mkubw awa kampeni Tarakea ambapo aliainisha kwa ufupi sana mafanikio hayo kwenye maeneo mbalimbali.
1. Ujenzi wa barabara ya lami; imeunganisha Rombo na wilaya ya Moshi Vijijini na maeneo mengine ya mipakani mwa wilaya. Barabara zote ni za kiwango kizuri na zinapitika wakati wote mwaka mzima.
2. Upanuzi wa Elimu ya Sekondari; Mwaka 2005 wakati ilani ya CCM iliagiza shule moja ya sekondari kwa kila kata Tanzania, Rombo ilikuwa tayari ina shule hizo. Lakini kwa nguvu ya utekelezaji wa ilani hiyo, Mheshimiwa mramba alisema kwa sasa Rombo ina Shule 41 za sekondari za kata. Shule kumi bora za mkoa wa Kilimanjaro, tano ziko Rombo. Aliongeza kuwa, mafanikio hayo yametokana na jitihada binafsi za wana Rombo kusambaza vitabu, walimu wa ziada waliomaliza kidato cha sita n.k. Kila mwaka wilaya ya Rombo inatoa zaidi ya wanafunzi 500 kwenda sekondari na 500 kuendelea na elimu ya juu. Mheshimiwa Mramba alisema mafanikio haya ni makubwa mno kwa ngazi ya wilaya na yasingetekelezwa kama si jitihada za Mheshimiwa Kikwete.
3. Upatikanaji wa Maji: Wilaya ya Rombo ni mojawapo ya wilaya chache Tanzania ambapo maji yanatiririka mwaka mzima kwa ujazo wakutosha.
4. Upatikanaji wa Umeme: Mheshimiwa Mramba alieleza umati mkubwa wa watu kwamba hivi karibuni wilaya ya Rombo itakuwa na umeme wa kutosha kutoka na mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA). Kuanzia mwisho wa mwaka huu, umeme utasambaa kwenye kila kitongoji wilaya ya Rombo.
5. Kilimo: Mafanikio makubwa yamepatikana kwenye kilimo cha kahawa na ndizi ambayo ndio mazao makuu ya chakula na biashara. Kuna mpango wa kuanzisha kilimo cha matunda kwenye ngazi ya kaya. Alisema jitihada hizi zitasaidia wakazi wa Rombo kujiongezea kipato na matunda yawe kama zao labiashara wilayani hapa.
6. Mwisho Mheshimiwa Mramba alimshukuru Mheshimiwa Kikwete kwa kusimamia ujenzi wa barabara kubwa ya lami inayopita wilayani Rombo. Na alitoa ombi kwa mheshimiwa Kikwete kusaidia katika jitihada za wana Rombo kupambana na umasikini kwenye ngazi ya kaya, ili kila Mtanzania wa Rombo aondokane na umasikini.
No comments:
Post a Comment