9/21/2010

Mkutano wa Kampeni Ismani: Lukuvi - Tumetekeleza Ilani ya CCM kwa zaidi ya 100%

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akimnadi Mgombea Ubunge wa Isimani Mheshimiwa William Lukuvi leo alipofanya mkutano mkubwa wa kampeni Isimani. Mheshimiwa Lukuvi ni mmoja wa wabunge waliopita bila upinzani kwenye jimbo lake.
Umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kumsikiliza mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipofanya mkutano wa kampeni Isimani.

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwa anashangilia kwa staili na mgombea ubunge wa Jimbo la Ismani Mheshimiwa Lukuvi jimboni hapo mara baada ya kumaliza kuhutubia mkutano mkubwa wa kampeni.Mgombea ubunge wa jimbo la Ismani aliyepita bila kupingwa Mheshimiwa William Lukuvi amesema utekelezaji wa ilani ya CCM kwenye upande wa elimu na afya Jimboni Isimani itekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100 kwa miaka mitano iliyopita.

Akizungumzia mafanikio ya CCM jimboni hapo na matarajio kwa miaka mitano ijayo, Mheshimiwa Lukuvi alisema japo Isimani ni jimbo jipya (1995), lakini huduma nyingi za jamii zimekuwa kwa kiwango na kasi ya ajabu hususan kwa miaka mitano ya Mheshimiwa Kikwete.

Kwenye upande wa elimu ya sekondari, Mheshimiwa Lukuvi alieleza jimbo lilipoanza hapakuwa na shule hata moja ya sekondari, lakini sasa kuna shule nane ambazo tano kati ya nane zimejengwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mafanikio mengine yaliyozungumziwa na Mheshimiwa Lukuvi ni kwenye upande wa afya ambapo alielezea karibu kila kijiji kuna kituo cha afya. Alielezea kwa sasa Isimani ina Zahanati 25 badala ya saba zilizokuwepo mwaka 2005.

Naye Mgombea Urais kupitia tiketi Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Jakaya Mrsiho Kikwete alichukua nafasi hiyo kufafanua mengine mengi yatakayofanywa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Aliwashukuru wananchi wa Ismani kwa kumpitisha mgombea ubunge wao kwa kishindo bila kupingwa. Aliwasihi kufanya hivyo kwa wagombea udiwani pamoja na yeye mwenyewe mgombea wa urais.

Baada ya kufanya mkutano wa kampeni Isimani, msafara wa Mheshimiwa Kikwete utaelekea Kalenga na Kilolo kabla ya kufika Iringa Mjini kwa mkutano mkubwa wa kampeni.

No comments:

Post a Comment